Taasisi
ya Mo Dewji imetangaza orodha ya wanafunzi 22 wa elimu ya juu waliopata
ufadhili kutoka katika taasisi hiyo kwa mwaka wa masomo 2017/2018
kupitia mpango wa Mo Scholars. Wanafunzi
hao ni Neema Charles, Winfrida Mrope, Henritha Rwegasira, Monica
Ubushimbali, Suzana Mkindi, Hamisa Selemani, Beatrice Shupa, Phoebe
Mwankemwa, Amon Abraham, Venance Makambe na Amos Ntandu.
Wengine
ni Benjamin Mkondya, Ally Mashaka, Amuniri Sebarua, Iddi Mbilinyi,
Samwel Ponda, Eram Temu, Busumilo Tumaini, Cosmadeus Mayunga, Amos
Kashinje, Kelvin Ernest na Barnaba Barnaba ambao wote ni wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Akizungumza
kuhusu ufadhili huo, Mwanzilishi wa Taasisi ya Mo Dewji, Mohammed Dewji
aliwapongeza washindi kwa kufanikiwa kupata ufadhili huo, lakini
akiwataka kujituma ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika
maisha yao.
Mohammed
Dewji akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao
wanafadhiliwa na Taasisi ya Mo Dewji (hawapo kwenye picha) katika hafla
ya kutangaza washindi wa mpango wa ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya
juu (Mo Scholars). Picha zote na Rabi Hume.
“Mmepata
ufadhili huu muutumie vizuri, wapo wengi ambao walituma maombi lakini
nyie mmefanikiwa kupata ufadhili. Msome kwa bidii na baadae mpate kazi
nzuri ambazo zitawasaidia kupata kipato na kusaidia ukuaji wa uchumi wa
nchi,” alisema Dewji. Dewji alisema
aliamua kuanza kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuunga
mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Pombe Magufuli ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.
Mohammed
Dewji akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao
wanafadhiliwa na Taasisi ya Mo Dewji katika hafla ya kutangaza washindi
wa mpango wa ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Mo Scholars).
Aliongeza
kuwa, dhamira yake ni kuona Watanzania wengi wananufaika na mpango huo
na amejipanga kuhakikisha kuwa idadi ya wanufaika wa mpango wa ufadhili
unaotolewa na taasisi yake unaongezeka kila mwaka.
“Kasi
yetu bado ni ndogo sana kulinganisha na ninavyotaka. Wakati tunaanza
kutoa ufadhili tuliamua kuanza na wanafunzi 10 lakini mimi nataka tuwape
ufadhili Watanzania wengi ikiwezekana tufike hata 100. Kwangu ni jambo
jema sana kusaidia Watanzania wenzangu kwa sababu nimezaliwa hapa na
nitazikwa hapa sina pengine pa kwenda,” alisema Dewji.
Mmoja
wa wanafunzi ambaye kabla ya kupata ufadhili aliweka tangazo kwenye
mtandao wa kijamii kwamba anauza figo yake, Amos Ntandu akielezea
histori ya maisha yake hadi alilopata ufadhili wa Taasisi ya Mo Dewji.
Nae
mmoja wa wanafunzi ambaye kabla ya kupata ufadhili aliweka tangazo
kwenye mtandao wa kijamii kwamba anauza figo yake, Amos Ntandu
aliishukuru Taasisi ya Mo Dewji kwa ufadhili ambao imewapatia kwani
baadhi yao waliokuwa wamepoteza matumaini ya kuendelea na masomo, lakini
pia kuomba uongozi wa taasisi kuendelea kutoa ufadhili kwa Watanzania
ili wapate elimu.
“Mimi
nilikuwa tayari kuweka maisha yangu hatarini kwa kutangaza kuuza figo
langu, lakini ufadhili huu mliotupatia umebadili maisha yetu. Idadi ya
wanafunzi wanaokosa mkopo ni kubwa hivyo nawaomba muwe na moyo wa
kuendelea kuwasaidia ili na wao wafikie ndoto zao,” alisema Ntandu.
Mkuu wa Taasisi ya Mo Dewji, Barbara Gonzalez akizungumza kuhusu mpango wa ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Mo Scholars).
Pamoja
na kutangaza washindi hao, pia taasisi hiyo ilitoa zawadi ya kompyuta
mpakato (laptop) kwa wanafunzi wa mwaka wa masomo 2016/2017 ambao
inawafadhili waliofanya vizuri katika masomo yao kwa mwaka wa kwanza
chuoni. Kwa sasa idadi ya wanafunzi
ambao wanapata ufadhili kutoka Taasisi ya Mo Dewji imefikia 30, ambapo
kati yao wanafunzi 7 ni wa mwaka wa masomo 2016/2017 na wanafunzi 22
mwaka wa masomo 2017/2018.
Baadhi ya wanufaika wa mpango wa ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu (Mo Scholars).
Mwanzilishi
wa Taasisi ya Mo Dewji, Mohammed Dewji akikabidhi zawadi kwa baadhi ya
wanafunzi wa elimu ya juu waliopata ufadhili kutoka katika taasisi hiyo
kwa mwaka wa masomo 2017/2018 kupitia mpango wa Mo Scholars.
Mwanzilishi
wa Taasisi ya Mo Dewji, Mohammed Dewji akikabidhi zawadi ya laptop kwa
baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu waliopata ufadhili kutoka katika
taasisi hiyo kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kupitia mpango wa Mo
Scholars.
No comments:
Post a Comment