Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji (R) Semistocles Kaijage
amewataka wasimamizi wa uchaguzi mdogo wa madiwani kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuepuka kuisababishia serikali
hasara.
Jaji
Kaijage ameyasema hayo leo (Tarehe 15.10.2017) mjini Dodoma wakati
akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa
uchaguzi.“…Tusipozingatia na kufuata taratibu za uchaguzi tunaweza
kusababisha kesi nyingi za uchaguzi na kuitumbukiza nchi katika gharama
ambazo zingeweza kutumika katika huduma za jamii,” ameonya Jaji Kaijage.
Mhe.
Kaijage amesema kuwa hamasa katika siasa za Tanzania imeongezeka sana
na kwamba kumekua na ongezeko la hali ya kutokuaminiana haswa katika
mchakato wa uchaguzi na kwamba endapo wasimamizi hawatafanya kazi yao
kwa ufasaha wataitumbukiza nchi kwenye matatizo makubwa.
“Mmeaminiwa
na kuteuliwa kwa sababu mna uwezo wa kufanya kazi hii, kitu cha muhimu
ni kujiamini na kujitambua. Pia kuhakikisha mnayajua vyema maeneo yenu
mnayofanyia kazi, kuhakikisha mnawatumia vizuri wasaidizi mlio nao kwa
matokeo bora,” alisema.
Jaji
Kaijage amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo juu ya jukumu lao la
kuimarisha imani ya wananchi kwa NEC, na kwamba Imani hiyo itadumishwa
endapo watafanya kazi kwa uwazi, uhuru na kwa ufanisi wa hali ya juu
bila kuegemea upande wowote.Ameogeza kusema kwamba uchaguzi ni mchakato
unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria na kikanuni
zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa.
“Hatua
na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na
usio na malalamiko au vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi kuanzia
utoaji wa fomu, uteuzi wa wagombea, uratibu wa kampeni, upigaji kura,
kuhesabu kura, kujumlisha hesabu za kura na kutangaza matokeo,” alisema.
Aidha,
Jaji Kaijage, amewaasa wasimamizi wenye uzoefu kujiepusha kufanya kazi
kwa mazoea na badala yake wazingatie mafunzo ambayo watapewa na tume
pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria
zinazosimamia uchaguzi.
Mkutano
huo wa ufunguzi ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Bw.
Ramadhan Kailima na maafisa wa kada mbalimbali wa NEC pamoja na
wasimamizi, wasimaizi wasaidizi na maafisa wa uchaguzi 230 ambao
walikula kiapo cha kuheshimu maadili ya uchaguzi.
Awali
Bw. Kailima amesema kwamba uchaguzi mdogo umepangwa kufanyika kwenye
Kata 43 tarehe 26 mwenzi Novemba, mwaka huu. “Uchaguzi mdogo unafanyika
kwenye Kata 43 ambazo zipo kwenye mikoa 19 kwenye Halmashauri 36 na
Majimbo 37 kwa hiyo uchaguzi huu mdogo unafanyika karibia maeneo ya nchi
nzima,” alisema Kailima.
Uchaguzi
huo unatarajiwa kuhusisha wapiga kura waliojiandikisha katika Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura wapatao 336,182 katika jumla ya vituo vya
kupigia kura 893 ambapo Kata yenye wapiga kura wengi wanafikia 58,622 na
Kata yenye wapiga kura wachache wanafikia 1,402.
No comments:
Post a Comment