Na Mwandishi wetu Boston
Makamo wa Kwanza Mstaafu wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amemaliza awamu ya pili ya ziara zake za Kimataafa hapa nchini Marekani iliyoanza wiki mbili zilizopita.
Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na Wazanzibar
Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) alikamilisha ziara yake hiyo tarehe 30 Julai kwa kuzungumza na Wazanzibari kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Massachusetts.
Mgeni huyo rasmi alikaribishwa kwa risala ya Jumuiya ya Wazanzibari waishio katika jiji la Boston kulikofanyika mkutano huo, Bwana Mohammed Lali, iliyoelezea imani yao juu ya uongozi wa Maalim Seif katika mapambano ya kupigania haki sawa na demokrasia Visiwani Zanzibar.
Akijibu risala hiyo, Mwanasiasa huyo alielezea shukrani zake za dhati kwa imani ya Wazanzibari juu uongozi wake na kuwahakikishia kuwa haki yao itapatikana.
Madhumuni ya Ziara zake.
Maalim Seif, aliyekuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana, alielezea lengo la mizunguko yake hiyo kuwa ni kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi na taasisi alizozitembelea ili kuwapa picha halisi ya hali ya mambo ilivyo huko Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika nyanja za demokrasia na haki za binadamu kufuatia uchaguzi huo.
"Tumekuwa tukiwasiliana ili kuwapa 'brief' (maelezo) ya hali halisi ilivyo" aligogoteza Maalim.
Alisema kuwa nchi nyingi kwa kupitia Balozi zao zilikuwa zikitetea demokrasia, na wala siyo chama au kiongozi fulani.
"Nchi nyingi kwa kupitia Balozi zao zilikuwa zinatetea demokrasia, na wala siyo CUF wala Maalim Seif", alisema gwiji huyo wa siasa, na kuongeza kuwa, "Msimamo huo ndio uliotusukuma kutembelea nchi hizi ili kuwapa 'utandu na ukoko', kwani kwa kufanya hivi tunapata nafasi ya kukutana na watunga sera wenyewe"
Hii ni kutokana na kuwa Mabalozi wanafanya kazi kutokana na maagizo ya viongozi wa nchi zao, "na kama hamkujikaza swala hili linaweza kusahaulika", alisistiza.
Migogoro ya Zanzibar.
Katika mkutano huo, mwanasiasa huyo mkongwe alielezea kwa mukhtasari juu ya historia ya migogoro visiwani Zanzibar kwa kusema kuwa migogoro visiwani humo ni tofauti na migogoro katika nchi nyengine ambako huwa inajikita katika misingi ya ukabila au udini. lakini swala la ukabila au udini haliko Zanzibar licha ya kuwa 97% ya watu wake ni Waislamu.
"Mgogoro zaidi ni wa kisiasa tangu zama hizo zinazoitwa za siasa", alifafanua mweledi huyo, na kuongeza: "Baada ya kuanzishwa kwa vyama vya ASP, ZNP na ZPP, siasa iliwagawa Wazanzibari na baadaye yakaja Mapinduzi ya mwaka 1964"
Mapinduzi hayo yalikomesha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, na kuendelea na Chama kimoja mpaka vyama vingi viliporukhusiwa tena mwaka 1992. Hata hivyo Chama tawala kiliukubali mfumo huo kwa vile ulikuja kutoakana na wimbi la mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ulimwenguni.
"Baada ya kurejeshwa kwa shingo upande, waliukubali kwa shingo upande", alisema Maalim Seif aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Zanzibar, na kuongeza "Tulitukanwa na kufanyiwa mambo mengi hata kabla ya kuzaliwa kwa CUF"
Itakumbukwa kuwa Chama Cha Wananchi (CUF) kilitimiza masharti ya usajili wa muda mapema mara tu baada ya vyama vingi kurukhusiwa lakini kikapata wakati mgumu kupata uajili.
"Chama chetu kilitimiza masharti mapema, lakini kupata usajili ikawa nongwa", alisema Maalim na kusisitiza kuwa "Baadaye ikwa hawana budi kutupa usajili, na CUF ikapata usajili namabari mbili baada ya Chama Cha Mapinduzi - CCM"
Mara baada ya hapo zilifuata chuki na uhasama miongoni mwa wananchi badala ya kuwa kitu kimoja kama Wazanaibari. Chuki hizo na uhasama vikaendela na kufuatiwa na machafuka ya kisiasa kiasi kwamba kufikia mwaka 2001, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, Tanzania ikazalisha wakimbizi.
Itakumbukwa kwamba, wafuasi wa CUF walifanya maandamano mnamo mwezi wa Januari 2001, maandamano ambayo yalikabiliwa vikali na vyombo vya dola na kuplekea watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kulazimika kuihama nchi na kukimbilia nchini Kenya na Somalia.
Maalim Seif, anayesifika kwa busara na hekima, aliendelea kueleza kuwa hali ya uhasama ikaendelea kuvigubika visiwa hivyo vya marashi ya karafuu mpaka mwaka 2009, ambapo alikutana na Rais wa Zanzibar wa wakati huo Dakta Amani Karume na kufikia maridhiano ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema: "Hali iliendelea kuwa ya uhasama mpaka 2009 tulipokutana na Rais Karume na kufikia maridhiano yaliyoungwa mkono na Baraza la Wawakilishi na wanachi"
Itafaa kukumbusha kuwa tangu kufanyika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Zanzibar ilikuwa ikikabiliwa na migogoro ya kisiasa iliyofuatiwa na mazungumzo ya upatanishi yakizishirikisha pande mbalimbali za Kimataifa na kufikiwa miafaka tete ambayo ilivunjika mara tu baada ya chaguzi. Hata hivyo, Maalim Seif na Rais Amani Karume walikutana na kufikia maridhiano ya kizalendo ambayo hayakushirikisha upande wowote wa nje.
Maridhiano hayo yaliyotaka kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yalipitishwa na wananchi katika kura ya maoni na kuidhinishwa rasmi na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
No comments:
Post a Comment