Mwanasiasa apokosa jukwaa la kufanyia siasa hulegea na kulendemka mithili ya teja na alosto! Mwanasiasa afanye matukio bila kuonekana kwenye vyombo vya habari, huumia kwelikweli!
Hii ndiyo sababu wanasiasa hulogana kwa wale wenye imani za kishirikina. Hupandikiziana fitina kwa wenye hulka za ufitini. Wanasiasa huwaonea wivu na kutamani kuwashusha wenzao wanaong’ara.
Ukitaka kujua kuwa mamlaka yanalevya na siasa ni uteja, msome Rais wa Sita wa Marekani, John Quincy Adams, aliyeongoza kwa muhula mmoja tu, kati ya mwaka 1825 mpaka 1829.
Baada ya kushindwa kwenye uchaguzi na Rais wa Saba, Andrew Jackson, Adams alikuwa kama teja. Maisha nje ya ulingo wa kisiasa yalimtesa. Washington DC, alipaona pagumu mno. Akaamua kurejea nyumbani kwao kwenye mji aliokulia wa Quincy, Massachusetts.
Kabla ya kuondoka Washington, Adams alisema: “The sun of my political life set in the deepest gloom.”
Kiswahili: Jua la maisha yangu ya kisiasa limewekwa kwenye giza totoro.
Alikuwa mwenye huzuni sana. Hata baada ya kufika Quincy, aliona bado hawezi kuishi nje ya siasa, akaamua kugombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, akashinda. Rais kwenda kuwa mbunge, hiyo ndiyo tabia ya mwanasiasa anapolewa. Mwanasiasa lake ni jukwaa, akilikosa ni kama teja.
Adams alishika vyeo vingi kabla hajawa rais lakini hakuridhika, alitaka aendelee kuongoza.
Alishika nafasi mpaka ya Uwaziri wa Mambo ya Nje lakini hakutosheka. Na alishinda ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, aligombea tena na tena kabla ya kufikwa na mauti mwaka 1848, tena akiwa bado mjumbe!
Alifikwa na mauti akiwa na umri wa miaka 80. Akiwa anaugua kiharusi, aliuona kabisa mwisho wake, akasema: “This is the end of earth, but I am content.”
Kiswahili: Huu ndiyo mwisho wa dunia, lakini nimeridhika.
Kwamba kutokana na ulevi wake wa vyeo, alipokuwa anakaribia kufa, aliona kama ndiyo na dunia inakwisha. Tangu mwaka 1848, dunia bado ipo!
No comments:
Post a Comment