Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Stephen Wasira amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo hakina hoja ya msingi ya kuzuia Uchaguzi Mkuu mwaka huu kwani kama ni mabadiliko wanayoyazungumza yameshafika tayari.
Amesema CHADEMA wao wanasema hawataki uchaguzi mpaka yafanyike mabadiliko ya uchaguzi, lakini ukweli wameshafanya marekebisho, na kusisitiza marekebisho yaliyofanyika yanahusisha sheria tatu ambazo zimefanyiwa mabadiliko.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Machi 27,2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Wasira aliyekuwa akihutubia wananchi hao amesema sheria zilizofanyiwa mabadiliko ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na madiwani.
Amesema nyingine ni sheria nyingine ni ya Tume ya uchaguzi pamoja na sheria ya vyama vya siasa vinavyosimamiwa na msajili wa vyama vya siasa na kuongeza mambo hayo ndiyo waliyokuwa wanalalamikia.
“Moja wanasema wao hawataki uchaguzi wanasema tume ile inateuliwa na Rais moja kwa moja kwahiyo sio huru, tukasema hamna tabu sheria mpya wabunge wako hapa, wakaunda kwamba tuweke kamati maalumu ili mtu anayetaka ukamishna wa tume ya uchaguzi waombe na ipo hiyo inaongozwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar na watu kutoka Tume ya Haki za Binafamu na Utawala Bora.
“Kwahiyo ukifika wakati atakayetaka ukamishna anaomba na huyo anayeomba anatazamwa kwa vigezo vilivyowekwa kulingana na kazi anayoomba ,hiyo kamati ipo na maana yake ni kwamba mamlaka ya Rais yamepunguzwa…zamani alikuwa anaweza kuteua sasa hawezi, mpaka kamati ya usaili halafu imuambie Rais umehitaji watu watano tunakupa wanane chagua watano.”
Wasira amesema hayo ni mabadiliko makubwa na kuongeza wapinzani walisema Wakurugenzi watendaji wa halmashauri wanaiba kura hivyo hawataki wasimamie uchaguzi na walienda mpaka Mahakama ya Afrika Mashariki kupinga wakurugenzi hao ,hivyo sheria mpya imewaondoa.
“Sasa tume itakuwa inateua watumishi wa umma waandamizi na watumishi waandamizi wa umma sio wote wanateuliwa na Rais hata ukienda vyuo vikuu utawakuta watumishi wa umma waandamizi ni watu wasomi lakini hawateuliwi na Rais bali wanateuliwa na bodi za vyuo vyao na wanakuwepo kwa ajili ya usomi wao.
“Wakiteuliwa watu wa namna hiyo na hasa watumishi wengine wa serikali waaminifu kwa ajili ya kusimamia uchaguzi na wakurugenzi waliokuwa wametamkwa kwenye ile sheria ya zamani wakaondolewa.Sasa hayo ndio mabadiliko makubwa ambayo yamefanywa,sasa imekuja hii hoja mpya mmeisikia na nyinyi ila inasemwa kwa kiingereza
“Inasema No Reform No election eti wanataka mabadiliko zaidi ya yale yaliyofanyika sasa tunawauliza wabunge ndio wenye kazi ya kufanya mabadiliko ya kisheria na Bunge linavunjwa Juni 27 na wabunge wanarudi kwetu wanakuwa raia kama sisi sasa uwalazimishe wafanye mabadiliko tena na presha ya ubunge iko juu,”amesema.
Ameongesa kuwa eti wabunge wabaki bungeni kwa ajili ya reform watakimbia hiyo reform kwani hawapo wamemaliza muda wao kwahiyo CHADEMA wanasema mambo ambayo hayawezekani.Unajua unaweza ukaeleza mambo hayatekelezeki hata wenye akili wakasema huyu anasema nini naye huyu
“Sasa hilo wametoka wanasema wanataka reform ipi wakati reform tumefanya kumbe ile ni danganya toto kwasababu wanaogopa uchaguzi wanakuja wakijua mtawapiga chini,walizoea kudanganya sasa udanganyifu mwisho ,wamekuwa kama timu ya mpira inayoweka mpira kwapani.
“Siunajua timu ya mpira ikiweka mpira kwapani ujue wanaogopa,nazungumzia mpira wa siasa sio wa uwanjani.Sasa nawaambia haya ndio mambo ,kwahiyo badala ya kusema tunaogopa uchaguzi wanasema mpaka yafanyike mabadiliko ,tutazuia uchaguzi,”
Wasira amewaambia wananchi wa Kahama wajue CHADEMA hawana uwezo wa kuzuia uchaguzi ,na waeleze watazuia kwa kufanyaje maana Katiba inasema katika ibara ya 41 hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia uchaguzi wa Tanzania
Amefafanua Uchaguzi utahairishwa kama kuna vita ,na nchi haina vita sasa anahairisha kwasababu ipi au vita iko ndani ya vichwa vyao maana inawezekana anatembea halafu ndani ya vichwa kuna vita inapiganwa.
“Uchaguzi unaanza kwa kujiandikisha na wakati wao wanaendelea na kelele za No Reform wenzao wanajiandikisha na Dar es Salaam maelfu ya watu wamejiandikisha mpaka siku zimeongezwa maana wanakwambia achana na no reform achana na maneno yao ,watu wanataka kupiga kura.”
Post a Comment