Pages

February 16, 2018

TPB BANK YAUNGANA NA SAVINGS AT THE FRONTIER KUTOA HUDUMA KWA WANANCHI WALIO PEMBEZONI

 Afisa Mtendaji Mkuu wa TPB Bank, Bw. Sabasaba Moshingi, (kulia), akipeana mikono na Meneja Mradi kutoka programu ya SatF, Bw. Steve Peachey, wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari makao makuu ya TPB jijini Dar es Salaam Februari 16, 2018.BENKI ya TPB imeungana na taasisi ya Savings at the Frontier (SatF), kwenye mradi utakaogharimu kiasi cha dola Milioni Moja. Mradi huo unaoitwa “Digitalizing Informal Savings Mechanisms”
NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

BENKI ya TPB imeungana na taasisi ya Savings at the Frontier (SatF), kwenye mradi utakaogharimu kiasi cha dola Milioni Moja. Mradi huo unaoitwa “Digitalizing Informal Savings Mechanisms” utaendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ambapo TPB inatarajia kuwaunganisha kwenye mfumo rasmi wa kifedha wateja wapya laki Mbili na nusu hadi kufikia mwaka 2020, Afisa Mtendaji Mkuu wa TPB Bank, Bw. Sabasaba Moshingi amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 16, 2018.

Kitangaza mradi huo mbele ya waandisahi wa habari, Bw. Moshingi alisema, mradi huo utaanzia Mkoa wa Ruvuma, na baadae kupelekwa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Njombe, Iringa na Morogoro.

“Watanzania wengi waishio kwenye mikoa ya pembezoni, hususani wenye vipato vidogo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa huduma za kifedha. Kupitia ushirikiano huu na SatF, TPB itawawezesha wananchi kupitia makundi au mtu mmoja mmoja, kujiwekea akiba kupitia teknolojia rahisi na salama isiyowalazimu kwenda kwenye tawi la benki ili kupata huduma hizo za kifedha. Njia hii itawawezesha wananchi kutatua changamoto zao mbalimbali za kifedha na pia kuwaingiza kwenye mfumo rasmi wa kiuchumi.

Akifafanua zaidi Bw. Moshingi alisema, Benki ya TPB ni benki ya kwanza hapa nchini kuanzisha utoaji wa huduma za kibenki kwa makundi kupitia simu za mkononi, maarufu TPB POPOTE. Hivi sasa, wateja kupitia vikundi vyao wanaweza kuweka akiba na hata kukopa kupitia simu zao za mkononi.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi kutoka programu ya SatF, Bw. Steve Peachey, amesema benki ya TPB ndio benki ya kwanza kufanya kazi na taasisi yake hapa nchini, na walivutiwa na namna ambavyo TPB imeonyesha dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi hao kupata huduma za kifedha.

Pia, amesema taasisi yake inayo furaha kubwa kupata nafasi ya kufanya kazi na benki ya TPB , taasisi ya fedha yenye sifa na historia ndefu  katika jitihada za kupeleka huduma za kifedha kwa wananchi wake popote walipo. Hii ni fursa nzuri kwa SatF na TPB kujenga umoja imara utakaowawezesha kuwafikia wananchi maskini.

“SatF ni programu maalum yenye malengo ya kuhakikisha huduma za kifedha za uhakika zinawafikia wananchi wengi walio nje ya mifumo rasmi ya kibenki, programu hii inaratibiwa na shirika la Oxford Policy Management kwa ufadhili wa taasisi ya kimataifa ya MasterCard Foundation, dhumuni kuu ikiwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na jamii zenye vipato vya chini kwenye nchi zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara.” Alifafanua Bw. Peachey

Aidha Bw.Peachey aliendelea kwa kusema kuwa lengo kuu la SatF ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma endelevu za kifedha, na kwa sababu hiyo, wapo tayari kushirikiana na benki ya TPB kwa kutoa msaada wa kifedha na kiufundi.

“Tunaamini kuwa jitihada tunazofanya zitakuza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi ambao hapo awali walitengwa na huduma hizi, na hivyo kukuza uwezo wao kiuchumi”, alisema.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Finscope mwaka 2017, asilimia 59 ya Watanzania wanavipato vya msimu, na miongoni mwa changamoto zinazowakabili kubwa ni pamoja na uwezo wa kumudu gharama za matibabu, na malipo ya ada za shule kwa ajili ya watoto wao. Utafiti huo pia ulionyesha kuwa asilimia 40 ya Watanzania hukopa fedha kutoka kwa jamaa ama rafiki kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za kifedha zinapojitokeza. Kiasi cha Watanzania Milioni 7.8 wametengwa na huduma za kifedha, na hili limeleta uhitaji mkubwa wa mazingira bora ya kuwawezesha wananchi hao kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba ili waweze kukabiliana na changamoto za kimaisha.

 Meneja wa mradi kutoka programu ya SatF, Bw. Steve Peachey(kushoto), akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Bw. Sabasaba Moshingi.
Meneja Mkuu anayeshuhughulikia masuala ya Kampuni ya TPB Bank, Bi. Noves Moses akizungumza mwanzoni mwa hafla hiyo.
 Bw. Moshingi, na Bw.Peachey, wakiwa na maafisa wa TPB Bank, na SatF.
 Maafisa wa TPB wakisikiliza

 Bw. Moshingi akifafanua jambo huku Bw. Peachey, (wakwanza kushoto), na Bw.Ignas Jacob kutpoka SatF, wakisikiliza.
Maafisa wa TPB, wakiwa kwenye mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...