WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
tayari imeshalipa sh. bilioni 722.7 kati ya sh. bilioni 964.2 za madeni
ya michango ya jumla ambayo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya
jamii nchini.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano
wa Sita wa wadau wa NSSF ulioanza leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC), Arusha na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya
600.
Amesema
sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015
hadi kufikia sh. trilioni 10.2 mwaka 2016. “Hadi kufikia Juni 2016,
takwimu zinaonesha idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia milioni
2.1. Rasilmali za mifuko zimefikia shilingi trilioni 10.28 na mafao
yaliyolipwa kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Juni 2016 ni shillingi
trilioni 2.93. Michango ya wanachama kwa mwaka ni shilingi trilioni 2.15
uwekezaji katika nyanja mbalimbali umefikia kiasi cha shilingi trilioni
9.29,” ameongeza.
Waziri Mkuu pia
amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Prof. Godius Kahyarara awaandikie barua waajiri wote wanaodaiwa
na shirika hilo na kuwataka wawasilishe fedha wanayodaiwa mara moja na
wale ambao hawatalipa ndani muda utakaowekwa wafikishwe mahakamani na
yeye apewe taarifa.
“Kumekuwepo
na changamoto ya muda mrefu ya baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa
wakati hali inayoleta usumbufu mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia
muda wa kustaafu. Suala hili halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa
waajiri wote nchini waheshimu sheria na wawasilishe michango yao kwa
wakati,” amesisitiza.
Mbali
ya kuwabana waajiri, Waziri Mkuu pia amewataka wanunuzi wa nyumba za
shirika hilo na wapangaji wote wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na
wasipofanya hivyo ndani ya muda uliopangwa wafikishwe mahakamani.
“Nimeambiwa
pia lipo tatizo la wadaiwa wa nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala
hili lilitolewa maelekezo na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na wenye Ulemavu. Nataka nisisitize kuwa watu wote walionunua
nyumba za NSSF na bado hawajakamilisha malipo na wale waliopanga lakini
hawalipi kodi wanatakiwa kulipa haraka au wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF
ziuzwe kwa watu wengine, vinginevyo nao wafikishwe mahakamani.”
Akizungumzia
utendaji wa shirika hilo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika
hilo na Bodi ya Wadhamini kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji
wa sukari nchini. Amesema kiwanda kitakachojengwa,
kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo
kuongeza wanachama katika mfuko wa NSSF.
“Nimefurahishwa
na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana ili kukabiliana na tatizo la sukari
nchini. Tumeelezwa hapa kuwa mashirika haya yatashirikiana kujenga
Kiwanda cha Sukari kitakachozalisha tani 200,000 kwa mwaka. Kiwanda
hicho kitajengwa katika eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,”
amesema.
Mapema, akielezea
utendaji wa shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius
Kahyarara alisema limeboresha mafao ya wanachama wake kutoka sh. 80,000
hadi sh. 100,000 kwa mwezi.
Alisema
limeanza kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga nyumba za watumishi
Dodoma ili kuendana na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma. “Upembuzi bado
unaendelea lakini tumeshabaini kuna uwezekano wa kujenga nyumba 200
hadi 300 mkoani Dodoma,” alisema.
Kuhusu
uwekezaji kwenye ujenzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere lililopo
Kigamboni, Dar es Salaam, Prof. Kahyarara alisema uwekezaji huo unalipa
kwa sababu makusanyo ya tozo kwa watumiaji yamefikia asilimia 109. “Tuna
uhakika kwamba fedha tulizowekeza zitarudi,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amepokea msaada wa tani 45 za
saruji ambazo ni sawa na mifuko 900 yenye thamani ya sh. milioni 15 kwa
ajili ya waathirika wa tetememo la ardhi mkoani Kagera. Amepokea msaada
huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Prof. Samuel
Wangwe.
Akiwasilisha
msaada huo, Prof. Wangwe alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani
Kagera na wameamua kutoa mchango ili kusaidia juhudi za Serikali
kukabiliana na maafa hayo. Pia alisema wamekamilisha ahadi yao ya
madawati 6,000 yenye thamani ya sh. milioni 400 ambayo waliitoa awali. Waziri Mkuu aliwashukuru kwa misaada hiyo na kuwahakikishia kwamba itafikishwa kwa walengwa.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki kuimba wimbo wa taifa kabla ya
kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki kuimba wimbo wa taifa kabla ya
kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo.
Wabunge
Aesh Hilaly wa Sumbawanga Mjini na Mohamed Mchengerwa wa Rufiji
wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majliwa wakati alipofungua Mkutano wa
Sita wa Wadau wa NSSFmjini Arusha Oktoba 20, 2016.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama akizungumza kabla ya
kumkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufungua Mkutano wa Sita wa
Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)
Oktoba 20, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipiga makofi baada ya kupokea tani 45 za saruji
zenye thamani ya shilinigi milioni 15 zilizotolewa na NSSF kabla ya
kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Meneja Mkuu wa Malipo wa Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO), Francis Mcharage cheti cha kuthamini michango
ya wafanyakazi wa shirika hilo kwa NSSF kila mwenzi wakati alipofungua
Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Watatu kushoto ni Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na wapili kushoto ni
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde. Kulia ni Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti
na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Irene Isaka baada ya
kufungua Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Kushoto ni Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde na kulia ni Mkuu wa mkoa wa
Arusha, Mrisho Gambo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment