Pages

July 28, 2017

SERIKALI YATOA SIKU 30 KWA WAAJIRI KOTE NCHINI KUJISAJILI NA MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI, (WCF), VINGINEVYO HATUA ZA ADHABU ZA VIFUNGO NA FAINI KUTEKELEZWA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, (kulia), akizungumza leo Julai 27, 2017 wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa kushtukiza kwenye Hospitali ya K’s iliyoko eneo la Mafyati jijini Mbeya ili kubaini kama mwajiri kwenye hospitali hiyo amejisajili katika  Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF). Waziri ametoa siku 30 kwa waajiri kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara, kujisajili na Mfuko huo, vinginevyo watakabiliwa na adhabu mbalimbali ikiwemo faini ya shilingi milioni 50, kifungo cha miaka 5 jela au vyote kwa pamoja. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdusalaam Omar.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, ametoa siku 30 kwa waajiri wote nchini ambao hawajasajili, kujisajili katika Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi (WCF), na kutoa michango kwa wakati, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Waziri Mhagama alitoa agizo hilo jijini Mbeya Julai 27, 2017 wakati wa zoezi la ukaguzi wa kushtukiza jijini humo kuwabaini waajiri ambao bado hawajatekeleza Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 Marejeo ya Mwaka 2015 kifungu cha 5, ambayo inawataka waajiri wote kutoka sekta ya Umma na Binafsi, Tanzania Bara kujisajili kwenye Mfuko huo.

“Mwajiri ambaye hajajisajili kwenye Mfuko, anaweza kufikishwa mahakamani na adhabu ni pamoja na kutozwa faini ya kiasi cha fedha kisichozidi shilingi milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka 5 jela au vyote kwa pamoja, hivyo nawasihi waajiri kutoka sekta binafsi na umma Tanzania Bara ambao hawajasajili kutekeleza sheria hiyo inayowataka kujisajili WCF katika muda huo nilioutoa.” Alisisitiza Mhe. Waziri Jenista Mhagama.

Katika ziara hiyo ya ukaguzi wa kushtukiza Mhe. Waziri alifuatana na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Mfuko huo, Bi. Laura Kunenge na Afisa Kazi wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Mary Patrick Mwansisya ambapo taasisi ya kwanza ambayo Mhe. Mhagama aliikagua ni Hospitali ya K’s iliyoko eneo la Mafyati na St. Aggrey iliyoko Uyole na kubaini kuwa taasisi hizo hazijajisajili katika Mfuko.

Aidha Waziri alitoa siku saba kwa waajiri wote Mkoani Mbeya wapatao 107 ambao bado hawajajisajili ikiwemo Hospitali ya K’s na Shule ya sekondari St. Aggrey kujisajili ndani ya muda huo.

“Mkishindwa kutekeleza agizo hilo maana yake mnatuelekeza kutumia kifungu cha 71(4), cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kinachotamka adhabu ya faini ya kiasi cha fedha kisichopungua shilingi milioni 50, kifungo cha miaka 5 jela au vyote kwa pamoja.” Alisema.

Aidha Waziri Jenista alihimiza kuwa mwajiri anapojisajili na Mfuko pia atimize wajibu wa kisheria wa kuchangia katika Mfuko kwa wakati stahiki. Mhe. Waziri alisema nia ya Serikali ya awamu ya Tano sio kuwatisha waajiri bali ni kuhakikisha wanafuata sheria ili hatimaye, wafanyakazi wapate haki yao stahiki pindi wanapoumia, kuugua ama kufariki wakati wakiwa wanatekeleza majukumu ya mwajiri wao kwa mujibu wa mkataba wa ajira.

Akifafanua zaidi Waziri alisema, takwimu zilizopo katika Mfuko za kipindi cha mwaka 2015/16 na 2016/17 zinaonesha kuna jumla ya waajiri 229 jijini Mbeya na kati yao ni waajiri 107 tu ndiyo waliojisajili katika Mfuko.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Tathmini wa WCF, Dk. Abdulsalaam Omar alisema Mfuko unamshukuru Mhe. Waziri kwa kushiriki katika ukaguzi huu wa kwanza wa aina yake kufanyika tangu Mfuko huu uanzishwe mnamo mwaka 2015 na kwamba Mfuko utasimamia na kutekeleza maagizo ya Mhe. Waziri.

"Kwa kipindi chote hicho Mfuko umekuwa ukijikita zaidi katika kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo waajiri ili waweze kuelewa umuhimu wa kujisajili katika Mfuko na faida ambazo mwajiri na mfanyakazi atazipata pindi anapoumia, kuugua au kufariki wakati akitekeleza majukumu ya mwajiri,” alisisitiza Dkt Omar.

Akifafanua zaidi, Mkurugenzi huyo alisema katika kazi ya uelimishaji kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 Mfuko ulitoa elimu kwa waajiri wapatao 4,901 kuhusu haki na wajibu lakini pia kuelewa sheria kuhusu wajibu wa waajiri kujisajili katika Mfuko. Aidha Mfuko umekuwa ukitumia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari, semina lakini pia kwa kuwaandikia waajiri kuhusu umuhimu wa wao kutekeleza sheria hiyo kwa kujisajili katika Mfuko na kutoa Michango kwa wakati kama ambavyo sheria inaelekeza.

