Pages

February 15, 2018

MADINI YA RUBY KUENDELEA KUWANUFAISHA WANANCHI LONGIDO

Na Veronica Simba – Loliondo
Serikali imewaahidi wakazi wa Kata ya Mundarara katika Wilaya ya Longido kuwa itahakikisha madini ya Ruby ambayo yanapatikana katika eneo hilo yanaendelea kuwanufaisha na siyo kuwadidimiza.
Ahadi hiyo ilitolewa jana, Februari 13 na Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Dotto Biteko baada ya kufanya ziara katika Mgodi unaojishughulisha na uchimbaji wa madini hayo na kisha kuzungumza na wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Nyongo na Biteko waliwataka wananchi wa Mundarara kuondoa hofu kuwa neema ya madini hayo yanayopatikana katika maeneo yao haitawanufaisha tena kutokana na kile wanachodai kuwa sheria mbalimbali zilizowekwa na Serikali zinasababisha kupungua kwa Soko lake.
Akizungumza na wananchi hao, Naibu Waziri Biteko aliwaambia kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaandaa mwongozo maalum utakaobainisha utaratibu unaopaswa kutumika katika biashara ya kila aina ya madini hapa nchini ili yaweze kuwanufaisha wananchi na Taifa ipasavyo.
“Nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha rasilimali zote zinazopatikana nchini yakiwemo madini, zinalinufaisha Taifa kwa kiwango kinachostahili. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiibiwa sana na watu wengine kunufaishwa na rasilimali zetu wenyewe ilhali sisi tunazidi kuwa maskini. Sasa tumeamua kuwa hatutaki kuibiwa tena,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi, Biteko alisema kwamba, mwongozo huo unaoandaliwa na Serikali utasaidia hata wananchi wanaozungukwa na Migodi ya Madini kunufaika zaidi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wananchi hao wa Mundarara kuwa na subira wakati Serikali ikishughulikia hoja zao walizoziwasilisha.
Hata hivyo, alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuziba mianya yote ya wizi wa rasilimali madini hivyo alitoa wito kwa wote waliozoea kufanya biashara hiyo kwa udanganyifu kuacha mara moja vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
“Mnapaswa kufanya biashara iliyo safi. Msiiibie Serikali maana tunahitaji kodi na tozo stahiki kutoka biashara hiyo ili zituwezeshe kuwaletea wananchi maendeleo ikiwemo kujenga barabara, hospitali, shule, huduma za maji safi na nyinginezo.”
Awali, akiwasilisha taarifa kwa Naibu Mawaziri kwa niaba ya wananchi wa Mundarara, Diwani wa Kata hiyo, Alais Mushao alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kadhaa, kubwa ikiwa ni kushuka kwa soko la madini ya Ruby, hali inayosababisha kushuka kwa kipato chao hivyo kurudisha nyuma maendeleo.
“Kutokana na idadi ya wanunuzi wa Ruby kuzidi kupungua siku hadi siku, inasababisha wao kujipangia bei wanayoitaka na hivyo sisi kutonufaika,” alisema Mushao.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali ya uasili wa madini ya Ruby kuwa madogomadogo husababisha kupasuka na kupukuchika. Kufuatia hali hiyo, madini hayo yanapokatwa ili kuyaongezea thamani, yanazidi kupoteza uasili na ubora wake hivyo kushusha zaidi thamani yake.
“Kwa hivyo, tunaiomba Serikali iondoe madini haya katika orodha ya madini yanayotakiwa kukatwa ili turuhusiwe kuyauza kama yalivyo, Soko lake lipande nasi tuendelee kunufaika,” alisema Diwani Mushao.
Wakihitimisha Mkutano huo, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko, walipongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Mwekezaji wa Mgodi na wananchi hao ambao walisema ni wa mfano wa kuigwa.
Ilielezwa kuwa pamoja na kusaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kata husika, Mwekezaji huyo amewaruhusu wananchi kuchukua na kuchekecha udongo kutoka Mgodini pasipo kuwalipisha chochote.
Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumza na wananchi wa Kata ya Mundarara Wilaya ya Longido, baada ya kufanya ziara katika Mgodi unaochimba madini ya Ruby eneo hilo Februari 13 mwaka huu. Biteko aliambatana na Naibu Waziri Stanslaus Nyongo (hayupo pichani)
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi wa Kata ya Mundarara Wilaya ya Longido, baada ya kufanya ziara katika Mgodi unaochimba madini ya Ruby katika eneo hilo, Februari 13 mwaka huu. Nyongo aliambatana na Naibu Waziri Dotto Biteko (hayupo pichani)
Sehemu ya umati wa wananchi wa Kata ya Mundarara wilayani Longido, wakiwa katika Mkutano wa Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Dotto Biteko (hawapo pichani), walipofanya ziara katika Mgodi unaochimba madini ya Ruby katika eneo hilo, Februari 13 mwaka huu na kuzungumza nao.
Naibu Mawaziri wa Madini Dotto Biteko na Stanslaus Nyongo wakizungumza na wawekezaji wa Mgodi wa Madini ya Ruby katika Kijiji cha Mundarara wilayani Longido, Februari 13 mwaka huu.
Mawe yaliyo na madini ya Ruby yakiwa yamehifadhiwa katika chumba maalum kilichopo katika Mgodi unaochimba madini hayo kijijini Mundarara, Wilaya ya Longido kabla ya kuchakatwa na kupelekwa Sokoni.
Sehemu ya eneo kunakochimbwa madini ya Ruby katika Kijiji cha Mundarara, Wilaya ya Longido.
Naibu Mawaziri wa Madini Dotto Biteko (kushoto) na Stanslaus Nyongo (katikati), wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (kulia), walipomtembelea ofisini kwake Februari 13 mwaka huu wakiwa katika ziara iliyohusisha kukagua shughuli mbalimbali za madini na kuzungumza na wadau wa sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...