Rais wa Marekani,Baraka Obama na Waziri Mkuu wa Uingereza,David Cameron |
Marekani na Uingereza zimeongeza
shinikizo kwa Urusi juu ya mgogoro wa Syria, lakini rais Barack Obama ameonya
kuwa hakutakuwa na suluhisho la haraka la mgogoro huo, huku jeshi la Assad
likipata mafanikio zaidi.
Obama na waziri mkuu wa Uingereza
David Cameron walitaka kujenga hamasa mpya nyuma ya mkutano wa kimataifa wa
Syria unaodhaminiwa na Marekani na Urusi, ambao sasa unatarajiwa kufanyika
mwezi Juni, wakati wawili hao walipokutana mjini Washington.
Cameron, akiwa ndiyo amekamilisha
ziara nchinin Urusi, alisema anaamini London, Washington na Moscow wamepata
muafaka juu ya mgogoro wa Syria, ambao umegharimu maisha ya maelfu ya watu.
Obama alisema Urusi ina maslahi na wajibu wa kusaidia kukomesha mgogoro huo,
akisema alikuwa amewasilisha ujumbe kwa rais Vladmir Putin kabla ya ziara ya waziri
wake wa mambo ya kigeni mjini Moscow wiki iliyopita.
Hali bado ni ngumu sana Syria
Lakini, Obama alionya kuwa itakuwa
vigumu sana kuishawishi Urusi kubadilisha msimamo wake, na kubainisha kuwa bado
kuna tofauti za msingi kati ya nchi hiyo na mataifa ya magharibi. Obama alisema
hata kama Urusi itashawishika na kusimama upande wao, hali nchini Syria bado ni
ngumu sana kutokana na ushiriki wa Iran, kundi la Hezbollah na wapiganaji walio
na mafungamano na mtandao wa Al-qaeda katika mgogoro huo.
"Siahidi kuwa kutakuwepo na
mafanikio. Ukweli ni kwamba miungu ya ghadhabu ikishaachiwa katika hali kama
tunayoshuhudia nchini Syria, inakuwa vigumu sana kuweka tena mambo sawa,"
alisema Obama.
Cameron aonyesha matumaini
Kwa upande wake, waziri mkuu Cameron
alikuwa mwenye matumaini zaidi, akisema anaamini London, Washington na Moscow
zimefikia muafaka juu ya mgogoro huo. Cameron alisema kuwa historia ya Syria
inaandikwa kwa kutumia damu ya raia wa nchi hiyo, huku dunia ikitizama tu, na
kuongeza kuwa wakati umefika kwa dunia kuja pamoja na kukomesha umuagaji huu wa
damu. Cameron pia aliahidi kuongeza msaada usio wa kijeshi kwa baadhi ya
makundi ya waasi nchini Syria kwa mara mbili katika kipindi cha mwaka ujao.
"Kama hatuusaidii upinzani
nchini Syria ambao tunautambua kuwa halali, na uliosaini tamko kuhusu
mustakabali wa Syria yenye kidemokrasia, inayoheshimu haki za wachache,
tusipofanya kazi na upande huo, basi tusishangae kuona makundi yenye itikadi
kali yakizidi kuongezeka," alisema Cameron.
No comments:
Post a Comment