Pages

August 11, 2013

UJANGILI UNAVYOITESA TANZANIA

tembo 5c70e
Wakati Taifa likididimia katika umaskini wa kutisha, wanyama ambao ni kitega uchumi cha nchi wanauawa kila siku na kundi la watu wenye uchu wa fedha.

Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo, baada ya Botswana.
 
Hata hivyo, ripoti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (Tawiri), inaonyesha kuwa tembo 30 wanauawa kila siku katika mbuga mbalimbali hapa nchini. (HM)

 
Tawiri inaeleza kuwa miaka ya 60, Tanzania ilikuwa na tembo kati ya 250,000 hadi 300,000, lakini mpaka kufikia mwaka 2011, kuna tembo 70,000.
 
Utafiti uliofanyika umebaini kuwa upotevu huu wa tembo, unafanywa na genge la maharamia wenye mtandao uliojisuka hadi serikalini.
 
Imebainika kuwa mtandao huo ni mgumu kuuvunja kwani unahusisha wanasiasa, askari wa wanyamapori, polisi, mahakimu, raia wa nchi jirani, raia wa China, Thailand na Vietnam pamoja na wafanyabiashara wakubwa nchini.
 
Mara kadhaa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki amekaririwa akikiri kuwa ujangili wa pembe za tembo unahusisha mtandao mkubwa, wakiwemo wanasiasa.
 
"Kwa bahati mbaya sana, mtandao wa majangili wa pembe za tembo unahusisha wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa," alisema. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya watu wanaufahamu ukweli, lakini wanaogopa kuwataja wanasiasa hao kwa sababu za kiusalama.
 
Taasisi za wanyama pori zinashindwa kufanya kazi vyema na kuwataja wahusika wa genge hilo, kwa sababu wamo wanasiasa wakubwa.
 
Ripoti iliyosomwa bungeni hivi karibuni inaonyesha kuwa, baadhi ya makada wa CCM wanahusika katika ujangili wa pembe za tembo kwa kumiliki vitalu 16 vya uwindaji kinyume cha sheria.
 
Ripoti hiyo iliyosomwa na Chadema inamtaja mmoja wa mnakada wa chama tawala CCM, kuhusika na tuhuma za ujangili wa meno ya tembo katika ngazi za kimataifa.
 
Ilibainika kuwa kada huyo anamiliki kampuni za vitalu kwa majina tofauti, ili kuficha kuwa ni za mmiliki mmoja.
 
Kada huyo aliyewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, ametajwa katika ripoti hiyo kuwa jangili wa kimataifa.
 
Allan Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Wanyama Pori (Tanapa), alikiri kuwa mtandao wa ujangili ni mkubwa na unahusisha watu wanaotumia silaha za kivita.
 
Kijazi alisema, kinachoikwamisha Tanapa ni mtandao mpana, silaha na watuhumiwa kuachiwa kinyemela baada ya kukamatwa.
 
Bandari ya Dar es Salaam
Ripoti iliyotolewa Juni 2013 na Taasisi ya Ulinzi wa Tembo Tanzania (TEPS), inaeleza kuwa Bandari ya Dar es Salaam ndicho kituo kikuu Afrika kinachotumika kusafirisha pembe za tembo kuelekea China, Vietnam, Japan, Ufilipino na Thailand.
 
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa mtandao wa ujangili una watu wake katika Bandari ya Dar es Salaam, ambao hushiriki kuipitisha mizigo ya pembe za tembo bila kugundulika.
 
Biashara hii inaendelea kukua nchini kutokana na nchi za Bara la Asia kuwa na soko kubwa la pembe hizo, ambayo hutumika katika tiba za asili na urembo.
 
Ripoti ya CITES iliyochapishwa Juni 2012, inaonyesha kuwa utoroshwaji wa makontena makubwa ya meno ya tembo huondoka Bara la Afrika kupitia Bahari ya Hindi hasa katika Bandari za Dar es Salaam na Mombasa.
 
Kinachozua maswali, ni kwa nini makontena mengi yanapita katika bandari hizo bila kugundulika, lakini hushikwa katika bandari nyingine kama Vietnam, Thailand, China na Ufilipino?
 
Kwa mfano, Januari 2009, mzigo mkubwa wa pembe za ndovu uliondoka salama Bandari ya Dar es Salaam, lakini ulikamatwa Machi 5, Vietnam katika Bandari ya Hai Phong.
 
Makontena hayo, yaliyobandikwa lebo kuwa ni taka za plastiki za kurejelezwa, maafisa wa Bandari ya Hai Phong waligundua tani sita za meno ya tembo.
 
Machi 2 na Machi 5, kontena lingine ziliwasili katika Bandari ya Manila Ufilipino.
 
Makontena hayo yaligundulika baada ya kukaa bandarini kwa wiki sita, bila mwenye mzigo kuuchukua.
Katika mzigo huo ambao ulikuwa na kiasi cha tani tano za pembe za tembo uligundulika kuwa umetoka Tanzania.
 
Kwa kontena zote tatu zilizokamatwa katika kipindi cha mwaka 2009 na 2010, wakala wa usafirishaji alibainika kuwa ni Kampuni ya Puja.
 
Hata hivyo, utafiti ulibaini kuwa haijasajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela), wala Wakala wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini,(Sumatra).
 
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema apewe muda wa kulifanyia kazi suala hilo.
 
Mtandao usioshikika
Chanzo kimoja cha habari kilibainisha kuwa, biashara ya pembe za tembo ni vigumu kwisha nchini kwa sababu inahusisha watu kutoka serikalini, askari wa wanyamapori, raia wa kigeni(Wasomali, Wachina na Warundi).
 
