Rais
Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Kugharamia Fursa
za Elimu Duniani Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekamilisha ziara yake ya
kuhamasisha utekekezaji wa Ripoti ya Kamisheni hiyo ijulikanayo kama
'Kizazi Cha Elimu' (The Learning Generation).
Katika
ziara hiyo iliyomfikisha katika nchi 15, Rais Mstaafu Kikwete amekutana
na Wakuu wa Nchi 12 wa nchi za Uganda, Malawi, Msumbiji, Congo,
Tunisia, Ghana, Chad, Gabon, Ivory Coast, Namibia, Afrika Kusini na
Botswana. Aidha amekutana na Makamu wa Rais wa Nigeria na Mawaziri Wakuu
wa Ethiopia na Tanzania. Pamoja na viongozi wa nchi na Serikali, Rais
Mstaafu amekutana na viongozi wa Taasisi za Kikanda 3 ambao ni
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC).
Madhumuni
ya ziara hizo yalikuwa ni kufikisha ujumbe wa Kamisheni na Ripoti yake
juu ya umuhimu wa nchi za uchumi wa kati na chini (low and middle income
countries) kufanya mapinduzi makubwa ya elimu ili kukabiliana na janga
kubwa la elimu linaloinyemelea dunia.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya Kamisheni hiyo, ubora wa elimu inayotolewa na nchi
zinazoendelea za uchumi wa kati na chini ni ile ambayo imetolewa na nchi
zilizoendelea miaka 70 iliyopita. Aidha, nchi zinazoendelea ziko nyuma
sana katika vigezo vitatu muhimu vya elimu vya fursa ya kujiunga na
elimu (access to education), kumaliza elimu (completion) na ufaulu na
kuelimika (learning outcomes).
Vile
vile, Ripoti ya Kamisheni inaonyesha kuwa Barani Afrika ni asilimia 5 tu
ndio wenye elimu ya Chuo Kikuu na asilimia 20 ndio wenye Elimu ya
Sekondari jambo ambalo linafanya bara la Afrika kuwa 'Bara la Wahitimu
wa Elimu ya Msingi'. Hali hii ni ya kukatisha tamaa wakati ambapo nchi
za Asia za Japan, Korea Kusini na Thailand zikitazamia kufikia lengo la
asilimia 80 ya wanafunzi wake kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu ifikapo
mwaka 2050. Barani Afrika, inatarajiwa kufikia asilimia 15 tu ya
wanafunzi wake, ambapo asilimia 10 kati ya hiyo ni Afrika ya Kaskazini
na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kubakia na asilimia 5 tu.
Kamisheni
inatahadharisha kwamba endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa,
inakisiwa kuwa ifikapo mwaka 2030, watoto milioni 160 barani Afrika
watakuwa nje ya mfumo wa Elimu wakati ambapo, Dunia imeazimia kupitia
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kuwa ifikapo mwaka 2030 pasiwepo na
mtoto aliyeachwa nyuma. Aidha, stadi zinaonyesha kuwa mapinduzi ya
teknolojia yatafuta ajira zipatazo bilioni 2 duniani ambapo asilimia 70
ya ajira hizo ziko barani Afrika. Bila kuwekeza katika Elimu, Bara la
Afrika halitakuwa na nafasi huko tuendako.
Kamisheni inapendekeza nchi zinazoendelea kufanya mageuzi katika mifumo yao ya elimu kwa kufanya yafuatayo:
1. Kuongeza Ufanisi kwa kuhimiza usimamizi mzuri na kuziba mianya ya rushwa na upotevu katika mfumo wa elimu;
2.
Kupanua fursa za elimu kwa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bila
kujali jamii anayotoka, jinsia au ubaguzi wa aina yoyote;
3.
Matumizi ya Teknolojia na mbinu bora za kitafiti za utoaji wa elimu
ikiwemo kuainisha mitaala iendane na mabadiliko ya dunia; na
4.
Kuongeza uwekezaji wa fedha katika elimu ili kuwezesha utoaji wa elimu
bora yenye kukidhi viwango na mahitaji ya sasa na baadae.
Katika
ziara yake katika nchi 14 zilizochaguliwa kuongoza mapinduzi ya elimu
(Pioneer Countries) za Botswana,Chad,Congo,Ethiopia,G abon,
Ghana,Ivory Coast, Malawi, Msumbiji, Nigeria,Namibia, Tanzania,Tunisia
na Uganda, Rais Mstaafu Kikwete ameridhishwa na jitihada na utashi wa
hali ya juu unaoonyeshwa na viongozi na serikali zao katika kupanua
fursa za elimu na kuinua hali ya elimu ya watoto wao. Changamoto kubwa
iliyoainishwa ni uwezo mdogo wa serikali hizo kugharamia kikamilifu
fursa za elimu. Tayari nchi hizo zinatumia wastani wa asilimia 18 hadi
20 wa bajeti zao katika elimu, na bajeti ya elimu ni kubwa katika nchi
zote alizotembelea. Imejidhihisha kuwa ni vigumu kwa nchi hizi kuvuka
ukomo wa bajeti huo bila kupata chanzo kingine cha fedha nje ya bajeti
zao.
Kwa
ajili hiyo, Kamisheni inaendelea na jitihada zake za kushawishi Jumuiya
ya Kimataifa kuongeza misaada na fedha za mikopo kugharamia elimu katika
nchi zinazoendelea. Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamisheni, fedha za
wahisani katika elimu zimekuwa zikipungua kutoka asilimia 13 mwaka 2003
hadi asilimia 10 mwaka 2013. Aidha, stadi imeonyesha kuwa fedha za elimu
zimekuwa zikipungua wakati ambapo fedha kwa ajili ya miundombinu na
afya zimekuwa zikiongezeka.
Kamisheni
ya Elimu inaendelea na jitihada za kushawishi nchi wahisani, mashirika
ya fedha ya kimataifa na washirika wa maendeleo kuongeza fedha na
uwekezaji katika elimu kwa manufaa ya dunia na kizazi kijacho. Lengo ni
kushawishi ongezeko la misaada katika elimu (ODA) kufikia asilimia 15
na fedha za mikopo kufikia walau asilimia 0.5 ya GDP zao ambayo ni sawa
na dola za kimarekani bilioni 50 ifikapo mwaka 2030.
Kwa
ajili hiyo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete amejumuika na Mwenyekiti
wa Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Uingereza
Mstaafu Gordon Brown kukutana na Mawaziri wa Fedha wa nchi 14 na Wakuu
wa Mashirika ya Fedha pembezoni mwa Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia
unaondelea jijini Washington D.C. kushawishi kutekelezwa kwa azma hiyo.
No comments:
Post a Comment