MAMENEJA TARURA WATAKIWA KUKAGUA MADARAJA, MAKALAVATI KABLA YA MVUA ‎

Mameneja wa mikoa na wilaya wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wametakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya barabara ikiwemo madaraja na makalavati ili kuhakikisha inabaki salama wakati wa mvua za El Nino.
‎Akizungumza mwishoni mwa wiki na Menejimenti na wafanyakazi wa TARURA mkoa wa Arusha, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema ni muhimu kufanya ukaguzi katika maeneo yote kuanzia ngazi za chini na kutoa taarifa makao makuu kuhusu maeneo yaliyo katika hatari.
‎"Mnatakiwa kuhakikisha barabara zote muhimu ambazo wananchi wanatumia katika shughuli zao za kila siku na kuwaingizia kipato zinabaki salama na kupitika kabla, wakati na baada ya mvua",  amesema.
‎Amesisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha usalama wa watumishi wanaokwenda kufanya ukaguzi wa miundombinu wakati wa mvua pamoja na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali.
‎Aidha, Mhandisi Seff amewataka mameneja wote kuwasilisha mipango ya utayari wa kukabiliana na mvua za El Nino ikiwemo kuainisha wakandarasi waliopo karibu na maeneo yao ili uharibifu utakapotokea hatua za kurejesha miundombinu zichukuliwe haraka na wananchi waendelee kupata huduma muhimu.
‎Kwa upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mameneja wa Mikoa wa TARURA, Mhandisi Nicholous Francis amesema wamepokea maelekezo hayo na wameanza kuchukua hatua za maandalizi kwa kushirikiana na mameneja wa wilaya.
‎Amesema moja ya hatua hizo ni kukagua maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kukumbwa na mafuriko na kuunda timu kuanzia ngazi za chini zitakazobaini maeneo hatarishi.
‎"Maeneo ambayo yanapata mvua nyingi na kubainika kuwa hatarishi tutayafunga na kutoa njia mbadala ambazo wananchi watataarifiwa kuzitumia", amesema.
‎Hata hivyo, Mhandisi Francis amewakumbusha wananchi kuwa maji hayapimwi kwa macho na kuwataka kutovuka barabara endapo watakutana na maji mengi yanayokatiza njia.
‎Pia amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto hawachezi kwenye makorongo au maeneo mengine hatarishi wakati wa mvua.
‎Aidha, amewaomba wamiliki wa shule zinazotumia magari kuwachukua wanafunzi kufanya marekebisho ya ratiba za kuwachukua na kuwarudisha watoto majumbani hasa nyakati za alfajiri na usiku katika kipindi chote cha mvua ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.












 

Post a Comment

أحدث أقدم