HALMASHAURI YA WILAYA YA KARATU YAPINGWA NA JAMII ZA WADZABE NA DATOGA


Mjumbe wa Bodi ya Lake Eyasi Culture Tourism Programme,Ushoka Kidobadi
Na Filbert Rweyemamu,Arusha
Jamii za Wadzabe na Watatoga  kwenye bonde la Eyasi wanaoishi kwa kutegemea mapato yanayotokana na utalii wa utamaduni kwenye maboma yao wamepinga mpango wa halmashauri ya wilaya ya Karatu kuanzisha sheria itakayoipa mamlaka ya kuendesha shughuli za utalii huo.



Wakizungumza kwenye mkutano wa wadau wa utalii wa kiutamaduni juzi katika Kijiji cha Qangded Kata ya Baray walisema wanaipinga sheria hiyo isisainiwe na Waziri Mkuu,Mizengo Pinda kwasababu itaharibu kabisa utalii wao ambao wanautegemea kama njia kuu ya mapato na kudumisha mila na desturi zao.



Mwenyekiti wa muda wa Lake Eyasi Cultural Tourism Programe,Issa Ngimba alisema Programu ya Utalii wa kiutamaduni ilipata baraka na inaratibiwa na bodi ya Utalii nchini(TTB)na utaratibu wa sasa kila gari la watalii linalipa Sh 30,000 wakati halmashauri ya wilaya inapata Sh.7,500 na pesa nyingine zinaenda kwenye ofisi za vijiji vitatu ambako utalii unafanyika.



Sehemu ya tangazo hilo inasema, Ada za utalii zitatozwa katika katika maeneo ya utalii zitakua ni moja ya chanzo cha mapato cha halmashauri pamoja na maendeleo ya kijiji tu na si kwaajili ya makundi maalum kama Tatoga,Wahunzi na Hadzabe na baada ya kukusanywa asilimia 20 itarudishwa kwenye kijiji kilichohusika na utalii huo.



Katika viwango vya halmashauri inapendekeza kila mtalii wa nje ya nchi atalipa Sh.15,000 wakati awali walikua hawalipi bali gari tu ndio lilikua linatozwa huku watalii wanafunzi wa nje watatozwa  Sh.7,500 na halmashauri ndio ita waajiri waongoza watalii jambo wanalolipinga.



Hata hivyo mmoja wa wajumbe wa bodi ya Lake Eyasi Cultural Tourism Programe,Ushoka Kidobadi alisema hawaamini kama halmashauri itarudisha asilimia 20 kwao kwani tangu halmashauri imeanza kutoza dola tano haijawahi kurejesha kwa wananchi kiasi chochote.



“Hatuko tayari kuunga mkono halmashauri yetu katika hili jambo,sisi tunatumia muda mwingi kukaa kwenye maboma yetu kuelimisha watalii halafu wao wanataka kubinafsisha utamaduni wetu kwa kisingizio cha kuongeza mapato ambayo hata hayatusaidii wananchi.”alisema



Ginyanyi Gisulu alidai iwapo halmashauri itang’ang’ania uamuzi wake,wao hawatatoa ushirikiano kwa waongoza utalii na hawatawaruhusu kufika kwenye maboma yao kwani kiwango kipya ambacho halmashauri inakusudia kutoza kitapunguza watalii na hawataweza kununua zawadi za kiasili kwenye maboma yao.



Alisema jamii ya wadzabe ambao hutegemea uwindaji na kuchimba mizizi,watalii ndio chanzo cha mapato yao yanayowasaidia kulipia gharama za matibabu,elimu na kununulia chakula hivyo kuona mpamgo huo kama wenye lengo la kurudisha nyuma maendeleo yao.
Mwanzilishi wa Utalii wa Utamaduni kwenye bonde la Lake Eyasi wilayani Karatu,mkoa wa Arusha,Momaya


Wanawake wa jamii wa Tatoga wakifatilia mkutano

Wajumbe kutoka jamiiya Kihadzabe na Tatoga wakiwa kwenye mkutano

Post a Comment

أحدث أقدم