Pages

June 23, 2014

MKUU WA MKOA WA ARUSHA,MAGESA MULONGO AYATAKA MABARAZA YA ARDHI KUEPUKA RUSHWA






Arusha.Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo ameyataka Mabaraza ya Ardhi  yaliyoanzishwa wilayani  Karatu na Ngorongoro  kujiepusha na vitendo vya kupokea rushwa ili kujenga imani kwa wananchi wanaopeleka mashauri yao kwao.

Wito huo ameutoa baada ya  kuwaapisha wajumbe saba wa mabaraza ya Ardhi ya wilaya hizo ofisini kwake jana,kuwa migogoro mingi ya ardhi inasababishwa  maamuzi yasizingatia ukweli uhalisia wa mwenye haki,jambo linaloongeza migogoro ya ardhi.

“Maeneo mengine migogoro ya ardhi ni kati ya wakulima na wafugaji ,lakini wilayani Ngorongoro ni wafugaji kwa wafugaji,mmepewa majukumu ya kuhakikisha mnasuluhisha kwa haki na kwa wakati,”alisema Magesa

Alisema inashangaza kuona migogoro ya ardhi inashindwa kutatuliwa katika ngazi ya Kijiji wakati kila mmoja  anafahamu eneo lenye mgogoro ni mali ya nani na nani anapaswa kulimiliki.

Magesa aliwataka wajumbe wanawake kuonesha uwezo wao  kisheria na kuwasaidia wajane ambao wamekua wahanga wa migogoro ya ardhi pindi waume zao wanapofariki dunia wanapata wakati mgumu kutetea haki zao.

Wajumbe walioteuliwa na kuapishwa kutoka wilaya ya Karatu ni Rukia Panga,Nicodemus Slagwe Iranghe,John Akunay na Peter Mushi wakati wajumbe wa wilaya ya Ngorongoro ni Pius Sanaya,Onesmo Marco na Josephine Ole Kashe

Kuapishwa kwa wajumbe hao kunawapunguzia wananchi kero ya kusafiri umbali mrefu kufika jijini Arusha kwaajili ya kutafuta haki zao huku wilaya za Arumeru na Longido wajumbe wake wakitarajiwa kuteuliwa siku za karibuni.


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...