Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, akimkaribisha Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma
za Jamii, Bw. Eliabi Chodota kutoa mada kwenye semina ya mtangamano
inayoendelea Kisiwani Pemba. Ushiriki na mwitikio katika semina hiyo
umekuwa mkubwa kwa washiriki ambapo wameonekana kuvutiwa sana na semina
hii pia wamekuwa wadadisi wazuri wa kutaka kujua zaidi fursa zinazo
patikana kwenye mtangamano huo.
Bw. Chodota akitoa mada kwenye semina ya mtangamano inayoendelea Pemba.
Sehemu ya washiriki wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikitolewa na Bw. Chodota (hayupo pichani).
Bw. Chodota akiendelea kutoa mada yake.
Mmoja wa washiriki Bi. Kauthari akiuliza swali mara baada ya mada kumalizika kutolewa na Bw. Chodota hayupo pichani.
Sehemu nyingine ya washiriki wakimsikiliza kwa makini.
Bw. Chodota akijibu swali lililokuwa limeulizwa na Bi Kauthari (hayupo pichani).
Bw.
Suleimani Haji kutoka ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Zanzibar naye akitoa mada kuhusu nafasi ya Zanzibar kwenye
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza kwa makini Bw. Suleimani (hayupo pichani).
Washiriki wakisikiliza kwa makini mada na maswali yaliyo kuwa yakiulizwa na washiriki wengine.
Mhe.
Mbarouk Salim Ali Mbunge wa Jimbo la Wete akiuliza swali kwenye semina.
Pembeni yake ni Mbunge wa Jimbo la Konga, Mhe. Mbarouk Ali akisikiliza
kwa makini.
Meneja wa TRA kwa upande wa Kisiwani Pemba Bw. Habibu Saleh naye akiuliza swali kwa mtoa mada, Bw. Suleimani (hayupo pichani).
Bw. Salehe akijibu maswali hayo na kutolea ufafanuzi kwa baadhi ya mambo.
Serikali
ya Zanzibar inashiriki moja kwa moja bila ukomo katika masuala yote ya
Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo Wazanzibari
wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Jumuiya hiyo na
kuondokana na dhana kuwa eti, Serikali yao inabaguliwa.
Akiwasilisha
mada leo kuhusu ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwenye semina ya masuala ya mtangamano wa EAC inayofanyika Pemba, Afisa
wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Bw. Suleima Haji alitoa ufafanuzi wa kina kuonesha
namna Zanzibar inavyoshiriki katika EAC.
Bw.
Haji alieleza kuwa licha ya Zanzibar kuwa sehemu ya muungano wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ushiriki wake umedhihirika katika mgawanyo wa
miradi ya maendeleo ya EAC, hususan miradi ya Miundombinu. Alisema
Zanzibar iliwasilisha mapendekezo ya miradi 10 kwenye Sekretarieti ya
EAC na kutokana na vipaumbe vilivyowekwa miradi 3 imekubaliwa na
mchakato wa kuitekeleza unaendelea. Miradi hiyo ni ujenzi wa Bandari ya
Marhubi kisiwani Pemba, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na ununuzi
wa meli kubwa zitakazosafirisha abiria na mizigo kwenye nchi wanachama
wa EAC.
Aidha,
kwenye miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Zanzibar haijasahaulika. Zanzibar inanufaika na miradi
inayofadhiliwa na taasisi inayojihusisha na masuala ya kukuza biashara
na kupunguza umasikini katika nchi za EAC inayoitwa "East Africa
Trademark" (TMEA). TMEA ambayo ni mdau mkubwa wa EAC inafadhili mradi
ambao unawawezesha Wazanzibari kufanya maombi kwa njia ya mtandao ili
kupata cheti cha uasili wa bidhaa. Cheti hicho ni muhimu kwa
wafanyabiashara kwani kinatambulisha bidhaa yako ilipotengenezwa na
kupata msamaha wa kodi ya forodha inapoingia nchi nyingine za EAC.
Mradi
mwingine unaofadhiliwa na TMEA huko Zanzibar ni ule wa kuwasilisha
malamiko kwa njia ya mtandao au ujumbe mfupi wa simu pale inapotokea
mfanyabiashara amekumbana na vikwazo visivyo vya forodha katika
kusafirisha bidhaa zake ndani ya Jumuiya. Ujumbe huo utakapopokelewa,
kikwazo kilicholalamikiwa kitafanyiwa kazi na taasisi husika mara moja.
Benki
ya dunia pia inaendesha mradi wa kutathmini utekelezaji wa Soko la
Pamoja kwa upande wa Zanzibar. Kama inavyotambulika soko la pamoja lina
vipengele vingi vikiwemo; usafirishaji huru wa bidhaa, huduma, mtaji na
watu. Hivyo kuna umuhimu wa kupima namna nchi wanachama zinavyotekeleza
vipengele hivyo.
Ushiriki
wa Zanzibar unapatikana pia kwenye uenyeji wa taasisi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Zanzibar imebahatika kuwa mwenyeji wa Kamisheni ya
Kiswahili ya EAC. Kuwa mwenyeji wa taasisi kuna faida kubwa zikiwemo
kujitangaza na ajira. Kwa upande wa ajira, Bw. Haji alisema sio tu
Wazanzibari wanafaidikia na ajira za Kamisheni ya Kiswahili, bali
wanapata ajira hata katika Sekretarieti ya EAC na kutolea mfano kuwa
Mhasibu Mkuu wa kwanza wa Sekretarieti hiyo alikuwa Mzanzibari.
Vile
vile, Zanzibar imekuwa mwenyeji wa vikao mbalimbali vya taasisi za
Jumuiya. Mwaka 2010 Mahakama ya Afrika Mashariki ilifanya kikao chake
Zanzibar, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) lilifanya kikao
chake Zanzibar mwaka 2016 na mwezi Agosti mwaka huu utafanyika mkutano
mkubwa wa masuala ya Kiswahili mjini Zanzibar. Aliendelea kusema kuwa
katika Bunge la EALA la kipindi hiki, Zanzibar ina wabunge watatu,
wawili wakitokea CCM na mmoja CUF.
Alihitimisha
mada yake kwa kuwasihi Wazanzibari waache fikra potofu za kujihisi
kubaguliwa badala yake waunganishe nguvu kuchangamkia fursa lukuki za
kibiashara zilizopo kwenye mtangamano wa EAC. Alisema Serikali ya
Zanzibar inashiriki katika kila jambo ikiwemo kushiriki mikutano ya
Marais. Mawaziri na Wataalamu ili kutetea maslahi ya Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 18 Mei, 2017
No comments:
Post a Comment