Na Emmanuel Ghula
WADAU
wa Takwimu nchini wamekutana ili kujadili upatikanaji wa Takwimu za
msingi na uzalishaji wa takwimu na mapungufu yaliyopo katika kupima na
kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Kitaifa, Kikanda na
Kimataifa.
Akizungumza
wakati akifungua warsha ya siku mbili ya wadau hao, Naibu Katibu
Mtendaji Tume ya Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Mhandisi Happiness
Mgalula amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
Maendeleo pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wameandaa warsha
hiyo ili kujadili namna bora ya upatikanaji wa takwimu zitakazosaidia
kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
“Leo
tumekutana hapa kwa pamoja ili kujadili namna bora ya upatikanaji wa
takwimu kwa ajili ya kupima na kutathmini utekelezaji wa viashiria vya
Malengo ya Maendeleo Endelevu na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa
katika sekta ya Ukuaji Uchumi, Ajira na Ushindani wa Kiuchumi,” amesema
Mhandisi Mgalula.
Amesema
Serikali itaendelea kuratibu upatikanaji wa takwimu rasmi nchini
kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na wadau wengine ili
kufanikisha utekelezaji wa seti za malengo ya ulimwengu katika muda
maalumu na ambayo mkazo wake ni kuondoa aina zote za umaskini pamoja na
njaa.
Amesema
Serikali imepiga hatua kubwa katika kuweka mikakati ya utekelezaji wa
Malengo ya Mandeleo Endelevu (SDGs) tangu mwaka 2015 ikiwa ni pamoja na
kufanya mikutano mikubwa miwili ya Kitaifa kwa ajili ya kuwajengea
wananchi uelewa mzuri kuhusu SDGs na utekelezaji wake.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa
ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya amesema NBS itaendelea kushirikiana na
wadau mbalimbali kuhak takwimu rasmi zinapatikana kwa wakati ili ziweze
kutumika na Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika
kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Aidha,
Ruyobya amesema washiriki watajadili namna bora zaidi ambayo wadau
wanaweza kushiriki katika kuchangia mapungufu ya upatikanaji na
uzalishaji wa takwimu pamoja na ubunifu na ujuzi wa teknologia katika
uzalishaji na upatikanaji wa takwimu.
Naibu
Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Mhandisi
Happiness Mgalula akizungumza wakati akifungua warsha ya siku mbili ya
wadau wa takwimu waliokutana kuanzia leo jijini Dr es Salaam katika
ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.
Mkurugenzi
wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius
Ruyobya akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari wakati wa hafla
ya ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya wadau wa takwimu waliokutana leo
jijini Dr es Salaam katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.
Baadhi
ya wadau wa takwimu waliokutana leo jijini Dar es Salaam katika warsha
ya siku mbili ili kujadili namna bora ya upatikanaji wa takwimu kwa
ajili ya kupima na kutathmini utekelezaji wa viashiria vya Malengo ya
Maendeleo Endelevu na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa.
No comments:
Post a Comment