Pages

August 5, 2017

Masauni awataka wananchi kuwafichua wahalifu, aamuru ujenzi wa kituo cha polisi Mbande uanze mara moja


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wananchi wa Mbande, Kata ya Chamazi, Tarafa ya Mbagala, Wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, wakati alipofanya ziara katika eneo hilo yenye lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo. Hata hivyo, Masauni aliamuru ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande ambao utajengwa kwa michango ya wananchi na Serikali uanze mara moja, na pia aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa kuwafichua askari polisi wanaohisiwa kushirikiana na wahalifu katika eneo hilo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia), akimsikiliza Mkazi wa Mbande, Mbagala, jijini Dar es Salaam, Muhidin Maftaa alipokua anamuuliza swali kuhusu hali ya ulinzi na usalama katika eneo hilo. Ambaye alifanya ziara katika eneo hilo yenye lengo la kuimarisha ulinzi na usalama, aliamuru ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande ambao utajengwa kwa michango ya wananchi na Serikali uanze mara moja, na pia aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa kuwafichua askari polisi wanaohisiwa kushirikiana na wahalifu katika eneo hilo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Gilles Muroto,alipokuwa anajibu mswali mbalimbali ya wananchi wa Mtaa wa Magengeni Mbande, Mbagala, jijini Dar es Salaam. Masauni alifanya ziara katika eneo hilo yenye lengo la kuimarisha ulinzi na usalama na aliamuru ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande ambao utajengwa kwa michango ya wananchi na Serikali uanze mara moja, na pia aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa kuwafichua askari polisi wanaohisiwa kushirikiana na wahalifu katika eneo hilo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akiwasalimia Maafisa wa Jeshi la Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa anawasili katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya ziara kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali wilayani Temeke. Kushoto ni Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Gilles Muroto. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Na Felix Mwagara (MOHA)

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amewataka wananchi wa Mbande, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahalifu ambao wanahatarisha amani na utulivu katika eneo hilo.

Masauni pia aliwataka wananchi wa eneo hilo, wawasiliane na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke endapo watamuona askari polisi wa Kituo kidogo cha Polisi Mbande au sehemu yoyote wilayani humo anashirikiana au anawatetea wahalifu katika eneo wanaloishi.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Mtaa wa Magengeni Mbande, Kata ya Chamazi, wilayani humo, Masauni alisema Serikali ya Magufuli inapambana kwa kuwaletea maendeleo wananchi wake, kuwajali na kuwalinda usiku na mchana, hivyo serikali haitakubali amani na utulivu wa eneo husika ipotee.

“Rais Magufuli anapambana kukuza uchumi wa nchi hii, viwanda vinajengwa sehemu mbalimbali nchini, safari za nje zimezuiliwa, mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo mheshimiwa Rais ana dhamira nzuri ya maendeleo ya nchi hii, nasisi wasaidizi wake pamoja na wananchi wote kwa ujumla tunapaswa kumuunga mkono Rais wetu,” alisema Masauni.

Alisema maendeleo yanayoonekana nchini yanaendana na amani katika maeneo yetu, hivyo ili nchi ijengwe pia inahitaji amani, na ndio mana Jeshi la Polisi halilali linafanya kazi kubwa kwa ajili ya kulinda amani ya wananchi, na ndio mipango thabiti ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Masauni kabla ya hotuba yake kwa wakazi wa eneo hilo, alisomewa taarifa ya Kata hiyo ya Ulinzi na Usalama na kuona jinsi wananchi wa eneo hilo walivyojitoa kuchanga fedha na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Mbande ambacho alielekeza ujenzi wa kituo hicho uanze haraka iwezekanavyo kwa kuwa wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo wamejitoa kuchangia ujenzi huo kwa kiasi kikubwa.

“Kutokana na jinsi mlivyojitoa katika kuchangia fedha pamoja na mahitaji mbalimbali ya ujenzi wa kituo cha polisi Mbande, nimefarijika sana na hatua hiyo na nina aamuru ujenzi uanze hata leo, waambieni wadau mbalimbali waliotoa ahadi sasa waanze kutekeleza,” alisema Masauni.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Gilles Muroto alipokea maelekezo ya ujenzi wa Kituo cha Polisi kuanza na aliahidi bega kwa bega kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi wa eneo hilo katika kukifanikisha kituo hicho kinakamilika.

“Ujenzi wa kituo hiki kitasaidia sana katika mapambano ya wahalifu katika maeneo yetu, hata hivyo tunaomba ushirikiano wenu wa kuwafichua wahalifu mbalimbali katika eneo mnaloishi,” alisema Muroto na kuongeza; “Nawaomba viongozi wa Serikali ya Mtaa akikisheni mnawajua wageni wanaokuja kupanga au kuuza nyumba, maana kuna wahalifu wanawatumia madalali kuuza nyumba au kupanga chumba, hivyo msiwapangishe watu msiowajua, kuweni makini.”

Hata hivyo, Muroto katika kuhakikisha ulinzi unaimarishwa zaidi katika eneo hilo, alitoa namba yake ya simu ya mkononi na kuwaelekeza wananchi katika mkutano huo, wawe huru kuitumia simu hiyo katika matukio mbalimbali ya kikazi kwa lengo la kuwasambaratisha wahalifu na pia kama watapata uonevu wowote dhidi yao kwa kutokutendwa haki na baadhi ya askari polisi wasiokuwa waaminifu na kazi zao, wananchi hao wampigie.

Katika hatua ya kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kujitolea kuchanga fedha na kutoa vifaa vya kujenga kituo cha polisi, Masauni naye alitoa mchango wa shilingi milioni mbili ili kufanikisha ujenzi wa vituo viwili wilayani humo, ambapo tayari Benki ya CRDB Mbande ilitoa ahadi ya kutoa shilingi milioni kumi, Mbunge wa Jimbo la Mbagala alitoa mifuko ya saruji, wafanyabiashara, viongozi wa CCM, wananchi mbalimbali nao walijitoa kuchanga fedha ambazo zilikusanywa na Kamanda wa Polisi Muroto.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...