Uamuzi huo wa Rais Magufuli umekuja siku chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia kwa Katibu wake wa Itikadi na Ueneze, Humphrey Polepole kutangaza msimamo wa chama hicho kutaka viongozi walioshindwa kudhibiti mauaji ya raia katika Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji waondolewe.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kwamba nafasi ya Mangu, imechukuliwa na Kamishna Simon Sirro.
Taarifa hiyo, ilisema IGP Sirro anachukua nafasi ya Mangu ambaye atapangiwa kazi nyingine huku Sirro akitarajiwa kuapishwa leo Ikulu saa 3:30 asubuhi.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli inaacha maswali mazito na kuibuka kwa mjadala mkali katika mitandao ya kijamii kwa kuwaacha wasaidizi wa IGP akiwemo Naibu IGP, Abdulrahman Kaniki ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuliongoza Jeshi la Polisi.
Pamoja na hali hiyo kwa muda mrefu sasa tangu yalipoanza matukio ya mauji ya raia katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, Mangu hakuwahi kutoka hadharani na kueleza kwa kina hatua za kuzuia matukio hayo huku akiwaachia kazi hiyo wasaidizi wake.
Kitendo hicho kimekuwa kikitajwa kama moja ya sababu za kung’olewa kwa Mangu ambaye anatajwa kubakiza mwaka mmoja kabla ya kustaafu kwake utumishi wa umma ndani ya jeshi hilo.
Hata hivyo katika ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, aliyoifanya Mei 21, mwaka huu wilayani Kibiti bosi huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi anatajwa kutokuwepo hali iliyowaacha maofisa wa jeshi hilo kubaki na maswali.
Katika siku za karibuni IGP Mangu, amekuwa akilaumiwa kushindwa kutoa kauli yanapotokea matukio makubwa nchini.
Miongoni mwa matukio hayo, ni mauaji ya askari polisi wanane wilayani Kibiti mkoani Pwani ambayo kama mkuu wa jeshi la polisi, amekuwa tofauti na watangulizi wake ambao walikuwa wepesi hata kuzungumza na vyombo vya habari.
Itakumbukwa mwaka huu, Rais Dk. Magufuli alimpongeza Mangu kwa kuwasimamisha kazi polisi 12 waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Alitoa pongezi hizo wakati wa kuwapisha Mkuu wa Majeshi, Luteni Jenerali Venance Mabeyo.
“Naomba nitoe pongezi kwa mkuu wa polisi kuwasimamisha kazi wale polisi. Nikupongeze mkuu umefanya vizuri na umetoa heshima kwa nchi yetu, tembea kifua mbele.
“Katika vita hii ya dawa za kulevya hakuna cha mtu aliye maarufu atakayeachwa, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri, au watoto wa fulani ambaye akijihusisha aachwe.
“Hata angekuwa mke wangu Janeth, akijihusisha we shika tu, kwa sababu madhara ya dawa ya kulevya katika Taifa letu imefikia mahali pabaya, haiwezekani watu wawe wanauza kama njugu, sisi sote hapa tuliopo tunafahamu hii vita ni ya kila mtu,”alisema.
Mbali na hayo Mangu pia analaumiwa kwa kushindwa kudhibiti wimbi la mauaji ya wananchi wilayani Kibiti ambako hadi sasa kuna operesheni kubwa inayoendeshwa na Jeshi la Polisi.
Sirro IGP wa 10
Uteuzi wa Sirro, unafanya kuwa IGP wa 10 katika historia ya Tanzania. Waliotangulia ni Elengwa Shaidi, Hamza Aziz, Samson Pundugu, Philemon Mgaya, Solomon Liani, Harun Mahundi, Omar Mahita, Said Mwema na Ernest Mangu.
Mangu aliteuliwa kushika wadhifa huo, Desemba 30, 2013, baada ya kuteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, akichukua nafasi ya mtangulizi wake Said Mwema alieyestafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria.
Kabla ya uteuzi huo, Mangu alikuwa Mkurugenzi wa Inteligensia ya Jinai katika jeshi hilo.
UCHAPAKAZI WAKE
IGP Sirro amewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Mwanza na baadae kuhamishiwa makao makuu ya jeshi hilo.
Baada ya kuhamishiwa makao makuu mwaka 2012, Sirro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Tanzania, akiwa na cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP), ambapo aliongoza Operesheni Kimbunga ambayo ilikuwa anaondoa makundi ya wahamiaji haramu waliovamia katika mikoa iliyokuwa mipakani.
Januari mwaka jana, Sirro aliteuliwa kuwa Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, akichukua nafasi ya Suleiman Kova ambaye alistaafu baada ya kulitumikia jeshi hilo kwa miaka 40.
Pamoja na mambo mengine aliongoza operesheni ya kupambana na dawa za kulevya kwa kuwatia mbaroni watu maarufu wakiwemo wasanii.
No comments:
Post a Comment