Pages

December 12, 2016

Tume ya Mipango yatembelea eneo la Likong’o Mkoani Lindi kitakapojengwa Kiwanda cha kuchakata Gesi Asilia

Na Adili Mhina, Lindi.

Kaimu Katibu Mtendaji, Wizara ya Fedha na Mipango upande wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri amefanya ziara katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Gesi Asilia lililopo katika mtaa wa Likong’o Manispaa ya Lindi na kushauri uongozi wa Manispaa hiyo kuongeza  juhudi za kuhakikisha wananchi waliopisha mradi huo wanalipwa fidia kwa wakati.
Mwanri alieleza kuwa ni vyema uongozi ukatilia mkazo umuhimu wa kuwalipa fidia wananchi ili waweze  kujiletea maendeleo yao kwa kuwa hawawezi tena kuendelea kutumia eneo hilo.
Alieleza kuwa dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda inaenda sambamba na kuwajali wananchi wake kwa kutoa fidia kwa mujibu  kanuni na sheria pale wanapolazimika kuachia  maeneo yao ili kupisha miradi ya maendeleo.
Mwanri aliongeza kuwa pamoja na kuwa mradi huo utakapojengwa na kukamilika utakuwa na faida kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla utasaidia pia kuinua kipato kwa wanachi wa Lindi kutokana na fursa mbalimbali za ajira zitakazojitokeza kwa wakazi hao.
 Nae Mtendaji wa Mtaa wa Ling’oko ambapo ndipo mradi huo unapotekelezwa, Bw. Jacob Anton alieleza kuwa wananchi wa eneo hilo wana matarajio makubwa na wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali kwa kuwa wanaamini ujio wa kiwanda hicho utasaidia kuboresha maisha yao.
Timu ya Ukaguzi wa Miradi kutoka Tume ya Mipango ikiongozwa na Naibu Katibu Mtendaji huyo, kwa sasa inaendelea na zoezi la ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara ambapo itatembelea miradi ya Serikali na ile ya sekta binafsi kwa lengo la kuhakikisha malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21) yanatekelezwa kwa ufasaha.
 Kaimu Katibu Mtendaji, Wizara ya Fedha na Mipango upande wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akikagua nyaraka mbalimbali ikiwemo ramani ya eneo litakalojengwa kujengwa kiwanda cha kuchakata gesi asilia katika eneo la Likong’o Mkoani Lindi. 
 Afisa Ardhi wa Manispaa ya Lindi, Bw. Munisi Andrew (aliyeshika nyaraka) akisikiliza maelekeza kutoka kwa Kaimu Katibu Mtendaji, Wizara ya Fedha na Mipango - Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri. Wengine ni maafisa wa manispaa hiyo pamoja na wataalamu kutoka Tume ya Mipango.
 Afisa Mipango Miji Manispaa ya Lindi, Bw. Ismaelo Chepa (mwenye t-shirt) akitoa maelezo juu ya ramani ya eneo la ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi. Pembeni ya Kaimu Katibu Mtendaji ni Mchumi Kuu kutoka Tume ya Mipango, Bibi Salome Kingdom.
 Mtendaji wa mtaa wa Likong’o , Bw. Jacob Anton akimwelezea Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri utayari wa wananchi wa eneo hilo katika ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata Gesi asilia. Kushoto (mwenye Tai) ni Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Lindi mjini Bw. Joel Kianza, Pembeni ya Kaimu Katibu Mtendaji ni Bw. Senya Tuni na Bibi Salome Kingdom wote wachumi kutoka Tume ya Mipango. 
 Kaimu Katibu Mtendaji, Wizara ya Fedha na Mipango - Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akiangalia eneo (hauonekani Pichani) lililotengwa kwa ajili ya Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia. 
Sehemu ya Eneo la ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata  gesi asilia. PICHA ZOTE NA ADILI MHINA, TUME YA MIPANGO

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...