Pages

May 27, 2017

ZINGATIA HAYA UNAPOTAKA KUENDESHA GARI UMBALI MREFU



Na Jumia Travel Tanzania

Linaweza kuwa si jambo la kushangaza kuwaona watu wakisafiri kwenye usafiri wao binafsi kuelekea mikoa mbalimbali nchini Tanzania. Na hii ni kutokana na maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi miongoni mwa watanzania wengi ambapo hapo awali walikuwa wanategemea usafiri wa umma.

Sababu za kusafiri zinaweza kuwa nyingi kama vile kifamilia, kutembelea ndugu na jamaa au vivutio mbalimbali vya kitalii. Lakini je ni wangapi wanayafahamu mambo ya kuzingatia kabla ya kuamua kuingia barabarani na usafiri binafsi kwenda umbali mrefu? Jumia Travel imekukusanyia masuala muhimu ambayo usipokuwa makini kuyafuata basi safari yako itakuwa ni shubiri badala ya asali huko njiani.

Jipange kwa safari nzima. Sidhani kama kuna jambo ambalo unaweza kufanikiwa bila ya kujipanga. Vivyo hivyo unapotaka kusafiri ni lazima uweke mipango madhubuti tangu mwanzo mpaka mwisho wa safari yako. Kwa mfano, safari itachukua muda gani, hoteli gani mtafikia, gari utakalolitumia litawatosha watu wangapi, gari litahitaji mafuta kiasi gani mpaka kumaliza safari, nini cha kufanya inapotokea dharura na kadhalika.   

Chunguza usafiri wako. Barabarani kuna mengi yanatokea ingawa kuna mengi unaweza kuyadhibiti endapo utachukua tahadhari kabla. Kwa mfano suala la gari kuharibika njiani linaweza kuepukika endapo utachukua muda wako kulipeleka kwa fundi kufanyiwa uchunguzi na matengezo pale yatakapohitajika. Huwezi jua inawezekana injini isingeweza kukupeleka hata nusu ya safari yako au jaribu kuvuta picha gari linapokuharibikia katikati ya msitu wenye wanyama wakali bila ya msaada.
Hakikisha usafiri wako umekidhi vigezo vyote vya kuwa barabarani. Kusafiri umbali mrefu hususani kutoka katikati ya jiji haimaanishi kwamba huko barabarani sheria hazifuatwi. Kwa hiyo hakikisha kuwa usafiri wako umekidhi vigezo vyote vya kuwepo barabarani kama vile leseni ya udereva, bima ya gari, leseni ya barabarani na sheria nyinginezo. Usipofanya hivi unaweza kujikuta unalipishwa faini, kukamatwa na hivyo kupotezewa muda ambao ilibidi uutumie kukufikisha huko uendako. Kwa mfano sio umefika Bagamoyo tu askari wa barabarani wanakukamata na kukuambia vibali vya gari lako kuwa barabarani vimekwisha muda wake.

Tarajia changamoto mbalimbali barabarani. Ni mara chache kusafiri barabarani bila ya kukutana na changamoto zozote kama vile foleni, njia kuwa mbovu, ukaguzi wa mara kwa mara, ajali na kadhalika. Hivyo lazima ujiandae kiakili wewe kama dereva pamoja na watu unaosafiri nao.
Usibebe mizigo mingi sana. Sawa mizigo ni muhimu kwa kuwa unasafiri umbali mrefu lakini kwa kufanya hivyo unaweza kujinyima fursa ya kubeba vitu vingine utakavyovutiwa navyo njiani. Hivyo basi hakikisha unabeba mizigo ambayo ni muhimu kwako kwani unaweza kupita sehemu na ukakuta vitu vya gharama nafuu ambavyo unaweza kununua.

Beba ramani ya kukusaidia huko uendako. Wengi wetu huwa tunapenda kwenda sehemu ambazo tunazifahamu hivyo inakuwa sio lazima sana kuwa na ramani ya kukupa mwongozo. Lakini siku hizi maendeleo ya teknolojia yamekuwa ni makubwa kwani sehemu nyingi zimewekwa kwenye ramani kupitia vifaa mbalimbali kama vile kompyuta, tabiti na simu. Mbali na teknolojia kurahisisha hilo lakini unashauriwa kubeba ramani ya karatasi, kwa mfano kama unanda Zanzibar unaweza kuwa na ramani inayokuonyesha sehemu zote za kule.
Kuwa na nyimbo au vitu vya kukuburudisha njiani. Kazi na dawa huwa wanasema Waswahili. Haimaanishi kwa sababu unasafiri umbali mrefu basi ndiyo uwe makini na usukani pasipo kujiburudisha. Beba vitu kama vile CD za muziki zenye nyimbo uzipendazo pamoja na michezo mbalimbali kwa ajili ya watoto wako kama unasafiri nao. Lakini pia hata vinywaji na vitafunwa vinaweza kuifanya safari iwe ni fupi na ya kuifurahia.

Beba pesa ya akiba. Unaposafiri njiani unaweza kukutana na changamoto ambazo zitahitaji pesa ya papo kwa papo ili kuweza kuzitatua. Hivyo hakikisha unakuwa na kiasi cha pesa taslimu kwani mara nyingi sehemu za kuzipata huwa ni nadra. Pia itakusaidia hata kununua vitu vya njiani, kwa mfano Morogoro kuna bidhaa nyingi sana kutoka kwa wakulima.  

Jaribu kuipumzisha simu yako kwa muda. Itakuwa haileti maana kuwa upo kwenye usafiri pamoja na wenzako au familia yako lakini unawasiliana na watu uliowaacha ulipotoka. Lengo la safari za namna hii mara nyingi ni kujaribu kubadili na kufurahia mazingira mapya. Basi jaribu kuendana na mazingira hayo kwa kuzungumza na wenzako ndani ya gari ninaamini kutaifanya safari kuwa ni ya kusisimua zaidi.  

Piga picha kwa ajili ya kumbukumbu. Ni muhimu kuwa na kumbukumbu ya baadhi ya matukio unayoyaona. Siku hizi kamera inapatikana kwenye simu za mkononi hivyo kurahisisha kuhifadhi kumbukumbu ya matukio mbalimbali. Basi hakikisha unapiga picha za sehemu na matukio utakayovutiwa nayo au hata wewe mwenyewe ukiwemo ili iwe kama ni ukumbusho kwako. Kwa mfano haiwezekani ukapita mbuga ya Mikumi bila ya kupiga picha ya Tembo au pundamilia wanaokatiza barabarani.
Kusafiri kwa kutumia gari binafsi hususani umbali mrefu ni starehe kubwa ambayo wengi bado hawajaigundua. Wapo wengine wanapanda ndege ili kuwahi kufanya vitu vingi huko waendapo pamoja na kuepuka uchovu. Lakini Jumia Travel inasisitiza kwamba kusafiri kwa njia ya barabara kunakupa fursa kubwa ya kujionea ni jinsi gani nchi yako imebarikiwa na fursa ya kujifunza mengi zaidi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...