Baadhi
ya mitambo ya Kiwanda cha Pamba cha Manonga wilayani Igunga ambayo
ilikuwa ikutumika kuchambua Pamba na kuzalisha mafuta yake ambayo
hafanyi kazi kwa kipindi kirefu baada ya wamiliki wake kusimamisha
uzalishaji. Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri( hayupo katika picha)
jana ametoa mwezi mmoja mitambo hiyo ianze kufanya kazi.
Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (aliye mbele) akiangalia mmoja wa
mitambo baaya kutembelea Kiwanda cha Pamba cha Manonga jana wilayani
Igunga kwa ajili ya kujionea hali halisi kilivyo hivi na mahitaji yake
ili kianze upya uzalishaji.
Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (kulia) akibadilishana mawazo na
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) Robert
Mayongela Jongera (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo
(kulia) baada viongozi mbalimbali kutembelea Kiwanda cha Pamba cha
Manonga jana wilayani Igunga kwa ajili ya kujionea hali halisi kilivyo
hivi na mahitaji yake ili kianze upya uzalishaji.
Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (kulia) akiwasisitiza wamiliki wa
Kiwanda cha Pamba cha Manonga kilichopo wilayani Igunga kuhakikisha
ndani ya mwezi mmoja mitambo ya kiwanda hicho iwe imeshaanza kazi.
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo. Mkuu wa Mkoa alitoa
maelezo hayo jana alikwenda kutafuta sababu za kwanini hakiendelei na
uzalishaji kwa zaidi ya miaka 20.
Na Tiganya Vincent-RS-Tabora.
SERIKALI
ya Mkoa wa Tabora imetoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa Kiwanda cha Pamba
cha Manonga kuhakikisha wamekikarabati ili kiweze kuanza tena uzalishaji
wa mafuta ya pamba na uchambuzi wa Pamba na kutengeneza ajira kwa
vijana mkoani hapo.
Agizo
hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri jana wilayani
Igunga wakati alipokwenda kujionea hali halisi ya kiwanda hicho ambacho
kwa maika zaidi ya 20 hakifanyi kazi.
Alisema
kuwa baada mwezi mmoja huo kukamilika atafanya ziara Kiwandani hapo ili
kuhakikisha kama ukarabati umeshakamilika na mitambo imeshaanza kufanya
kazi na kinyume cha hapo atalazimika kumwandikia Waziri wenye dhamana
na viwanda ili wamiliki wake wanyang’anye kwa ajili ya kumpa mwekezaji
mwingine.
Mwanri
aliwaagiza Wamiliki wa Kiwanda hicho ambao ni Rajani pamoja na Chama
Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo kupanga ratiba ya mpango kazi wa
utekelezaji shughuli zitakazoonyesha mipango ya ufufuaji na muda wa
ukamilishaji kwa ajili kufanikisha zoezi hilo ndani ya muda ulipangwa ,
vinginevyo watashindwa.
“Tengenezeni
ratiba itakayowasaidia katika upangaji wa mambo yenu,Mfano siku fulani
mnakwenda TANESCO kwa ajili ya kuomba umeme three phase ili kuachana na
ule single phase ambao mnasemaje hauwezi kuwasaidia katika uendeshaji wa
kiwanda chenu…kisha mnapanga siku ya kufuatilia upatikanaji wa maji
kiwandani mtaona mambo yanakwenda mbamumbamu na ukarabati ukamika kwa
wakati” alisisitiza Mwanri.
“Nataka
nikirudi hapa nikute mitambo inaunguruma…vingine nitamwita Mheshimiwa
Mwijage aje hapa kuchukua kiwanda hiki…sitaki mambo yafike huko fanye
kazi ili kiwanda kianze uzalishaji na vijana wetu wapate ajira” alisema
Mkuu huyo wa Mkoa.
Mmoja
wa Wabia katika Umikili wa Kiwanda cha Pamba cha Manonga Urveshi Rajani
alisema kuwa watahakikisha kuwa ndani ya mwezi mmoja Kiwanda hicho
kinakuwa tayari kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya pamba na uchambaji
wa zao hilo.
Alitoa
wito kwa viongozi kuhakikisha wanahamasisha wakulima kulima pamba kwa
wingi ili Kiwanda cha kiwe na malighafi za kosha kwa ajili ya uzalishaji
wa mafuta na uchambuzi wa zao hilo.
Naye
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU)
Jospeh Mihangwa alisema kuwa mitambo ya Kiwanda cha Pamba cha Mananga
ni mizuri na inasaidia kuchamba pamba bila kukatakata na hivyo kuwa na
soko kubwa duniani.
Alisema
kuwa kwa sababu ya ubora wa kiwanda hicho wao kama majirani na Mkoa wa
Tabora wako tayari kushirikiana na wamiliki wake kama watahitaji msaada
wa mafundi wa kusaidia kukarabati mitambo ili kianze tena uzalishaji kwa
sababu kiwanda hicho ni muhimu sana katika uchambuzi wa pamba.
“Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa kiwanda hiki ni kizuri sana kina mitambo ya Platt Lumus
ambacho wakati wa uchambuaji wa pamba haikati nyuzi na kufanya pamba
inachambua hapa iwe na bei kubwa katika soko la dunia…sisi kama watahiji
msaada wa mafundi wa kusaidia kufufua tuko tayari kuwasaidia” alisema
Meneja huyo Mkuu wa SHIRECU.
Kwa
upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga
Revocatus Kuuli aliwahakikishia Wamiliki wa Kiwanda cha Pamba cha
Manongo wasiwe na wasiwasi kuhusu upatikanaji malighafi ya kutosha kwa
ajili ya kiwanda hicho,kwani uongozi umeshajipanga kuhakikisha msimu
ujao wananchi walima Pamba kwa wingi na wanavuna pamba nyingi kuliko ya
msimu uliopita.
Alisema
pamoja na jitihada kuwa za muda mfupi msimu uliopita Wakulima katika
Wilaya ya Igunga walifanikiwa kuzalisha kilo 10, 700,000 ,msimu ujao
wanatarajia mavuno kuwa mara mbili ya kilo hizo na hivyo kuwa malighafi
nyingi kwa ajili ya viwanda..
Kiwanda
hicho kinamilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Igembensabo kwa
asilimia 20 na M/S Rajani Metals and Machinery Ltd mwenyewe anamikili
asilimia 80.
Kiwanda
cha Manonga ambacho kilijengwa mwaka 1958 na Kampuni ya wafanyabiashara
binafsi na mnamo mwaka 1962 Serikali ilikitaifisha na kuipatia Kampuni
ya Wakulima wa Kahama na Nzega (KANZECO) kina miaka zaidi ya ishirini
bila kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment