Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ameipongeza
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA) kwa kukamilisha ujenzi wa
gati ya Lindi na kuwataka kutafuta masoko ili bandari hiyo iweze
kunufaisha Serikali na wananchi wa Mkoa huo.
Prof.
Mbarawa ametoa kauli hiyo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa
gati hiyo mkoani Lindi ambapo amesema mradi umekamilika kwa asilimia 92
na kukamilika kwa gati hiyo kutarahisisha biashara na kukuza uchumi kwa
wananchi kwani meli kubwa zitaanza kutia nanga katika bandari hiyo.
“Napenda
kuwapongeza sana TPA kwa kazi kubwa mliyoifanya kukamilisha mradi huu,
ni wakati sasa mkatafute masoko ili mpate faida na kurahisisha
usafirishaji kati ya mkoa huu na visiwa vinavyozunguka” amesema Prof.
Mbarawa.
Waziri
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa pamoja na kukamilisha mradi huo TPA itunze
miundombinu hiyo na kuifanyia ukarabati wa mara kwa mara ili iweze
kudumu kwa muda mrefu.
Kwa
Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Karim Mattaka,
amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa, kuwa Mamlaka itazingatia maelekezo
yake na kuahidi kusimamia sehemu ndogo iliyobaki ili iweze kukamilika
kwa wakati na viwango vilivyokubaliwa.
Mhandisi
Mattaka ameongeza kuwa ujenzi wa gati hiyo imegharimu kiasi cha
shilingi zaidi ya bilioni 3 na fedha hizo zimefadhiliwa kwa asilimia 100
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika
hatua nyingine Waziri Profesa Mbarawa, amesema Kivuko kwa ajili ya
Lindi na Kitunda kitawasili mapema katikati ya wiki ili kianze kutoa
huduma kwa wakazi wa mkoa huo.
Aidha
ameauagiza uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuhakikisha
wanatafuta fedha na kujenga majengo ya abiria kwa upande wa Lindi na
Kitunda ili kupunguza changamoto inayowakabilia abiria hasa nyakati za
mvua.
Naye
Mkandarasi wa Kampuni ya Hematec, Emmanuel Lyimo amesema mpaka sasa
ujenzi uko kwenye hatua za mwisho na ambapo ndani ya siku chache mradi
huo utakamilika na kukabidhiwa kwa ajili kuanza kutoa huduma.
Waziri
Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku mbili kwenye mikoa ya Mtwara
na Lindi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Bandari na
Vivuko.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA, Eng
Karim Mattaka, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), kuhusu hatua za
ujenzi wa gati ya Lindi, wakati Waziri huyo alipotembelea mradi kukagua
maendeleo yake.
Muonekano
wa Gati mpya ya Bandari ya Lindi ambayo ujenzi wake umekamilika kwa
asilimia zaidi ya 90. Gati hiyo imegharimu kiasi zaidi ya shilingi
bilioni 3 ikiwa ni fedha za Serikali kwa asilimia 100.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akipanda
kwenye boti kuelelekea katika eneo la Kitunda mkoani Lindi, wakati
akikagua maendeleo ya ujenzi wa maegesho ya kivuko Mkoani humo. Waziri
Prof. Mbarawa amewahakikishia wakazi wa Mkoani humo kuwa kivuko hicho
kitawasili na kuanza kutoa huduma mwishoni mwa wiki hii.
Muonekano
wa hatua ilipofikia Gati ya kuegeshea kivuko katika eneo la Kitunda
Mkoani Lindi. Ujenzi wa Gati hiyo umefikia asilimia zaidi ya 90 na
imejengwa kwa fedha za Serikali.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto)
akishiriki katika kuchanganya zege katika ujenzi wa barabara ya maegesho
ya kivuko Mkoani Lindi, alipokagua maendeleo ya ujenzi wake.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na
wakazi wa Mkoani Lindi, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi
maegesho ya Kivuko. Waziri Prof. Mbarawa amewahakikishia wakazi hao kuwa
kivuko kitawasili katikatia ya wiki na kuanza kazi mwishoni mwa wiki.
No comments:
Post a Comment