Kwa ufupi
- Kwa mujibu wa mpango wa Serikali, barabara hiyo ingepitia Mto wa Mbu-Engaruka-Loliondo- Kleins Gate-Serengeti-Mugumu-Nata na kuungana na ile ya Tarime-Musoma-Mwanza, hivyo kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi wa maeneo haya ambao baadhi hulazimika kupitia Nairobi nchini Kenya.
Arusha. Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), imeizuia Serikali ya
Tanzania kujenga barabara ya lami kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
ikieleza kuwa ujenzi huo utaathiri mazingira, maisha ya wanyamawwpori na baoanuai
ya hifadhi hiyo.
Katika hukumu iliyotolewa jijini Arusha jana, jopo la majaji
watatu wa mahakama hiyo wakiongozwa na Jaji Kiongozi Jean Bosco Butasi,
liliiamuru Tanzania kutotekeleza mradi wowote wa ujenzi au ukarabati wa
barabara hiyo utakaokuwa na madhara kwa mazingira na baoanuai ya hifadhi ya
Serengeti.
“Zuio la kudumu linatolewa dhidi ya mdaiwa (Tanzania)
kutekeleza mipango ya awali au pendekezo la ujenzi au ukarabati wa barabara kwa
kiwango cha lami kupitia Hifadhi ya Serengeti itakayosababisha madhara
kimazingira na baoanuai ya hifadhi hiyo,” inasema sehemu ya hukumu hiyo.
Kila upande umeamriwa kubeba gharama zake katika shauri hilo
lililoshuhudia mgawanyiko kati ya taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali,
kwa yale ya Tanzania kuunga mkono ujenzi huo kwa madai kuwa una faida kwa
maisha na jamii inayoishi maeneo itakayopita barabara hiyo.
Kwa mujibu wa mpango wa Serikali, barabara hiyo ingepitia
Mto wa Mbu-Engaruka-Loliondo- Kleins Gate-Serengeti-Mugumu-Nata na kuungana na
ile ya Tarime-Musoma-Mwanza, hivyo kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi
wa maeneo haya ambao baadhi hulazimika kupitia Nairobi nchini Kenya.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya Taasisi ya Africa Network For
Animal Welfare (ANAW), ya jijini Nairobi, Kenya kufungua kesi dhidi ya Serikali
ya Tanzania kupinga ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 239, ikidai
itaathiri mazingira, uhai wa wanyama na baionuai wa Hifadhi ya Serengeti kwa
kuongeza shughuli za kibinadamu.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya majaji wenzake, Jaji Isaac
Lenaola alisema Serikali ya Tanzania ina haki ya kutunga sera na kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya umma, lakini sharti izingatie
upembuzi yakinifu kuepuka athari za kimazingira na baoanuai.
Jaji wa tatu katika jopo hilo ni Jaji John Mkwawa kutoka
Tanzania ambaye anakamilisha mkataba wake mwishoni mwa mwezi huu. Nafasi yake
tayari imejazwa na Jaji Fakih Jundu ambaye hadi uteuzi wake Aprili 30, mwaka
huu, alikuwa Jaji Kiongozi.
Hukumu hiyo inasema kuwa licha ya haki ya nchi zote wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupanga na kutekeleza miradi na majukumu
ya msingi kwa maendeleo ya wananchi, mipango hiyo lazima izingatie hoja ya
kidunia ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira, maendeleo endelevu, sheria na sera
za kimataifa kuhusu mazingira na maliasili.
Mahakama imekubaliana na hoja za walalamikaji waliokuwa
wakiwakilishwa kwenye shauri hilo na wakili Saitabao Ole Kanchory kuwa ujenzi
wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 239, ungeathiri mazingira na baionuai
ya Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya kwa kuwa
kungeongeza shughuli za kibinadamu.
Hukumu hiyo inasema kuwa licha ya ukweli kwamba Serikali ya
Tanzania ilipanga kuacha barabara yenye urefu wa Kilomita 53 inayopita ndani ya
hifadhi katika kiwango cha changarawe, bado magari mengi yangepita kwenye
barabara hiyo iwapo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa barabara hiyo ungetekelezwa ungekiuka ibara za
5(3), 8(1), 111(2) na 114 (1) ya mkataba wa EAC, zinazozungumzia wajibu wa kila
nchi mwanachama kupanga na kutekeleza sera na miradi yote iliyo chini ya
mamlaka na wajibu wao kwa kuzingatia ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwa faida
na masilahi ya jumuiya nzima.
Desemba
10, 2010, ANAW ilifungua shauri namba 9 ya mwaka 2010 dhidi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ya Tanzania na kutaja madhara kumi yatakayosababishwa na ujenzi wa
barabara hiyo, ikiwamo kusumbua wanyamapori katika maeneo yao ya asili,
ongezeko la magari, kelele na uchafuzi wa hewa.Madhara mengine ni uchafuzi wa maji kutokana na kumwagika kwa mafuta ya magari yanapoharibika, ongezeko la uwindaji haramu, ongezeko la vifo vya wanyama kwa kugongwa na magari na kupotea kwa uoto wa asili.
Mwanasheria Mkuu aliyekuwa akiwakilishwa kwenye shauri hilo na Wakili Pascal Malata ambaye jana aliwakilishwa na wakili wa Serikali, Marcelino Mwamunyange alipinga maombi hayo akidai tayari Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa kuepuka madhara hayo ikiwamo kufanya upembuzi yakinifu wa madhara ya kimazingira na njia ya kuziepuka.
Awali, Serikali iliweka pingamizi ikidai ANAW haikuwa na haki kisheria kufungua madai hayo na wala Mahakama haikuwa na uwezo wa kuyasikiliza kwa sababu mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia sheria halali za nchi na wajibu wa Serikali wa kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Pingamizi hilo lilitupwa na Mahakama.
Baada ya hukumu hiyo, Wakili Saitabao na wateja wake walielezea kufurahishwa na uamuzi wa Mahakama, waliodai ni ushindi mkubwa kwa wadau wote wa mazingira na ulinzi wa maliasili kwa ajili ya faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ni siku kubwa kwa uhifadhi wa mazingira na wananchi wote wa EAC. Vizazi vijavyo vina haki ya kuona na kufaidi maliasili hii tuliyoirithi na tutachukua hatua za kisheria dhidi ya serikali yoyote ndani ya EAC kupinga uharibifu wa mazingira,” alisema Wachira Benson, katibu wa ANAW.
Wachira alisema kesi hiyo haikulenga kuzuia miradi ya maendeleo ya Tanzania, wala taasisi yake haichukii Watanzania, bali walitimiza wajibu wa kutetea mazingira kwa faida ya umma wote wa Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa jumla.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment