Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw.kailima Ramadhani akifungua
mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa
Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma.
Baadhi
ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya
jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea
uwezo wa kutekeleza majukumu yao wakati wa Uchaguzi mdogo utakaofanyika
Januari 22, 2017 leo mjini Dodoma. Picha na Aron Msigwa - NEC
Na. Aron Msigwa - NEC
TUME
YA TAIFA YA UCHAGUZI imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa
Uchaguzi mdogo wa Udiwani utakaofanyika katika Kata 20 za Tanzania Bara
na Ubunge katika jimbo la Dimani Visiwani Zanzibar Januari 22, 2017
kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ili Uchaguzi huo uwe Huru na wa
Haki.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Bw. Kailima Ramadhan wakati akifungua mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa
Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na
Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi
Kailima amewataka Wasimamizi hao kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria,
Kanuni na miongozo mbalimbali katika kushughulikia mambo
yatakayojitokeza wakati wa uchaguzi huo.
Katika
kutimiza majukumu yao wawe tayari kutoa ufafanuzi juu masuala
mbalimbali kwa kuzingatia sheria na kutokuwa tayari kukubali kuyumbishwa
na mtu yeyote atakayekiuka miongozo, sheria na kanuni za Uchaguzi.
Amewataka
Wasimamizi hao watende mambo yote kwa kuzingatia kanuni na Sheria na
kutoa maamuzi sahihi kwa mustakabali wa Taifa na kuwasisitiza kuepuka
kutoa upendeleo katika maamuzi wanayoyafanya na wasikubali kuyumbishwa
na matakwa ya baadhi ya watu.
Amewaeleza
kuwa milango ya Tume iko wazi pale watakapohitaji ufafanuzi huku akitoa
wito kwa Wasimamizi hao kuwasiliana na watendaji wa Tume katika mambo
yanayowatatiza ili wapate ufafanuzi.
Aidha,
amewataka wawe makini na hatua ya utangazaji wa matokeo kwa kutoa
taarifa kwa wananchi mara kwa mara juu ya hatua zinazoendelea vituoni
wakati wa ukusanyaji wa matokea ili kuwaondolea wasiwasi pindi wanapoona
matokeo yamechelewa kutolewa.
"
Hili naomba nilisisitize, mnapoona baadhi ya taratibu hazijakamilika
tokeni nje muwaambie wananchi nini kinaendelea ili wawe na taarifa na
hii itawaongezea imani wananchi wanaosubiri matokeo na kuepusha vurugu
vituoni" Amesisitiza Bw.Kailima.
Amesema
kuwa mfumo wa Uchaguzi wa Tanzania ni wa uwazi kwa kuwa kila chama
kinakuwa na Wakala anayesimamia maslahi ya chama chake wakati wa
uchaguzi, pia uwazi katika hatua zote za uchaguzi ikiwemo upigaji wa
kura, uhesabuji wa Matokeo na ujumlishaji wa matokeo ambayo
hulinganishwa na vishina.
Kwa
upande wa Mawakala wa Vyama vya Siasa watakaoshiriki katika Uchaguzi
mdogo amesisitiza kuwa wanatakiwa kuzingatia maadili ikiwemo kuepuka
kutoa matokeo ambayo hawajaruhusiwa kuyasema wakati wa zoezi la upigaji
wa kura na wanatakiwa kuapa kiapo cha kutunza siri na kujaza fomu kwa
mujibu matakwa ya kikanuni.
"
Wakala Chama cha Siasa haruhusiwi kutangaza matokeo kwa mgombea wake
wakati zoezi la kuhesbu kura likiendelea kituoni, na hili nalilisisitiza
Mawakala wote ni lazima waape kiapo cha kutunza Siri, ni matakwa ya
kikanuni, wakala asiyeapa na kujaza fomu asipewe ridhaa ya kuwa wakala
wa chama cha siasa ndani ya kituo" Amesisitiza Bw. Kailima.
