Pages

May 30, 2013

MWILI WA ERNEST ZULU WAREJESHWA NYUMBANI LEO

Thursday, May 30, 2013

Waombolezaji wakitoa mwili wa marehemu Zulu kuiingiza kwenye gari
The late Ernest Zulu
MWILI wa Ofisa Habari Mkuu wa Bunge, Ernest Zulu (56) aliyefariki Mei 23 mwaka huu nchini Malaysia alikokuwa masomoni, umewasili nchini majira ya saa 1.30 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar.

Majira ya mchana mke wake Theresia Zulu na watoto wake walifika kumtambua marehemu na kisha kundi la waombolezaji lilimsindikiza marehemu katika gari  ili kuanza safari yake ya mwisho kabla ya kwenda kupu
mzika milele kijiji kwao ndilima, Songea vijijini.

Kwa wakazi wa dare s salaam Zulu ataagwa kesho nyumbani kwake Ubungo Kibangu.

Baadhi ya watu waliokuwapo mchana wa leo uwanja wa ndege kuupokea mwili wa Zulu ni Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na waumini wa Kituo cha Maombezi cha Marian Ubungo, wakiongozwa na Padri Felician Nkwera.

 Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa marehemu ambaye hakuwa tayari kutaja jina gazetini , Zulu alikutwa  damu zikimtoka sehemu ya kichwa na kuegama mezani akiwa ameshika msalaba na picha ya Bikira Maria vilivyokuwa chumbani.

Awali, taarifa ya Katibu huyo kuhusu kifo hicho, iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge, Dodoma ilieleza kuwa Zulu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kichwa kwa muda mrefu.

Zulu aliyeacha mjane na watoto wanne, Philomena, Maria Emmaculate, Felistas na Augustina,  alikuwa nchini Malaysia, akisoma Shahada ya kwanza ya Mawasiliano na Usimamizi wa Vyombo vya Habari katika Chuo Kikuu cha Taylor tangu Julai 2010, na alitarajiwa kumaliza masomo yake Julai, mwaka huu.
Alizaliwa Julai 10 mwaka 1957 huko Songea. 

Alipata elimu ya msingi na sekondari Songea kabla ya kusomea uandishi wa habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari (TSJ) (sasa SJMC-UDSM) jijini Dar es Salaam.

Aliwahi kufanyakazi katika Shirika la Utangazaji la Tanzania (RTD) sasa TBC Taifa mwaka 1976 kama Mwandishi wa Habari Msaidizi na hatimaye kupandishwa cheo kuwa Mwandishi wa Habari kabla ya kuhamia Shirika la Magazeti la Chama (Uhuru na Mzalendo) kama Mwandishi Mwandamizi mwaka 1985. 

Mwaka 1986 hadi 1987 alipata fursa ya kusomea masomo ya Uandishi wa Habari ya Kimataifa huko nchini Urusi. Mwaka 1991 aliajiriwa kama Mhariri Msaidizi katika gazeti la The Express kabla ya kujiunga na Sauti ya Ujerumani ambapo alifanya kazi kama Mwandishi Mwandamizi kuanzia mwaka 1995.

 Aliajiriwa na Bunge mwaka 1998 kwa cheo cha Ofisa Habari Mwandamizi, mpaka mauti inamkuta alikuwa Afisa Habari Mkuu Daraja la Pili.
CHANZO JUMAMTANDA BLOG

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...