Mheshimiwa
Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki akiwa kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao wawili
walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini wakati
wa ziara ya kikazi ya siku tatu ya Waziri Mahiga nchini humo.
:Dkt.
Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Chang Yaong Hun,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea Kusini. Viongozi hao
wawili walikutana kwenye ofisi za Benki hiyo Jijini Seoul Korea Kusini.
Dkt.
Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki akiwa kwenye picha ya pamoja na Bw. Jundong Kim, Makamu
Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI). Mwingine
pichani ni Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Matilda
Masuka.
Dkt.
Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki akiwa na ujumbe wake kwenye mazungumzo na Bw. Jundong Kim,
Makamu Mwenyekiti wa Korea Chamber of Commerce and Industries (KCCI).
Mheshimiwa
Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki akimkabidhi zawadi ya majani ya chain a kahawa za Tanzania Bw. Choi
Jong-won, Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Dong Myeong ya Korea Kusini.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt.
Augustine Mahiga ameahidi kusimamia uimarishwaji wa uhusiano wa kiuchumi
na biashara kati ya Tanzania na Korea Kusini ili wananchi wa pande zote
mbili wapate manufaa.
Waziri
Mahiga ameyasema hayo alipokuwa anahitimisha ziara yake ya kikazi ya
siku tatu ambapo siku ya mwisho aliitumia kikamilifu kukutana na taasisi
za umma za biashara na viwanda, Benki ya Exim ya Korea pamoja na
makampuni binafsi yanayojipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo nchini Tanzania.
Amesema
kuwa miaka 25 ya kwanza ya uhusiano wetu na Jamhuri ya Korea ilijikita
kwenye kuweka misingi imara ya uhusiano wa kidiplomasia ambapo nchi zetu
zilikuwa zinajiimarisha kama mataifa huru. “Sasa ni wakati wa kushamiri
kiuchumi tuone sekta binafsi zinavyoshiriki katika kukuza uchumi,
wananchi wa Tanzania waje kwa wingi nchini Korea kujifunza masuala ya
teknolojia, uhandisi na hata usanifu na ubunifu. Huu ndio uhusiano wenye
tija kwa mataifa yetu”. Mheshimiwa Waziri alisema.
Akizungumza
na Bw. Chang Yaong Hun, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya Korea,
Mheshimiwa Mahiga mbali na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kutoa
mikopo na misaada nchini Tanzania, Waziri Mahiga alieleza kuwa Serikali
ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli sasa imejikita kwenye
mapambano dhidi ya rushwa na ujenzi wa viwanda ili kuleta maendeleo ya
kweli kwa wananchi wetu. Kwasasa Benki hiyo inatekeleza miradi ya ujenzi
wa miundombinu ya umeme na maji mikoa mbalimbali ya Tanzania ukiwemo
Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa
Mahiga alifafanua kuwa ajenda ya Mheshimiwa Magufuli ya viwanda,
haiwezi kukamilika bila kuwa na miundombinu ya msingi kama vile
uzalishaji wa umeme wa kutosha na ukuaji wa sekta ya uchukuzi na
mawasiliano ambapo Korea Kusini ni wabobezi kwenye masuala hayo.
Alitumia
fursa hiyo kumkaribisha Bw. Chang na timu yake kwenda Tanzania kufanya
tathmini ya miradi tunayoshirikiana nao, lakini pia miradi mipya kwenye
sekta ya uchukuzi kama ujenzi wa Standard Railway Gauge “SRG” kutoka
Isaka hadi Kigali, n.k. ambayo ni miradi ya kipaumbele kwa sasa kwa
taifa letu.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Chang alisifu utendaji kazi wa Rais John Pombe
Magufuli, na Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania na kusema kuwa
utendaji kazi wa aina hii ni wa kupigiwa mfano barani Afrika, na umekuja
wakati muafaka tunapoingia kwenye hatua nyingine ya uhusiano wa
kiuchumi baina ya nchi zetu mbili. Aidha aliongeza kuwa, wakati umefika
sasa wa kufanya kazi, nay eye yuko tayari kufanya kazi na Tanzania kwani
Serikali yake, imetoa kipaumbele kwa nchi hii.
Korea
Exim Bank ni taasisi ya Serikali inayosimamia mikopo na misaada ya
Jamhuri ya Korea inayotoa kwa nchi nyingine. Katika kipindi cha miaka
minne (tangu 2016 hadi 2020), Korea Kusini kupitia taasisi hiyo,
imeongeza mikopo ya maendeleo kwa bara la Afrika kwa asilimia 20. Uamuzi
wa Serikali iliyokuwa madarakani mwaka 2016 wa kuichagua Tanzania
kupokea kiasi kikubwa cha msaada huo kuliko nchi nyingine ya Afrika,
umeendelezwa na Serikali iliyopo sasa madarakani ya Mheshimiwa Moon
Jae-in, Rais wa Jamhuri ya Korea.
Ujumbe
wa Mheshimiwa Augustine Mahiga pia ulikutana na kufanya mazungumzo na
Bw. Judong Kim, Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara na Viwanda ya
Korea (Korea Chamber of Commerce and Industries KCCI), ambapo Waziri
Mahiga aliwasisitiza kuja Dar es salaam kuangalia fursa zilizopo ili
kuwashawishi wanachama wao kutafuta bidhaa na masoko nchini Tanzania.