Dkt Omar alisema Mfuko ulianza kutekeleza majukumu yake tarehe 1 Julai 2015 kama ilivyoelekezwa katika tangazo la Serikali Na. 169/2015 ambapo majukumu hayo ni pamoja na kusajili waajiri, kukusanya michango na kulipa fidia stahiki.Tayari Mfuko umeanza kulipa fidia kwa wafanyakazi walioumia, kuugua ama kufariki kuanzia tarehe 1 Julai 2016.

Ili mfanyakazi aweze kulipwa fidia, ni lazima mwajiri wake awe amechangia katika Mfuko, hivyo waajiri wanao wajibu kisheria chini ya Vifungu vya 71 – 78 vya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kujisajili, kuwasilisha michango, kutoa taarifa ya matukio ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi pamoja na kuwasilisha mapato ya mwaka." Alifafanua Dkt. Omar.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha Mfuko huo, Bi. Laura Kunenge alisema, "Tamko alilotoa Mhe. Waziri wetu litakuwa chachu kwa waajiri wengine nchini kujiunga na Mfuko kwa kujisajili na kuwasilisha michango kwa wakati na hivyo kuwezesha kufikia lengo la Mfuko la kulipa Fidia Stahiki kwa wakati." Alisema.

Bi. Kunenge pia alisema, Ofisi za WCF ziko wazi na kwamba huduma za Mfuko huo zinapatikana kila mkoa hapa Tanzania Bara ambapo Maafisa Kazi wa Mikoa ndio wanafanya kazi kwa niaba ya Mfuko kwa sasa.
 Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Mfuko huo, Bi. Laura Kunenge. (kushoto), na Afisa Kazi Mkoa wa Mbeya, Bi.Mary Patrick Mwansisya, (kulia), wakiuliza alipo mkurugenzi wa Hospitali ya K's mara baada ya kuwasili na waziri Mhagama katika ziara ya ukaguzi wa kushtukiza leo Julai 27, 2017.
 Waziri Mhagama, (wakwanza kulia), Bi. Laura na Dkt. Omar, wakimsubiri Mfanyakazi huyu wa K's Hospital akiwasiliana kwa simu na mwajiri wake ili kumjulisha uwepo wa Waziri na ujumbe wake kwenye hospitali hiyo.
 Maafisa wa polisi wakiwa tayari kuhakikisha usalama unazingatiwa wakati wa zoezi hilo.
 Waziri Mhagama na Dkt. Omar(kushoto), wakisubiri ujio wa Mkurugenzi wa hospitali ya K's
 Afisa Matekeelzo Mwandamizi wa WCF, Bw.Dan Kapogo, (kulia), akijadiliana jambo na Afisa Kazi Mkoa wa Mbeya, Bi.Mary Patrick Mwansisya.
  Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Mfuko huo, Bi. Laura Kunenge. (kushoto), Afisa Matekelezo Mwandamizi wa Mfuko huo Bw. Dan Kapogo,na Afisa Kazi Mkoa wa Mbeya, Bi.Mary Patrick Mwansisya, wakijadiliana jambo.
 Mhe. Mhagama akisalimiana na Mkurugenzi wa Hospitali ya K's Dkt.Victoria Kanama, baada ya kuitwa ili aonane na waziri kueleza kwa nini hajajisajili na Mfuko licha ya kupatiwa elimu lakini pia kujulishwa kwa barua.
 Dkt. Omar, Kulia), akimuongoza waziri Mhagama wakati wakitoka kwenye Hospitali ya K's baada ya ukaguzi. (wakwazna kushoto) ni Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dkt.Victoria Kanama.
 Dkt. Omar akitoa shukrani za WCF kufuatia ziara hiyo ya kushtukiza aliyofanya Mhe. Waziri na kubainisha kuwa maagizo hayo yatasimamiwa na kutekelezwa.
 Bi. Kunenge na Bw. Kapogo kutoka WCF wakijadiliana jambo
 Mratibu wa Hospitali ya K's Bw.Mtunda Mwankwasya akizungumza.
  Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Mfuko huo, Bi. Laura Kunenge
 Afisa Kazi Mkoa wa Mbeya, Bi.Mary Patrick Mwansisya akizungumza. "Tumewapa taarifa waajiri wote mkoani Mbeya hivyo wanajua fika kuhusu sheria hii inayowataka kujisajili na kutoa Michango katika Mfuko.
 Dkt. Omar akiteta jambo na Mhe. Waziri Mhagama.

 Waziri akitoka kwenye Hospitali ya K's akiongozana na Mratibu wa hospitali hiyo,Bw.Mtunda Mwankwasya
 Mkuu wa shule ya St. Aggrey.

Waziri Mhagama akizungumza mbele ya Meneja wa shule ya St. Aggrey, Bw.Melas Paul Mdemu

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...