Na: Dk. Reubeni Lumbagala
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea na mikakati yake ya ndani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2025. Mathalani, katika safu ya Urais, kazi imeshamalizika. Dk. Samia Suluhu Hassan ndiye mgombea wa nafasi ya Urais kwa Tanzania Bara huku mgombea mwenza wake akiwa Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye pia kwa sasa ndiye Katibu Mkuu wa CCM Taifa.
Kwa upande wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi ndiye mgombea wa Urais, akigombea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili. Kwa nafasi za Ubunge, Uwakilishi Zanzibar na Udiwani, mchakato wake bado, na wakati utakapofika, pazia litafunguliwa ili mwanachama yeyote mwenye nia ya kuwania nafasi hizo awe huru kugombea ikiwa ni moja ya haki ya kikatiba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 11, 2025 na Katibu wa NEC - Organaizesheni wa CCM, Issa Ussi (Gavu), inaeleza kuwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imefanya kikao chake maalum Machi 10, 2025 chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo pamoja na mambo mengine imejadili Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030 ambayo inakwenda sambamba na kauli mbiu itakayotumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 inayosema "Kazi na Utu, Tunasonga Mbele."

"Vilevile, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imepitisha Kauli Mbiu rasmi kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 isemayo; KAZI NA UTU, TUNASONGA MBELE. Kauli Mbiu hiyo inaakisi dhamira ya Chama ya kuendelea juhudi za ujenzi wa Taifa lenye maendeleo jumuishi, mshikamano wa kitaifa na ustawi wa watu wenye kujali UTU," imesema taarifa hiyo.
Katika kufikia malengo ambayo taasisi imejiwekea, uwepo wa kauli mbiu ni muhimu sana. Niipogeze CCM kuja na kauli mbiu ambayo inasisitiza kufanya kazi kwa kuthamini utu wa watu ili kusonga mbele kimaendeleo. Kimsingi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imejipambanua kuwa ni serikali yenye kuwajibika kwa wananchi wake kikamilifu kwa kuwatumikia kupitia utekelezaji wa majukumu na ndiyo maana inasisitiza "Kazi Iendelee."
Kumekuwa na mafanikio mengi katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025. Mafanikio haya yametokana na dhamira ya dhati ya serikali na utashi wa kisiasa wa kuwatumikia wananchi wake kwa kuzingatia ahadi zilizomo kwenye Ilani ya uchaguzi. Kwa mfano, Mitaa, Vitongoji, Vijiji, Kata, Wilaya na Mikoa kote nchini imepokea fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi mingi ya maendeleo katika sekta mbalimbali kama vile maji, afya, masoko, elimu, uvuvi, kilimo, barabara, ufugaji, umeme na sekta nyingine kadha wa kadha.
Aidha, ni katika msingi wa kazi na uwajibikaji wa chama na serikali ndipo yalipozaliwa mafanikio haya makubwa ya kimaendeleo nchini. Kwa kuwa juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo zimelenga kuchochea maendeleo ya watu, ni muhimu suala la utu wa watu ukazingatiwa ipasavyo katika uwajibikaji wa serikali katika kuwatumikia wananchi. Ni maelekezo ya Chama kupitia Kauli Mbiu ya "Kazi na Utu, Tunasonga Mbele," kuwa juhudi na utekelezaji wa majukumu ya kazi yanayofanywa yanapaswa kuzingatia utu kwanza ili kusonga mbele kimaendeleo.
Kwa hiyo, wagombea wote katika mafiga matatu yaani Urais, Ubunge na Udiwani kuzingatia kuwa uwajibikaji wa kazi ni lazima uzingatie utu ili kusonga mbele. Kazi zenye kutweza utu wa watu kamwe haziwezi kuleta matokeo chanya na furaha katika jamii na Taifa kwa ujumla. Wananchi ambao ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka serikali madarakani wanapaswa kuthaminiwa utu wao. Wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mipango mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao wanayoishi ili waweze kutoa maoni yao ambayo ni muhimu sana.
Uwajibikaji wa kazi unaweza kufanyika na tija ikaonekana katika maendeleo bila kutweza utu wa wananchi. Hivyo basi, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, wagombea wazingatie kuwa kiu ya wananchi ni maendeleo. Wananchi wanataka viongozi ambao watasukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa kuzingatia utu. Tunaweza kusonga mbele kwa kufanya kazi kwa kuzingatia utu kama ambayo kauli mbiu ya CCM inavyoelekeza kunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2025.
Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Post a Comment