WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya
Viettel ya Vietnam inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya
mawasiliano vijijini ambao umefanikisha kuweka miundombinu ya mtandao wa
intaneti kwenye shule 417 hapa nchini.
Amesema
mradi huo ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia
2015-2017, umewezesha pia ofisi za Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali
za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi za Posta 68
kufikiwa na mtandao huo.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) Bungeni mjini
Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za
Serikali kwa mwaka 2016/2017 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka
2017/2018 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya
Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake ukiwemo Mfuko wa Bunge kwa
mwaka 2017/2018
Waziri
Mkuu amesema katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi zilizofanyika
kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano; Mradi wa Anuani za Makazi na Postikodi; na kuanzisha huduma
ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji wa huduma muhimu
katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na huduma za
kibenki.
“Sekta
ya mawasiliano inatekeleza Programu ya Miundombinu ya Kikanda ambayo
inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school), Mradi wa Video Conference
ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na ufungaji wa vifaa vya TEHAMA
katika mikoa 26 na taasisi za Serikali,” amesema.
Amesema
Serikali imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi taarifa na mifumo
ya Serikali (Government Data Centre) ambacho lengo lake ni kuimarisha
usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na uhakika wa upatikanaji
wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Akizungumzia
kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema Serikali inahamasisha
wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa
ili kujenga uchumi wa viwanda, na kwamba inatoa kipaumbele kwenye
viwanda vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini,
vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko hapa
nchini na nje ya nchi.
“Katika
kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda,
Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa nchini pamoja na
mashirika ya umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha mifuko ya
Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua,
kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo
mbalimbali nchini,” amesisitiza.
Ameyataka
mashirika ya umma yahakikishe kwamba mipango yao inaendana na
utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni
kujenga uchumi wa viwanda.
Akizungumzia
kuhusu juhudi za Serikali kupambana na rushwa, Waziri Mkuu amesema
Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala
uvumilivu na vitendo vya rushwa.
“Hatua
zilizochukuliwa kupambana na rushwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano
iingie madarakani Novemba, 2015 zimetambuliwa na mashirika ya Kimataifa
yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa duniani. Taarifa
ya Shirika la Transparency International kwenye utafiti wake kuhusu
mtazamo wa rushwa mwaka 2016, imeonesha kuwa viwango vya rushwa
vinaendelea kupungua hapa nchini,” amesema.
Akifafanua
zaidi, Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali
iliweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.75 kutokana na operesheni
zilizofanywa na TAKUKURU,
“TAKUKURU
imefanya uchunguzi wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali
cha Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea na mashtaka kwa majalada
104. Katika kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi
mpya 182, ambapo katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na hatia na
kuhukumiwa kifungo au kulipa faini. Kesi 407 zinaendelea kusikilizwa
mahakamani,” amesema.
Amesema
katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya
rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, kudhibiti
matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya fedha za
ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imefungua balozi mpya sita katika
nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Amesema
Balozi hizo zina kazi ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama
nchi yenye vivutio vingi vya utalii na rasilimali zinazoweza kutumika
kuvuta uwekezaji kutoka mataifa hayo ikizingatiwa utulivu na amani
iliyopo nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA, ALHAMISI, APRILI 4, 2017.
No comments:
Post a Comment