Pages

August 8, 2017

Waziri Lukuvi Akabidhi hati zaidi ya 4000 Dar


 Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi  akizungumza leo na wananchi wa mtaa Lungule juu ya kudhibiti matapeli wa ardhi, na migogoro mbalimbali ya ardhi hapa nchini.
Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob akizungumza mbele ya Wananchi leo katika hafla ya kukabidhi hati 88  kwa wakazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi mtaa Lungule waliokabidhiwa hati wakiwa katika picha ya pamoja.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.


Na Jonas Kamaleki-MAELEZO

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amekabidhi hatimiliki 88 kwa wakazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam kati ya 4333 ambazo ziko kwenye hatua za mwisho katika mradi wa urasimishaji wa makazi holela.

Akikabidhi hatimiliki hizo, Mhe. Lukuvi amesema hizi hati ni mtaji uliofufuliwa baada ya wakazi kukakaa na kuendeleza maeneo yasiyopimwa yaani mtaji mfu kwani hakuna mtu yeyote ambaye angewezakupata mkopo bila hati.

Mhe. Lukuvi amesema kuwa Serikali ya Aawamu ya Tano inayo dhamira ya dhati ya kurasimisha makazi nchi nzima ili kuongeza thamani ya ardhi au maeneo husika. Ardhi yenye hatimiliki thamani yake inaongezeka kwani inatambuliwa na taasisi za fedha ambazo ni rahisi kukuopesha wenye hati.

“Kwa hati hizi zilizotolewa takribani 4333 tukisema kila nyumba ikopeshwe kwa kiwango cha chini cha shilingi milioni 10, kwa siku ya leo Kimara inapata mtaji wa karibu bilioni 40.5,”alisema Mhe. Lukuvi.

Aliongeza kuwa maeneo yote ya miji ambayo hayajapimwa, yapimwe na halmashauri na manispaa zote nchini ili kuyaongezea thamani na kuondokana adha ya watu kujenga kwenye makazi holela.

Waziri huyo wa Ardhi amesema kuwa kwa sasa wakazi wa Kimara wameondoka kwenye kuitwa watu wanaokaa kwenye makazi holela na sasa wanajulikana kuwa wakazi wa maeneo rasmi.

Aidha, Mhe. Lukuvi ametoa onyo kali kwa matepeli wa ardhi kuacha vitendo hivyo mara moja kwani dawa yao ipo tayari. Ameongeza kuwa na madalali uchwara wa ardhi waache tabia ya kuwaonea wanyonge na kusababisha mali zao ziuzwe kwa njia ya udanganyifu.

“Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya matapeli hao ambao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya maafisa wasiowaaminifu,”alisisitiza Lukuvi.

Amewaonya wanaotunza mapori mijini kuwa wakae makini kwani watanyang’anywa wasipoendeleza maeneo hayo. Ameongeza kuwa na wale waliokuwa wanamiliki maeneo makubwa bila kuwa na hati itabidi waanze kulipa kodi ya pango la ardhi ili Serikali ipate mapato.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob amempongeza Mhe. Lukuvi kuwa ni mtu anayejali maendeleo ya wananchi bila kujali vyama vyao wala itikadi zao. Amesema Lukuvi anafuata nyayo za Mhe. Rais John Pombe Magufuli ambaye anafanya maendeleo kwa watanzania wote bila kujali vyama vyao.

Hivyo, amewataka wanasiasa wengine waige mfano wa Mhe. Rais Magufuli na William Lukuvi ili kuwaletea wananchi maendeleo pasipokuangalia vyama wala dini.

Naye mkazi wa Kilungule, Kimara ambaye amekadhiwa hati na Mhe. Lukuvi, Bwana Prackson Lugazia amesema hatua hii ya kupata hati ni jambo zuri na la kimaendeleo kwani ataweza kupata mikopo kwenye taasisi za fedha kwa kutumia hati hiyo.

“Nimefurahi sana kupata hati hii kwani kwa sasa ardhi yangu imeongezeka thamani kuliko ilivyokuwa awali,” alisema Lugazia.

Hati hizo zimetolewa kwenye mpango wa Urasmishaji wa Makazi Holela katika kata za Saranga na Kimara, jijini Dar es Salaam. Mpango huu umesimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na ni mpango darasa ambao unaweka msingi kwa ajili ya urasimishaji wa makazi nchi nzima.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...