Nasibu Abdul ‘Diamond Plutnumz’.
KUMEKUCHA! Unaweza
kusema kwa maana nyingine wakati wasanii kutoka Afrika watakapokuwa
pamoja kwenye Ukumbi wa Nokia Theatre uliopo Los Angeles, Marekani
katika sherehe za utoaji tuzo za BET 2014 kesho Juni 29.
Macho na masikio yote yameelekezwa kwa mtu mmoja kutoka Tanzania ambaye ni Nasibu Abdul ‘Diamond Plutnumz’.
Wapo wanaofurahia mafanikio yake na wengine kuchukia na kuona kama anapendelewa.
Katika makala haya yanachambua safari nzima
za tuzo ambazo ameshashiriki na anazoendelea kushiriki kwa
sasa; Awashangaza Watanzania
Aliivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na
mwanamuziki Abass Hamis Kinzasa ‘20%’, ya mwaka 2011 ambayo
alijinyakulia tuzo tano kwa mpigo zilizotambulika kama Kilimanjaro Music
Awards 2011.
Katika tuzo za Kilimanjaro za mwaka 2014
zilizofanyika Mlimani City jijini Dar, Diamond aliondoka shujaa kwa
kujizolea tuzo saba kwa mpigo na kuweka rekodi ya aina yake huku maswali
mengi yakibaki midomoni mwa watu na hata wengine wakidhani amebebwa na
hakustahili kupewa tuzo hizo zote.
Mpaka Diamond anaelekea Afrika Kusini Juni 7
mwaka huu, alionekana kama msanii anayeongoza kwa kupigiwa kura nyingi
na mashabiki akiwa na asilimia zaidi ya 60. Watanzania wengi walijua
ataibuka kidedea.
Wakati
wa ufunguzi wa tuzo hizo alianza kwa kufanya shoo ya nguvu akiwa
sambamba na mwanamuziki kutoka Nigeria, Davido. Walilivaa jukwaa na
wimbo wa My Number One Remix.
Hata wale ambao hawakujua lugha ya
Kiswahili aliyokuwa akiimba Diamond katika wimbo huo walionekana
kumfurahia kwa kucheza naye pamoja.
Kilichokuja kufanyika wakati wa utoaji wa
tuzo hizo, Diamond hakuambulia kitu chochote. Tuzo zilimpita machoni na
kukimbilia kwa wasanii kama Davido, Tiwa Savage, Uhuru pamoja na
Mafikizolo.
Atatoka katika tuzo za BET 2014?
Habari kila kona ni siku ya kesho
Juni 29, katika utoaji tuzo za BET 2014 ambapo Diamond ameingia katika
kategori ya Mwanamuziki Bora wa Kimataifa kutoka Afrika akiwa sambamba
na Sarkodie (Ghana), Mafikizolo (Afrika Kusini), Davido (Nigeria),
Toofan (Togo) na Tiwa Savage (Nigeria) ambao wote kwa pamoja
wameshaning’iniza kwapani tuzo za MTV Afrika 2014 na za BET 2012 kasoro
Diamond kutoka Tanzania.
Swali gumu la kujiuliza ni jinsi mpangilio mzima uliopangwa na waandaaji wa tuzo za BET 2014 zitakazofanyika kesho.
Wakati wale waandaaji wa MTV Afrika
2014 walimpa Diamond nafasi ya kupafomu wimbo wake kwa kushirikiana na
Davido, mambo yamekuwa tofauti kwa BET 2014.
Wamewakusanya wasanii wengi kutoka
Nigeria mbaya zaidi ni wale wanaoshirikiana naye katika kugombea tuzo
hizo ambapo kesho watapanda jukwaani kwa pamoja na kuimba wimbo maalum
unaohusu Afrika.
Wasanii hao ni pamoja na Sarkodie kutoka Ghana, Mafikizolo kutoka Afrika Kusini, Tiwa Savage na Davido wote kutoka Nigeria.
Abakiza tuzo mbili tu
Bado anayo nafasi kubwa ya kusonga
mbele na kugombea tuzo mbalimbali za kimataifa hata kama katika tuzo za
BET atazikosa kesho. Mpaka sasa amebakiza tuzo mbili ambazo ni AFRIMMA
2014 na zile za KORA Africa 2014.




Post a Comment