Na Bushiri Matenda Na Agness Moshi - MAELEZO
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) imetoa rai kwa wadau wa Takwimu
Nchini kufuata kanuni na taratibu za utoaji takwimu ili kuepusha
sintofahamu baina yao, wapokeaji taarifa na Taasisi husika .
Rai
hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dkt. Albina Chuwa wakati
akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo kufuatia
taarifa zisizo sahihi zilizotolewa na Kampuni ya Utafiti ya Geopoll
yenye ofisi ya Kanda ya Afrika, mjini Nairobi, Kenya kuhusiana Viwango
na Idadi ya watazamaji wa vituo mbali mbali vya habari vinavyorushwa
hapa nchini .
“Taarifa
zozote zinazohusu utafiti ni lazima zihusishe wadau mbalimbali, na kwa
kuzingatia vigezo vyote vinavyotakiwa na mamlaka iliyoidhinishwa
kisheria kuhusiana na utoaji takwimu”, Dkt.Chuwa alivitaja vigezo hivyo
kuwa ni pamoja na uwazi na ukweli, uhusishwaji wa Wadau na kwa
kuzingatia weledi.
Aidha,
amefafanua kuwa ni vyema Taasisi yoyote inayotaka kukusanya taarifa
mbalimbali za takwimu ni budi kushirikisha wahusika ili kuepusha
mkanganyiko na upotoshwaji kama ilivyofanywa na Kampuni hiyo kutoka
Nairobi, Kenya.
“Takwimu
zinazotolewa bila kuzingatia taratibu zinazohitajika hazitatambulika na
Serikali kwani utoaji wa Takwimu haufanywi kama unavyohesabu migomba
shambani, hivyo ni lazima wahusika wafuate taratibu zote”, alifafanua
Dkt.Chuwa.
Dkt.Chuwa
amesema, Serikali haitambui Takwimu zilizotolewa hivi karibuni kupitia
mitandao ya kijamii kwani hazikufuata Sheria ya Takwimu na hazijakidhi
vigezo rasmi vya Takwimu na hivyo kuathiri mahusiano ya kiutendaji baina
ya vyombo vya habari hapa nchini.
Kufuatia
tukio hili, Ofisi ya Takwimu nchini inapenda kuzijulisha Taasisi
zinazojihusisha na utoaji wa taarifa zinazotokana na utafiti nchini
kwamba kwa mujibu wa Sheria ya 2015 NBS imepewa mamlaka ya kutoa,
kusimamia na kuratibu upatikanaji wa takwimu kwa ajili ya matumizi ya
Serikali na Wadau wa Takwimu.
Amesema,
kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria hiyo, kinaipa NBS jukumu la
kutoa na kusimamia miongozo na viwango vya utoaji rasmi wa Takwimu.
“Hapo awali Ofisi ya Taifa ya Takwimu haikua na meno lakini mara baada
ya marekebisho ya Sheria hiyo, sasa inayo meno ya kuiwezesha kudhibiti
utoaji holea wa Takwimu nchini” Amesisitiza Dkt. Chuwa.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi.
Zamaradi Kawawa amewataka Waandishi wa Habari kuacha kuandika taarifa
ambazo hazijathibitishwa na NBS, pia ambazo hazina mashiko kwa Wananchi
na Serikali kwa ujumla.
“Vyombo
vya habari nchini viache kushabikia taarifa zinazotolewa na Taasisi
zozote zisizo tambulika na kuthibitishwa na NBS hususani katika maswala
ya Takwimu”, alisisitiza Bi. Zamaradi.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria
ya Takwimu ya Mwaka 2015. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, NBS imepewa mamlaka
ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji wa Takwimu rasmi kwa ajili
ya matumizi ya Serikali na Wadau wa Takwimu.
Mkurugenzi
mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akiongea na waandishi
wa habari hawapo pichani katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Habari
maelezo Jijini Dar es Salaam , kushoto Bw. Ephraim Kwisigabo Mkurugenzi
Sensa na Takwimu za jamii.
No comments:
Post a Comment