Pages

April 20, 2017

TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE YAPIMA MOYO WA MTOTO ALIYE TUMBONI MWA MAMA YAKE


Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara nyingine tena imefanya upimaji wa moyo wa mtoto aliye tumboni mwa mama yake, kuchunguza magonjwa mbalimbali ya moyo.
Upimaji huo umefanywa katika taasisi hiyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI, Naiz Majani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Naiz amesema kuna faida lukuki iwapo mjamzito ataamua kufanya kipimo maalumu.
"Tunatumia Ultra sound kama kawaida kufanya kipimo hiki, lakini inakuwa ina tofauti kidogo... hatutumii mionzi yoyote, hivyo hakuna madhara anayoweza kuyapata mama au mtoto wake aliye tumboni," amesema. 

Ametaja faida hizo kuwa ni kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa na magonjwa ya moyo, na kuwaondoa kwenye masumbufu wanayoweza kuyapata kutokana na kuchelewa kupata matibabu.
"Kwa mara ya  kwanza tuliwafanyia kipimo hicho wajawazito 25 mwishoni mwa mwaka jana ambapo watano kati yao mimba zao zilikutwa na matatizo.
"Wajawazito hao wanatarajiwa kujifungua wakati wowote kuanzia sasa na watoto hao wataanza kufuatiliwa kwa ukaribu na kupewa matibabu ya haraka," amesema.
Amesema waliamua kuanza kufanya kipimo hicho baada ya kugundua watoto kadhaa hufikishwa katika taasisi hiyo wakiwa katika hatua mbaya kiasi cha wao kushindwa kuwapatia matibabu.
Amesema inakadiriwa katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini mmoja anakuwa amezaliwa na magonjwa ya moyo.
"Mwaka jana inakadiriwa walizaliwa watoto milioni moja, kwa msingi huo watoto wapatao 12,000 walizaliwa na magonjwa haya lakini tuliowaona kliniki yetu ni kati ya 700 hadi 750 pekee," amesema.

"Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo yanatakiwa kutibiwa mapema, lakini wanakuja umri umeshakwenda tunashindwa kuwasaidia," amesema.
Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi  amesema dhumuni kubwa la kuanzisha huduma hiyo ni kugundua matatizo hayo mapema.


"Tunahamasisha kina mama wajitokeze, Tanzania sasa imepiga hatua kubwa, tunafanya hivi kwa sababu asilimia 85 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji ni watoto.
"Na hawa ndiyo tunaowategemea kuwa Taifa la kesho, tusipowagundua na kuwatibu mapema maana yake ni kwamba watakuja kuwa mzigo kwa Taifa miaka ijayo," amesema.
Amefafanua kwamba miaka ya nyuma si  kwamba magonjwa ya moyo hayakuwapata watoto bali hayakuweza kugundulika kutokana na uhaba wa wataalamu, vifaa. 
"Watoto wengi walikufa kwa kile kilichoelezwa ama ni typhoid, nimonia au surua, leo hii wataalamu tupo, tulikwenda kujifunza kwa wenzetu katika nchi zilizoendelea ili tuisaidie nchi yetu, magonjwa yote ya moyo yanatibika," amesisitiza.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...