KAMATI
ya Bunge ya Katiba na Sheria imepongeza namna mifuko ya hifadhi ya
jamii ya NSSF na PPF inavyotekeleza mradi wa pamoja wa ujenzi wa kiwanda
cha sukari unaofahamika kama Mkulazi huku ikitoa wito kwa wadau hao
kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati ili kulinusuru taifa na
uhaba wa bidhaa hiyo.
Mwisho
mwa wiki kamati hiyo ilitembelea mradi huo unaotekelezwa katika gereza
la Mbigiri, lililopo Dakawa mkoani Morogoro kupitia kampuni Hodhi ya
Mkulazi Holding inayoshirikiana na Jeshi la Magereza nchini.
"Baada
ya kusikiliza mpango mikakati na kisha kutembelea shamba husika
kiukweli kamati yetu imeridhishwa sana na jinsi wadau hawa
wanavyotekeleza mradi huu. Ni wazi kuwa walifanya utafiti wa kutosha
kabla na matunda yake kiukweli yameanza kuonekana kikubwa tu
tunachowaomba wamalize mradi huu kwa wakati .'' alisisitiza Mwenyekiti
wa kamati hiyo Bw Mohamedi Mchengelwa.
Aidha,
wajumbe wa kamati hiyo walionyesha kuridhiswa zaidi na namna mradi huo
unavyohusisha wananchi walio jirani na maeneo ya mradi ambao mbali na
kupata ajira za moja kwa moja pia wamepatiwa fursa ya kulima miwa ili
kukiuzia kiwanda hicho, hatua waliyosema kuwa itapunguza tatizo la ajira
na kuongeza kipato cha wananchi.
"Kingine
kikubwa zaidi kwa wadau hawa ni kuhakikisha kuwa mradi huu hauishii
kwenye kuzalisha sukari tu bali pia bidhaa zitokanazo na mabaki ya
malighafi za miwa ikiwemo ethanol, vyakula vya mifugo pamoja na
uzalishaji wa nishati umeme,'' alisema mjumbe Selemani Zedi huku
akiungwa mkono na wenzie akiwemo Mbunge wa Wawi Ali Salehe.
Akijibu
baadhi ya hoja za wabunge hao ambao pia walitaka kufahamu uwezekano wa
mifuko hiyo kuwekeza kwenye sekta ya uvuvi hapa nchini Waziri wa Kazi,
Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama alisema
uwezekano huo upo ikiwa mamlaka zinazosimamia mifuko hiyo zikiwemo bodi
pamoja na Mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii
(SSRA) zitaridhia miradi hiyo kwa kuangalia vigezo muhimu.
"Ili
kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama hii inahitaji ruhusa za mamlaka
mbalimbali zinazosimamia mifuko hiyo kwa kuwa mamlaka hizo pia
zinahitaji kujiridhisha pasipo kuacha chembe ya shaka kuwa utekelezaji
wa miradi hii haihatarishi fedha za wanachama japo habari njema ni
kwamba kati ya miradi 27 inayotarajiwa kutekelezwa na mifuko hii tayari
miradi 15 imepatiwa ruhusa ya utekelezwaji na mamlaka hizi,'' alisema.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,
Prof Godius Kahyarara pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa
PPF, Bw.William Erio, waliihakikishia kamati hiyo, serikali, wananchama
na wadau wote wa mifuko hiyo kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka ujao
mradi huo utakuwa tayari umeanza kuzalisha sukari pamoja na baadhi ya
bidhaa ambatanishi kulingana na wito wa wabunge hao.
"Mradi
huu mliotembelea leo unaolenga kuzalisha tani 50 za sukari kwa mwaka na
ni sehemu tu ya mradi mkubwa unaotekelezwa na mifuko yetu miwili yaani
NSSF na PPF ukiwepo mwingine mkubwa zaidi katika eneo la Ngerengere,
Wilaya ya Morogoro Vijijini unaofahamika kama Mkulazi I ambao unaolenga
kuzalisha tani 200,000 za sukari kwa mwaka,'' alisema Prof Kahyarara.
"Zaidi
tuwahakikishie tu waheshimiwa wabunge kuwa hoja zenu tumezipokea na
tutasimamia kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa wakati na zaidi
si tu kwamba tutalisha soko la ndani bali pia soko la nje hususani
mataifa jirani ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,''
aliongeza Bw Erio.
Naye
Mwakilishi wa jeshi la Magereza, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro
(RPO), Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP)Mzee Nyamka mbali na
kuishukuru mifuko hiyo pia alitoa wito kwa mifuko mingine ya hifadhi ya
jamii pamoja na wadau wengine kujitokeza ili kushirikiana na Jeshi hilo
katika utekelezaji wa miradi mingine huku akibainisha kuwa jeshi hilo
lina eneo kubwa la ardhi pamoja na nguvu kazi ya kutosha.
Mkuu
wa Mkoa wa Morogoro Dk Stephen Kebwe alisema mkoa wake umekuwa ukiupa
kipaumbele kikubwa mradi huo kuwa utekelezaji wake pamoja na mambo
mengine unalenga kuongeza ajira kwa wananchi wa mkoa huo na kupunguza
kabisa kasi ya mfumuko wa bei ya sukari kwa kuongeza uzalishaji wa
bidhaa hiyo muhimu.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Bw Mohamedi Mchengelwa
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba kubwa la
miwa lililopo katika gereza la Mbigiri lililopo Dakawa mkoani Morogoro
ambalo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha sukari kinachojengwa
kwa ubia kati ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF na jeshi la
Magereza nchini.
Waziri
wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama
(wa tatu kulia) akiwaongoza baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria kukagua shamba hilo.
Waziri
wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama
(katikati) akiwaongoza baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge inayohusika
na Katiba na Sheria chini ya mwenyekiti wake Bw Mohamedi Mchengelwa (wa
pili kulia) kukagua shamba hilo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk
Stephen Kebwe .
Waziri
wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba hilo.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF,
Prof Godius Kahyarara akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kukagua shamba hilo. Kwa mujibu wa Prof. Kahyarara hadi kufikia mwishoni
mwa mwaka ujao mradi huo utakuwa tayari umeanza kuzalisha sukari pamoja
na baadhi ya bidhaa ambatanishi ikiwemo uzalishaji wa umeme.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bw.William Erio, akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya kukagua shamba hilo. Erio
aliihakikishia kamati hiyo kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati na
utalisha pia soko la nje hususani mataifa jirani ya Burundi na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwakilishi
wa jeshi la Magereza, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro (RPO), Kamishna
Msaidizi wa Magereza (ACP)Mzee Nyamka akizungumza kwenye ziara hiyo.
Wadau wote wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Pamoja
na mambo mengine huo tayari umeanza kutoa ajira kwa wananchi wanaoishi
jirani na eneo la mradi kama walivyokutwa siku ya ziara.
Waziri
wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama
(Kushoto) akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambae pia
ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara mara baada ya
kumaliza ziara hiyo. Anaeshuhudia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Pensheni wa PPF, Bw.William Erio (Katikati)
No comments:
Post a Comment