Pages

June 10, 2017

RC TABORA ASEMA KUWEKA MAKUNDI KATIKA MABARAZA YANARUDISHA NYUMA MAENDELEO YA WANANCHI

Na Tiganya Vincent, NZEGA

Madiwani katika Halmashauri za  Mkoa wa Tabora  wametakiwa kuepuka kujenga makundi miongoni mwao ambayo yamekuwa yakisababisha wananchi waliowachagua kuchelewa kupata maendeleo kwa sababu ya muda mwingi kushughulikia migogoro badala ya kutatua matatizo mbalimbali ya wananchi.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri wakati akifunga mafunzo ya siku nne ya Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Tabora yaliyofanyika wilayani Nzega  kuhusu jitihada za jamii kupitia mbinu shirikishi jamii ya fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD) iliyoboreshwa na usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo (LGDG)

Alisema makundi yatawafanya washindwe kuwajibika vizuri na kujikuta miaka mitano ya uongozi wao inakwisha bila kuwafanyia chochote wananachi zaidi ya kupigania kuondoana katika uongozi badala kukazania maslahi ya wananchi.

“Nyie ndio mliko zamu sasa mkiendekeza makundi na migogoro isiyokwisha, mtajikuta zamu zenu zinamalizika hamjawafanyia chochote wananchi waliowachagua badala yake kupambana kila mnapokutana katika vikao vyenu ….kila kikao itakuwa sisi hatumutaki fulani atuongoze au fulani fulani hatufai” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.

Bw. Mwanri aliongeza kuwa wakimruhusu Shetani wa namna hiyo apite kati yao hakuna tena kazi wala maendeleo kwa wananchi wao waliowachagua.

Alisisitiza kuwa viongozi wa aina hiyo wanakuwa wamekosa sifa ya kuendelea kuaminiwa na jamiii iliyowachagua tena kuwatetea wananchi katika matatizo yanayokwamisha maendeleo yao.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Madiwani wote washirikiane bila kujali itikadi za vyama vyao, dini zao, kabila zao katika kuhakikisha kuwa wanatetea vyema wananchi wao na wanasimamia vyema watendaji wa Halmashauri zao kwa ajili ya kuwaletea wananchi maisha bora.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Leopold Chundu Ulaya alisema kuwa mafunzo walipatiwa na wawezeshaji kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na TAMISEMI yatawasaidia kuhakikisha kuwa miradi yote inatekezwa kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Alisema kuwa watajitahidi kuunganisha nguvu kwa pamoja kwa kubadilika ili kuhakikisha kuwa wanatatua matatizo ya wananchi waliowachagua na kuwaletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
RC TABORA KUWACHUKULIA HATUA WATETEZI WA WAKOSAJI.
Na Tiganya Vincent
Nzega

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri amesema kuwa atawachukulia hatua ikiwemo kuwapeleka katika Mamlaka zao za uteuzi viongozi na Madiwani ambao wamekuwa wakijitokeza kuwatetea watumishi waliosimamishwa au kufukuzwa kwa  makosa mbalimbali kama vile ubadhirifu wa mali za umma .

Bw. Mwanri alitoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya siku nne ya Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Tabora yaliyofanyika wilayani Nzega  kuhusu jitihada za jamii kupitia mbinu shirikishi jamii ya fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD) iliyoboreshwa na usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo (LGDG)

Alisema kuwa imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo mtumishi anakuwa ametuhumiwa kwa makosa mbalimbali na kusimamishwa ili kupisha uchunguzi tuhuma zake kunajitokeza baadhi ya  madiwani au viongozi kujifanya wao ni watetezi wake bila  kujali hasara iliyotokana na utendaji wake na utovu wa nidhamu.

Bw. Mwanri alisema hali hiyo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya Halmashauri kwa sababu ya baadhi ya Madiwani au viongozi fulani kuwa na maslahi binafsi na mtuhumiwa kwa sababu wanaona kuwa kutokuwepo kwake ni pigo kwao.

Alisisitiza kuwa somo la wajibu na maadili walilofundishwa linawataka kuhakikisha kuwa wanakuwa wazalendo kwa kulinda maslahi ya wananchi na sio kikundi fulani cha waharifu au wezi.

“Nikimsikia mtu anamtetea mtumishi aliyefukuzwa au kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu naanza nay eye kama yuko katika uwezo wangu nitamdoa  na yeye ili akamtetee vizuri akiwa nje  …na kama ni Diwani nitampeleka katika Chama chake kwa kuwa ndio kilichompa dhamana ya kwenda kwa wananchi kuomba kura ili aweze kuchukuliwa hatua kwa sababu ya kuwasaliti wananchi waliomchagua” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Aliwataka Madiwani wawe na uchungu na wananchi kwanza na kuacha kutetea maovu katika Halmashauri zao kama wanahitaji maendeleo ya watu wao yaonekana na  majina yao yawekwe kwenye Historia nzuri na sio ile ya kudharauliwa hata na vijana wadogo.

Naye Afisa Utumishi , Ofisi ya Rais-TAMISEMI Debora Mkemwa akitoa mada kuhusu nidhamu kwa watumishi na mashauri ya nidhamu kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa alisema kuwa uchunguzi wa awali unafanyika kabla ya hatua za kinadhamu kwa mtumishi  hazijachukuliwa ili kujiridhisha iwapo zipo sababu za msingi za kuanzishwa mchakato huo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...