Akielezea
umuhimu wa KCCI kuzuru Tanzania na kujifunza soko la biashara, Bw.
Edwin Rutageruka Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE aliyeongozana na ujumbe wa
Mheshimiwa Waziri Mahiga, alisema njia nzuri ya kupata picha halisi ni
kupitia Maonesho ya Biashara ya Saba Saba. Hivyo alitumia fursa hiyo
kualika ujumbe wa KCCI kushiriki kwenye maonesho ya 42 yanayotarajiwa
kuanza tarehe 28 Juni – 10 Julai, 2018.
Kabla
ya kuhitimisha ziara yake, Mheshimiwa Mahiga pia alikutana na kufanya
mazungumzo na watendaji wakuu wa makampuni ya DOHWA, ambao wamejikita
kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya reli n.k. Makampuni mengine
ni KORAIL, STX Engine, KTMI & STX Offshore pamoja na GS E&C,
ambao wote wameonesha nia ya kuwekeza au kufanya biashara nchini
Tanzania. Ujumbe mkuu kwa taasisi na makampuni hayo ulikua ni kupanua
fursa za ushirikiano wa biaashara na uwekezaji, ubadilishanaji wa ujuzi
na ujengaji uwezo wa wafanyakazi ambao ndio nguvu kazi ya taifa letu.
Pamoja
na kuzungumza na makampuni ya umma na sekta binafsi yaliyoorodheshwa
hapo juu, ziara ya Mheshimiwa Augustine Mahiga, ilimuwezesha kuwa mgeni
rasmi kwenye Kongamano la Kwanza la Biashara kati ya Tanzania na Korea
Kusini ambapo alihutubia mamia ya wafanyabiashara wa Korea kuhusu
utayari wa Tanzania kushirikiana na nchi hiyo kibiashara.
Mkutano
huo uliopewa kauli mbiu ya “Eplore Tanzania” ulifuatiwa na mikutano
midogo midogo iliyowakutanisha baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania na
Korea Kusini ili kuangalia kwa ukaribu maeneo ya ushirikiano. Balozi wa
Tanzania nchini Korea Kusini na mwenzake wa Korea Kusini nchini Tanzania
wameazimia kuendeleza makongamano hayo ya kila mwaka ili kuwa na
ushirikiano wa karikiano wa karibu wa kibiashara kwa mataifa hayo mawili
kwa maendeleo ya wananchi wote.
Wajumbe
wengine walioongozana na Mheshimiwa Waziri Mahiga nao walipata fursa ya
kuhutubia hadhara hiyo kuhusu Tanzania ambapo Bw. Geoffrey Mwambe,
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Investment Centre alitoa utangulizi
kuhusu uwekezaji Tanzania; Kanali (mstaafu) Joseph Simbakalia,
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA alizungumzia maeneo ya kipaumbele kwenye maeneo
maalum ya uwekezaji nchini Tanzania. Naye Bi. Nasriya Nassor, Mkurugenzi
wa Biashara wa Taasisi ya Uwekezaji Zanzibar alitoa taarifa fupi kuhusu
Zanzibar kama kivutio cha utalii ndani ya Tanzania na eneo
linalopendelewa na watalii wengi duniani.
Jamhuri
ya Korea, kama inavyojulikana rasmi na Umoja wa Mataifa, ni mojawapo ya
nchi zinazofanya vizuri zaidi duniani kiuchumi kwa sasa. Viashiria vya
uchumi vinaonyesha uchumi wa nchi hiyo utaendelea kukua kwa viwango
kutokana na jitihada za dhati za viongozi wa nchi hiyo za kufuta kabisa
umaskini kwa wananchi wao. Kwa sasa wastani wa pato kwa mtu “per capital
income” inakadiriwa kuwa zaidi ya US$ 34,000, ukilinganisha na US$
22,670 mwaka 2012. Baada ya vita ya Korea kwenye miaka ya mwanzo ya
1950, nchi ya Korea Kusini ilikua maskini kuliko nchi nyingi barani
Afrika ikiwemo Tanzania ambapo wastani wa pato kwa mtu ilikua na US$67.
Mheshimiwa
Mahiga anatarajiwa kurejea nyumbani baada yakuhitimisha ziara hiyo
aliyosema italeta faida sio tu kwa wafanyabiashara, ila kwa jamii kwa
ujumla. “Nchi hii ni tajiri sana kiuchumi; lakini utajiri wake mkubwa
pia uko kwenye taaluma ya rasilimali watu, hivyo kwa Tanzania kufanikiwa
kufungua ubalozi hapa, sasa tumefungua milango ya ushirikiano wa
karibu, kuliko ilivyokuwa mwanzo. Tuchangamke tuige mfano wa uchapa kazi
wao, na sisi tutaondoka kwenye umasikini” Waziri Mahiga alisema kwa
umaliza, kabla ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Incheon,
uliopo mjini Seoul, Jamhuri ya Korea.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Seoul, Korea Kusini,
No comments:
Post a Comment