Na Jovina Bujulu MAELEZO Dar es Salaam
TAASISI
ya sekta binafsi nchini (TPSF) imetoa wito kwa wahitimu na vijana
waliopo vyuoni kuchangamkia fursa ya mpango maalum uliobuniwa baina yake
na Serikali ambao umekusudia kuwajengea ujuzi kabla ya kuajiriwa ili
waweze kufanya kazi kwa weledi.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF,
Godfrey Simbeye wakati alipokuwa akichangia mada kuhusu wahitimu wa vyuo
vikuu kushindwa kuonyesha ujuzi baada ya kuajiriwa.
“Upo
upungufu mkubwa wa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wengi wanaomaliza
vyuo vikuu nchini na imedhihirika kuwa wahitimu hao hushindwa kufanya
kazi kwa weledi wanapokuwa wameajiriwa na sekta mbali mbali.
Alisema
kuwa mpango huo maalum umeanzishwa kwa lengo la kuwatayarisha wahitimu
wa vyuo kupata mafunzo ya muda mfupi ili kuondoa changamoto
wanazokabiliana nazo pindi wanapoajiriwa au kutaka kujiajiri.
Simbeye
alisema Mpango huo pia umekusudia kuwapunguzia gharama waajiri, hasa wa
sekta binafsi kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kwa
kuwapeleka waajiriwa wapya katika mafunzo ili waweze kumudu kazi zao.
Akifafanua
zaidi alisema katika mpango huo waajiriwa wataweza kupata mafunzo
mtambuka na gharama zote za mafunzo zinagharimiwa na Serikali.
“Chini
ya mpango huu, wahitimu na vijana walioko vyuoni wanatakiwa
kujiandikisha kwa hiari, na baada ya mafunzo inakuwa rahisi kwao kupata
ajira kupitia katika sekta binafsi au makampuni” aliongeza Bwana
Simbeye.
Aidha
Bwana Simbeye alisema kuwa mpango huo pia utawawezesha wahitimu
kutengeneza mazingira ya kuanzisha biashara nyingi na kupanua biashara
zilizopo ili waweze kupata fursa nyingi za kuajiriwa na kujiajiri hasa
katika wakati huu ambao nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda.
Akizungumzia
mpango huo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana, na
Walemavu), Anthony Mavunde alisema kuwa mpango wa Serikali ni
kuhakikisha kuwa kila chuo kinajitengenezea mwongozo wake unaomwezesha
kila mwanafunzi kupata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo.
Aidha
aliongeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu na
unafanya kazi kama ilivyokusudiwa na kutoa wito kwa sekta binafsi na
waajiri kutoa maoni yao ili kuboresha mpango huo.
No comments:
Post a Comment