Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi mkoa wa Mwanza Dk. Pius Masele.
Shirika
la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI)
limeendesha mafunzo kuhusu msaada na huduma za kisaikolojia kwa wahudumu
wa jamii wanaosaidia kazi katika vituo vya tiba na matunzo kwa watu
wanaoishi na Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) vilivyopo katika
halmashauri za wilaya mkoani Mwanza.
Mafunzo
hayo ya siku tano yanayokutanisha wahudumu wa jamii kutoka halmashauri
za wilaya za Ilemela,Kwimba, Magu,Buchosa,Misungwi,Sengerema na
Nyamagana yanafanyika kuanzia Jumatatu Februari 12,2018 hadi Ijumaa 16
Februari ,2018 katika ukumbi wa Midland Hotel jijini Mwanza.
Akizungumza
wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi mkoa wa
Mwanza Dk. Pius Masele alisema mafunzo hayo yatawasaidia watoa huduma
ngazi ya jamii kuboresha huduma katika vituo vya afya kwenye maeneo yao.
“Kupitia
mafunzo haya mtaweza kuwaunganisha wateja na huduma mbalimbali za
kijamii ili kuhakikisha kunakuwepo uendelevu wa huduma kwenye vituo vya
tiba na matunzo ikiwa ni pamoja na kuwarudisha kwenye huduma wateja
waliopotea”,alisema Dk. Masele.
“Naomba
mkafuatilie wateja waliopotea, muwaelimishe kuzingatia ufuasi mzuri wa
dawa na kuhakikisha hawapati maambukizi mapya na magonjwa nyemelezi
kwani hatutaki kuona mgonjwa anakuwa wa kulala kitandani, sisi tunataka
watu washiriki katika shughuli za maendeleo”,aliongeza Dk. Masele.
Aidha
alilishukuru shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia
Centres for Disease Control (CDC) kwa kuendelea kushirikiana na serikali
ya Tanzania katika kuwahudumia watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.
“Juhudi
za mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi zitafanikiwa zaidi pia kama
tutaboresha kamati za Ukimwi za ngazi ya kijiji na kata kwa ajili ya
kubadilishana mawazo na uzoefu ili kupunguza maambukizi ya VVU katika
mkoa wetu ambao maambukizi yameongezeka kutoka asilimia 4.2 hadi
7.2”,alisema Dk. Masele.
Naye
Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia
Yona alisema lengo la mafunzo hayo ya msaada wa kisaikolojia ni
kuwezesha upatikanaji wa huduma rafiki kwa watoto, vijana na watu wazima
wanaoishi na VVU ili watambue umuhimu wao katika taifa na jamii zao.
“Mafunzo
haya pia yatasaidia katika kutoa ushauri na mafunzo sahihi kwa watoto
na vijana kuhusiana na majibu ya changamoto zinazowakabili, matumizi ya
dawa/ARV na ufuasi mzuri wa dawa lakini pia kuboresha mawasiliano kati
ya watoa huduma,wazazi, walezi, vijana na watoto”,aliongeza.
Aliyataja
baadhi ya madhara yanayompata mtu iwapo atakosa msaada wa kisaikolojia
kuwa ni pamoja na kukata tamaa ya maisha, kuacha dawa, kuchanganyikiwa,
kujitenga ama kuwa na hali ya upweke na kupoteza maisha.
Shirika
la AGPAHI linatekeleza miradi ya VVU na Ukimwi katika mikoa sita nchini
ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita,Mwanza, Tanga na Mara likishirikiana
na serikali ya Tanzania kupitia ufadhili wa serikali ya Watu wa
Marekani kupitia CDC katika kutekeleza mradi wa “Boresha” ambao unatoa
huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi.
Mratibu
wa Kudhibiti Ukimwi mkoa wa Mwanza Dk. Pius Masele akifungua mafunzo
kuhusu msaada wa huduma za kisaikolojia kwa wahudumu wa jamii. Kulia ni
Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia
Yona.
Dk.
Masele akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo watumie mafunzo
wanayopewa ili wakaboreshe huduma kwenye vituo vya tiba na matunzo.
Dk. Masele akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia mbinu mbalimbali kurudisha wateja waliopotea.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada ukumbini.
Afisa
Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona
akielezea malengo ya mafunzo ya huduma na msaada wa kisaikolojia na
maana yake kwa wahudumu wa jamii.
Cecilia
Yona akielezea shughuli zinazofanywa na shirika la AGPAHI katika kuzuia
maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mwezeshaji
katika mafunzo hayo, Gaston Kakungu ambaye ni Afisa Muuguzi Mstaafu
akitoa mada wakati wa huduma na msaada wa kisaikolojia.
Kakungu akiwaasa washiriki wa mafunzo hayo kuwa daraja muhimu la kuunganisha wateja katika huduma za tiba na matunzo.
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Dk. Joseph Musagasa akielezea juu ya ukweli kuhusu VVU na Ukimwi.
Dk.
Musagasa akiwasihi washiriki wa mafunzo hayo kuwa mstari wa mbele katika
kupiga vita imani potofu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi
ya VVU, ikiwemo kuendekeza waganga wa kienyeji ambao baadhi yao hawana
elimu ya kutosha kuhusu VVU na Ukimwi.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
No comments:
Post a Comment