Amesema
kila Chama kitakuwa na Mawakala wa aina tatu kwa maana ya Wakala wa
Kupiga kura, Wakala wa kuhesabu kura, Wakala wa kujumlisha kura na
Kutangaza Matokeo ambao watakua na jukumu la kulinda maslahi ya vyama
vyao na wagombea wawapo kituoni, kumsaidia msaidizi wa kituo pamoja na
kuangalia taratibu zinavyokwenda kituoni.
Amesisitiza
kuwa maamuzi ya kituo yatatolewa na Msimamizi wa kituo na Wakala ambaye
hatakubaliana na maamuzi hayo atajaza fomu namba 16 kuonyesha kuridhika
au kutokuridhika.
Kuhusu
mafunzo amesema yanalenga kuwajengea uwezo Wasimamizi wa Uchaguzi,
Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa
Uchaguzi kuelewa Misingi, Sheria na Wajibu wa namna bora ya kutekeleza
majukumu yao katika usimamizi wa hatua zote za uchaguzi ikiwemo upigaji
wa kura na utangazaji wa matokeo.
Ameongeza
kuwa Wasimamizi na Waratibu hao watafundishwa maadili ya kuzingatia
wakati wakitekeleza majukumu yao ikiwemo maadili ya uchaguzi,maelekezo
kwa wasimamizi ya Uchaguzi, wajibu wao, majukumu ya makarani , taratibu
za kupiga kura, kuhesabu kura, kujumlisha kura na kutangaza matokeo,
kuandaa taarifa za uchaguzi pamoja na masuala mbalimbali kuhusu uchaguzi
huo.
Akizungumzia
kuhusu Rufaa za mapingamizi ya wagombea amesema kuwa kwa mujibu wa
kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya
292, Tume ilipokea Rufaa za wagombea kutoka Kata mbalimbali ikiwemo ya
Kijichi - Manispaa ya Temeke, Misugusugu- Halmashauri ya mji Kibaha,
Pwani na Kata ya Ihumwa Manispaa ya Dodoma.
Amesema
katika kikao cha Tume cha Desemba, 30, 2016 Tume ya Taifa ya Uchaguzi
ilitoa maamuzi ya Rufaa zote kwa haki na kwa kuzingatia kanuni,
taratibu, miongozo na sheria zinazosimamia Uchaguzi ikiwemo Rufaa ya
Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambayo imeondolewa kwa
kuwa mkata Rufaa ameiondoa mwenyewe na amejitoa katika ugombea Udiwani
kabla Rufaa yake haijasikilizwa.
Kwa
Upande wa Rufaa ya jimbo la Dimani, Zanzibar Bw. Kailima ameeleza kuwa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 40 (6) ilipokea
Rufaa ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi ya kupinga maamuzi ya Msimamizi
wa Uchaguzi wa jimbo hilo kumthibitisha mgombea wa Chama cha Wananchi
CUF kwamba ni mgombea halali katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani,
Zanzibar.
Bw.
Kailima ameeleza kuwa katika kikao cha Maamuzi cha Tume cha kupitia
Rufaa za wagombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikubaliana na Uamuzi wa
Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kuwa mgombea wa Chama cha Wananchi
CUF aliyewekewa pingamizi na mgombea wa CCM amekidhi vigezo na uteuzi
wake ni halali hivyo anaweza kuendelea na kampeni za kugombea nafasi ya
Ubunge katika jimbo hilo.
"
Napenda nisisitize kuwa maamuzi yote yaliyofanywa na Tume yamezingatia
Kanuni, Taratibu, Sheria na miongozo inayosimamia chaguzi, hali hii ya
wagombea kukubali maamuzi ya Tume inatujengea msingi imara wa kuendelea
kufanya vizuri zaidi kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 huku
tukitimiza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria bila kupendelea"
Amesisitiza Bw.Kailima.
No comments:
Post a Comment