MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Tanzania Bara amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kupitia kauli mbiu yake ya kazi iendelee ametekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo iliyoachwa na mtangulizi wake Hayati Dk.John Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano.
Wasira amesema kuwa Dk.Magufuli alikuwa na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu lakini Rais Samia alipochukua uongozi wa nchi hakuacha neno kazi na hivyo akaja na Kazi iendelee na hakika katika miaka minne ya uongozi wake amefanya mambo makubwa licha ya kwamba wapo baadhi ya watu hawakuamini kama ataweza.
Akizungumza Machi 17,2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Soko la Mwanjelwa jijini Mbeya, Wasira ambaye yupo katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani , kuzungumza na wana CCM pamoja na kusikiliza kero za wananchi amesema kwa mujibu wa Katiba baada ya kifo cha Rais , basi Makamu wa Rais ndio anaapishwa kuwa Rais.
“Katiba inasema Rais akifa Makamu wa Rais anaapishwa kuwa Rais, kwahiyo tarerehe 19 siku mbili zijazo Rais Samia alitangazwa kuwa Rais kuchukua nafasi ya Dk.John Pombe Magufuli na kama mnavyojua John Magufuli alikuwa na kauli mbiu anasema Hapa Kazi Tu…
“Sasa Rais Samia alipochukua hakutaka kuacha neno Kazi lakini akasema Kazi Iendelee, hiyo ndio historia ya miaka minne na yalipotokea hayo kama kawaida ya binadamu wanasitasita hivi inawezekana , nchi itakuwa salama?Miradi iliyoanzishwa itamalizwa? Lakini leo tulipo hapa unaweza kuuliza kazi imeendelea au haijaendelee?
“Kazi imendelee tena kuliko wengine tulivyodhani , nitawapa mifano michache, moja wakati Dk.Magufuli anaondoka duniani alianzisha ujenzi wa reli ilikuwa imefika Morogoro lakini ilikuwa haijakamilika ,Rais Samia ameendeleza reli ya SGR sasa imefika Makutupola mkoani Singida,leo Dar es Salaam na Morogoro mpaka Dodoma imekuwa karibu kwasababu ya reli hii,”amesema Wasira.
Ameongeza katika ujenzi wa reli hiyo kila kipande kuna mkandarasi na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu na miaka miwili ijayo reli itakuwa imefika Tabora, Kigoma lakini itakuwa inafika Mwanza .Kwahiyo kazi iliyokuwa imeachwa inafanyika.
Amesema kazi nyingine aliyoachiwa ni kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo limefikia asilimia 100 lakini wakati Rais Samia anachukua nchi ujenzi wake ulikuwa asilimia 30, hivyo kazi imendelee na kuongeza kulikuwa na tatizo la mgao lakini sasa hakuna.
“Kuna matatizo ya miundombinu ambapo umeme unaweza kukatika kwa muda lakini hakuna mgao , nchi yetu inaumeme wa kutosha na hay oni baadhi ya mambo ambayo utekelezaji wake umefanyika kwa asilimia 100 chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na ndio maana tunasema Rais Samia mitano tena.
Amesema Rais Samia amefanya mambo makubwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake na kutoa mfano kwa Mkoa wa Mbeya Mjini na Vijijni kwa upande wa elimu ya msingi madarasa mapya 156 yamejengwa lakini kwa upande wa sekondari yamejengwa madarasa 335 tena ya kisasa.
“Katika eneo la afya hapa Mbeya katika kipindi cha miaka minne zahanati 20 na vituo vya afya 14 vimejengwa na lengo kuu ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Jana nilipokuwa Songwe niliambiwa jambo ambalo sikutarajia kuambiwa, nimeambiwa akina mama wakienda kujifungua wanadaiwa hadi Sh.300,000 .
“Sera ya CCM katika suala la tiba inasema kwanza wakina mama wajawazito hawatakiwi kutozwa hata sh.10 kwa ajili ya kujifungua.Sera yetu inasema watoto chini ya miaka mitano watibiwe bila masharti bila kudaiwa chochote,shabaha yetu watu watibiwe bure na ndio maana tunazungumza kuhusu bima kwa wote.
“Pia tunasema wazee wasiojiweza wakiorodheshwa na halmashauri wakienda na kadi walizopewa wanatakiwa kupewa matibabu bure. Jana usiku nimeongea na Waziri wa Afya naye amefikisha jambo hilo katika vituo vya afya na hospitali zote ambapo amepiga marufuku wajawazito wanaokwenda kujifungua kutozwa fedha.”
Kuhusu usambazaji maji katika Mkoa wa Mbeya, Wasira amesema usambazaji maji uko vizuri kwani umefikia asilimia 90 kutoka asilimia 80 na asilimia 10 iliyobakia itaingizwa katika Ilani inayokuja lengo likiwa kuhakikisha upatikanaji wa maji mijini unakuwa kwa asilimia 100 na vijijini asilimia 95.
Post a Comment