Wananchi wametakiwa kuachana na dhana potofu kuwa chakula kinachopikwa kwa gesi ya LPG hakina ladha kama cha kupikwa kwa mkaa, huku ikielezwa kuwa tafiti zimebaini hakuna tofauti ya ubora wa chakula kinachopikwa kwa kutumia nishati hizo mbili.
Hayo yameelezwa na Afisa wa Ufundi wa Chama cha Wadau wa Gesi Tanzania TZLPGA, Mhandisi Huruma Msigwa, Mei 22, Jijini Dodoma, wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM kuhusu matumizi salama ya gesi ya LPG pamoja na fursa zilizopo katika sekta hiyo inayozidi kukua nchini.
Mhandisi Msigwa ametoa wito kwa jamii kuondokana na mtazamo potofu kuwa matumizi ya gesi ni hatari zaidi kuliko mkaa, akieleza kuwa ajali nyingi zinazohusishwa na gesi husababishwa na matumizi yasiyo sahihi pamoja na kukosa elimu ya matumizi salama ya nishati hiyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Wanawake kwenye Sekta ya Gesi ya LPG kutoka TZLPGA Winner Joram Lukumay amesema tafiti zinaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanaotumia gesi ya LPG kupikia ni wanawake, jambo linaloonesha nafasi kubwa ya wanawake katika mapinduzi ya matumizi ya nishati safi nchini pamoja na mchango wao katika kulinda afya na mazingira.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa kuhusu sekta ya LPG, matumizi salama ya gesi pamoja na fursa za ajira na biashara zilizopo, huku wakiahidi kuendelea kutoa elimu hiyo kwa jamii ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mafunzo hayo yaliyowashirikisha zaidi ya wanafunzi 120 kutoka kada mbalimbali za uhandisi na sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma, yamelenga kuwaandaa vijana kuwa wataalamu na mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

.jpeg)
.jpeg)
إرسال تعليق