Pages

August 10, 2017

DKT TIZEBA: SEKTA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI ITAENDELEA KUWA KICHOCHEO CHA UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe Dkt Dk Charles Tizeba akisisitiza jambo kabla ya kufungwa kwa Maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi .

Na Mathias Canal, Lindi

Serikali imesema kuwa  Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi itaendelea kuwa muhimili na kichocheo katika kujenga uchumi wa viwanda ambao ndio kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli. 

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Dkt Charles Tizeba  wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima, nane nane kitaifa, katika viwanja vya ngongo katika manispaa ya lindi jana tarehe 8/8/2017.

Dkt Tizeba alisema kuwa kwa ushirikiano na Watumishi wote katika Wizara, amejipanga kuhakikisha kuwa, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inaendelea kukua sawa sawa na mahitaji ya Wananchi. 

Alisema kuwa jambo hilo linawezekana ambapo inawezekana kwa kiasi kikubwa kuzalisha malighafi za kutosha za kuwezesha viwanda kuzalisha bidhaa mbalimbali, ambazo zitauzwa ndani na nje ya nchi kwa bei nzuri na ya ushindani. 

Alisema kuwa kupitia mbinu hiyo wizara itakuwa imefanikisha kuongeza mchango wa Sekta hizo katika uchumi wa Taifa na pia katika kuondoa umaskini kwa Watanzania wengi.

Sambamba na hayo pia Mhe Dt Tizeba alisema kuwa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, mabadiliko ya tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa uzalishaji na tija ya mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji.  

Katika kukabiliana na jambo hilo Mheshimiwa Dkt Tizeba alisema kuwa Wizara yake imejipanga kuendelea, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora zinazovumilia ukame, magonjwa na kutoa mavuno mengi. 

Alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Wabia wa Maendeleo, wamekamilisha Mpango wa Kilimo Kinachohimili Mabaliliko ya Tabianchi na Miongozi ya uzalishaji mazao, ufugaji na uvuvi. Muongozo wa kilimo umetolewa kulingana na Kanda za Kilimo za Kiteknolojia. Miongozo hiyo, imezinduliwa na kuanza kusambazwa kwa Maafisa Ugani wa Kilimo Mifugo na Uvuvi na kwa wananchi, kuanzia Mwezi, Mei na Juni, 2017. 

Alisema Mikakati mingine, inayoendelea ni pamoja na kuhakikisha kuwa mbolea bora, inapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu zaidi, sawasawa na agizo la Makamu wa Rais la kuwasaidia Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kupunguza gharama za uzalishaji ili waweze kufaidika na matunda ya juhudi zao.   

Sambamba na hilo aliongeza kuwa wizara yake imejipanga ili kuhakikisha kuwa inaendelea kuwaelimisha na kuwasaidia Wafugaji wa Tanzania, kufuga kitaalamu zaidi ili kuepuka hali ya kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho na maji. 

Alisema kuwa jambo hilo litawezesha kufuga kwa tija na pia kupunguza migogoro ya Wakulima na Wafugaji.


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...