Alisema baadhi ya askari wa wanyamapori ndiyo huwaua tembo au kuchukua pembe hizo kutoka chumba yanapohifadhiwa, 'ivory room' (pembe zilizopatikana kutoka kwa tembo waliojifia) na kuyauza.
Alisema polisi au askari wa wanyamapori ambao hulipwa, hutakiwa kuwapasha habari ya mipango inayofanywa na Serikali au kuwaachia wahusika wanaposhikwa.
 
"Polisi wengine wenye vyeo wanapata malipo ya kila mwezi kwa kiasi cha Sh 5,000,000 hadi 7,000,000 kwa mwezi," kilisema chanzo hicho.
 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema, mtandao wa ujangili ni mkubwa na umejichimbia mizizi.
 
Alisema mtandao huo unahusisha wanajeshi, baadhi ya watumishi wa serikali, wafanyakazi wa bandari na baadhi ya askari wa wanyama pori.
 
"Ingawa tunajitahidi kupambana na ujangili huu, lakini vita yake ni ngumu kwa sababu tunapambana na watu wenye silaha za kivita, wenye pesa na wanapeana taarifa," alisema Nyalandu.
 
Jinsi uharamia unavyofanyika
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa maharamia wa ngazi ya chini huingia katika maeneo ya hifadhi na kulala katika nyumba za wageni.
 
Wakiwa hapo wanaweza kukaa kwa kipindi cha wiki mbili hadi mwezi mmoja. Katika kipindi hicho wanaweza kuua tembo 10 hadi 20.
 
Mtandao huu ni kama biashara ya fedha ambapo fedha huzunguka na mtu wa mwisho atakayeishika ni vigumu kujulikana.
 
Maharamia wa ngazi ya chini hupata wateja kutoka Dar es Salaam ambao nao pia huwa na wateja wao wakubwa.
 
Inaelezwa kuwa shughuli za uuaji wa ujangili hufanyika zaidi nyakati za mvua na msimu ambao hakuna watalii wengi.
 
Maharamia wakubwa ambao mara nyingi ni wafanyabiashara wakubwa na wanasiasa, huuza pembe hizo kwa raia wa Bara la Asia, hasa hasa China, Ufilipino, Thailand na Vietnam.
 
Mkurugenzi wa Mahusiano wa Mtandao wa Kusimamia Biashara ya Wanyamapori (TRAFFIC), Dk Richard Thomas alizungumza na Mwananchi Jumamosi na kueleza kukiri kuwa kuna uhusiano kati ya nchi za Afrika na watu wachache kutoka Hong Kong, Malaysia, Ufilipino na Vietnam wanaohusika katika ujangili huu.
 
"Ripoti ya Machi 2013 ya mkutano wa ETIS inaeleza jinsi ambavyo Tanzania inatumika kama njia kuu ya kupitisha pembe za tembo kuelekea Asia," alieleza Dk Thomas.
 
Wauzaji wengine wa meno ya tembo katika ngazi ya chini ilibainika kuwa wamejiwekea makazi yao eneo la Mwenge kwa wachonga vinyago vya Kimakonde.
 
Eneo la Mwenge unaweza kupata bidhaa zilizotengenezwa kwa pembe za tembo kuanzia hereni, cheni na vidani.
 
Pia unaweza kupata pembe ambazo hazijatengenezwa bado(raw ivory) na mara nyingi huwa yametundikwa katika paa au chini ya ardhi.
 
Wafanyabiashara hao bila kufahamu walisema hupata pembe hizo kutoka kwa maofisa wa Hifadhi za Ugalla, Selous na Serengeti.
 
Maharamia wakuu wanaozitoa pembe hizo kwenda nje, wamejenga mtandao mwingine na watu wa bandari na baada ya mzigo kupitishwa wapokeaji ambao ni nchi za Asia, huipokea mizigo hiyo.
 
Pia wapo 'watu kati' ambao wao husambaza fedha kwa maharamia wadogo ambao huwaletea pembe. Baada ya kukusanya pembe za kutosha, huuzwa kwa wafanyabiashara wakubwa ambao nao huyauza nchi za nje.
 
Bei
Bei hutofautiana kuanzia katika ngazi ya kijiji, hadi kwa wauzaji wakubwa wa kimataifa.
 
Wauzaji wa ngazi ya chini hupanga katika nyumba za wageni au hoteli zilizopo katika maeneo ya hifadhi.
Wakiwa hapo husubiri meno kutoka kwa wakala wao ambao ni wanakijiji.
 
Wauzaji huweza kuuza kilo moja ya pembe za tembo kwa kiasi cha Sh45,000 hadi Sh 80,000. Baada ya wanunuzi kupata pembe wanazohitaji huzisafirisha kwenda Dar es Salaam kwa kutumia mabasi au magari ya Serikali.
 
Chanzo cha habari kilibainisha kuwa wakati mwingine wanajeshi, polisi au askari wa askari magereza huweza kununua pembe kwa sh 25,000 iwapo wametoa silaha kwa majangili.
 
Wafanyabiashara wakubwa hununua pembe hizo kwa gharama kubwa zaidi na huyauza kwa gharama zaidi nje ya nchi katika 'black market'
 
Bei ya pembe za tembo katika soko la dunia kwa sasa ni kiasi cha Dola za Marekani 2,000 (sawa na 3,200,000) kwa kilo. Chanzo: mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...