Pages

August 4, 2016

MAALIM SEIF AZUNGUMZA NA WAZANIBARI BOSTON, SEHEMU YA TATU

Na Mwandishi wetu Boston
Karibuni tena wapenzi Wasomaji wetu. Hii ni sehemu ya tatu ya mfululizo wetu wa "Maalim Seif azungumza na Wazanzibari Boston" katika mkutano wake na Wazanzibari uliofanyika katika jiji la Boston, Marekani 30 Juali 2016.
Maalim Seif akizungumza na Wazanzibari Boston Picha na (Swahilivilla.bog)
Katika sehemu iliyopita, Maalim Seif alielezea lengo la ziara zake za hivi karibuni katika mataifa mbalimbali Ulimwenguni. Kisha akaelezea historia ya migogoro visiwani Zanzibar, tangu enzi zile zinazoitwa za siasa mpaka kufikia Maridhiano yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo. Leo tunaendelea na sehemu ya tatu:
Amani na utulivu
Katibu Mkuu wa Chama Cha wanancni (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, aliendelea kwa kusema kuwa kufuatia maridhiano hayo, uhasama wa kisiasa na jazba zake vilitoweka, na watu wakawa wanaishi kwa amni na utulivu. Uchaguzi wa mwaka 2010 ukapita kwa salama na amani. 
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho kutokana na maridhiano hayo, ilikubaliwa kuwa Chama kitakachoshika nafasi ya kwanza katika uchaguzi kitatoa rais wa Zanzibar. 
Makamo wa kwanza atatoka katika chama kitakachoshika nafasi ya pili, wakati ambapo makamo wa pili atatoka kwenye chama kilichoshika nafasi ya kwanza.
Aidha kwa mujibu wa Katiba hiyo Wajumbe wa Baraza la Mawaziri walitakiwa watoke kutoka vyama vilivyopata uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi. 
"Baada ya uchaguzi tuliunda serikali ya Umoja wa Kitaifa kati ya CUF na CCM, huku CUF ikiwa na Mawaziri 7", alisema Maalim Seif.
Uchaguzi wa 2015
Uchaguzi wa mwezi Oktoba 2015 ulikuwa wa kihistoria. katika chaguzi zilizotangulia, ushindi ulikuwa kwa tofauti ndogo ya kura. Lakini katika uchaguzi wa 2015, CUF ilipata ushindi wa kishindo: "Tulishinda kwa zaidi ya kura 25,000" alijigamba Maalim Seif.
Alitoa siri ya ushindi huo kuwa ni maandalizi mazuri na chama kuwa madhubuti katika kulinda kura zao: "Tulijidhatiti kulinda matokeo yetu", alisisitiza.
Zoezi la kuhesabu kura lilienda vizuri mpaka tarehe 27 Oktoba ambapo zaidi ya 34% kwa upande wa uraisi zilikuwa zimeshahesabiwa, hapo mambo yakaanza kubadilika, na vituko kuanza. Kutokana na hali livyokuwa ikiendelea, Maalim Seif akaamua kuyaaanika hadharani matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa takwimu sahihi walizokuwa nazo.
Kwa upande mwengine, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bwana Jecha Salim Jecha alitoweka na hatimaye kujitokeza kwenye vyombo vya khabari vya serikali akitangaza kufutwa kwa uchaguzi.
"Walimamua kumwamuru Mweyekiti wa Tume ya Uchaguzi afute matokeo ya uchaguzi", alisema Maalim Seif. Kitendo hicho cha Mwenyekiti wa ZEC kilikwenda kinyume na Sheria na Katiba ya Zanzibar, kwani hakuna kipengele hata kimoja kinachompa mamlaka Mwenyekiti wa Tume kufuta uchaguzi.
"Hakuna kipengele hata kimoja cha sheria kinachoruhusu kufutwa kwa uchaguzi......., hakuna mtu au chombo chochote kinachoweza kufuta uchaguzi wa Zanzibar" Alisisitiza msomi huyo wa Sayansi ya Siasa. Aliendelea kusema kuwa kitendo hicho kiliingiza Zanzibar kwenye mgogoro wa kikatiba.
Baada ya kufutwa kwa uchaguzi. 
Kufuatia kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi kinyume na sheria, Maalim Seif aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa rais alifanya juhudi za kuwasiliana na rais wa Zanzibar wa wakati huo Mheshimiwa Ali Mohammed Shein ili wakutane na kujadili juu ya namna ya kuitoa Zaiznbar kwenye mgogoro huo wa kikatiba.
Baada ya majaribio kadhaa, hatimaye Dkt Shein akakubali kukutana naye na kuanza msusuro wa vikao vya mazungumzo vilivyowashirikisha pia Makamo wa Pili wa rais wa wakati huo Balozi Ali Seif Iddi pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar.
Wanasiasa hao waliendelea kujadiliana katika vikao vya faragha kwa wiki kadhaa huku 'drip' zikiwa zinamiminika mitaani mpaka wakafikisha jumla ya vikao nane bila mafanikio. Mazungumzo hayo yalivunjika baada ya Serikali kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio bila maafikiano ya vikao hivyo ambavyo bado vilikuwa vinaendelea.
Mbali na utata wa hatua ya Mwenyekiti ya kuufuta uchaguzi kinyume na sheria, tofauti nyingine zilizojitokeza katika mazungumzo hayo zilikuwa ni kurejewa kwa uchaguzi na uhalali wa kufanya hivyo kisheria, Tume itakayosimamia uchaguzi huo wa marudio; iwe ni ilele ya Mheshimiwa Jecha aliyevuruga mambo, iundwe Tume mpya au uchaguzi usimamwe na Tume huru ya Kimataifa?
Licha ya kutofikiwa kwa makubaliano kwenye mazungumzo hayo, 'serikali' iliendelea na mpango wake wa kufanya uchaguzi wa marudio. Tunasema 'serikali' kwa vile kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar serikali iliyoingia madarakani kufuatia uchaguzi wa 2010, ilikuwa imeshamaliza muda wake, na haikuwa na mamlaka yoyote ya kisheria.
Hilo alilisistiza kiongozi mwadilifu Maalim Seif kwa kusema kuwa Mawaziri wa CUF wakati huo tayari walikuwa wameshajiondoa kama inavyotakiwa na Katiba ya Zanzibar.
Maalim Seif alisisitiza kuwa kile kinachoitwa uchaguzi wa marudio hakikupata ridhaa ya wananchi, na vituo vya kupigia kura vilikuwa vitupu.
"Ni wapiga kura chini ya 15% tu ndio waliojitokeza kupiga kura, kinyume na 57% iliyotangazwa na serikali" alisema Maalim Seif na kusisitza: "Na kwa bahati walifedheheka, kwani Televisheni zilionesha vituo vya kupigia kura vikiwa vitupu"

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...