Pages

July 2, 2014

WANANCHI MANYARA WATAKIWA KUTUMIA HUDUMA ZA KIBENKI



 Na Mwandishi Wetu,Babati
Wananchi wa Mkoa wa Manyara, wametakiwa kutumia fursa ya kuwepo kwa huduma ya benki ya CRDB Tawi la Babati, kwa kujiwekea akiba na kuchukua mikopo kwa lengo la kujinufaisha kiuchumi na kuongeza pato la Taifa.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo aliyasema hayo wakati wa benki ya CRDB tawi la Babati, lilipoanza kutoa huduma ya fedha kwa wateja wake na yeye kuwa mtu wa kwanza kuweka fedha kwenye tawi hilo.

Mbwilo aliwataka wananchi wa mkoa huo kufungua akaunti za fedha kwenye benki tofauti ikiwemo CRDB, NMB, NBC, Posta na Exim, ambazo zipo mjini Babati, kuliko kuweka kwenye benki moja na kuitegemea yenyewe pekee.

“Waswahili wanasema usiweke mayai yote kwenye kapu moja, hivyo tutumie fursa hii kwa kuweka akiba katika benki tofauti tofauti, hapa unaweka sh200, kule sh300, pengine sh100 ndiyo nidhamu ya fedha ilivyo,” alisema Mbwilo.

Hata hivyo, alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda au Rais Jakaya Kikwete mmoja wao ndiye atakayekuja kulizindua rasmi Tawi hilo na alitoa wito kwa benki hiyo ya CRDB kuanzisha matawi mengine kwenye wilaya za mkoa wa Manyara.

“Siku za nyuma tulikuwa tunaona gari la benki linakuwa hapa kwa wiki mara moja ila sasa mmeweza kuweka Tawi hapa Babati, sambaeni na sehemu nyingine huko wilayani msogeze huduma hizi karibu na jamii,” alisema Mbwilo.

Naye, Meneja wa CRDB Tawi la Babati Ronald Paul aliwataka wafanyabiashara, watumishi, wakulima na wafugaji wa mkoa huo kutumia fursa ya kuwepo kwa benki hiyo kwa ajili ya kupata huduma za kifedha ikiwemo kuweka akiba.

“Jamii itumie nafasi hii kwa kuweka na kutoa fedha na pia hapa Babati ni kwenye barabara kuu hata viongozi wengi wanapita kuelekea Dodoma, hivyo watatumia fursa hii ya kuwepo kwa tawi letu kupata huduma ya fedha,” alisema Paul.


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...