Pages

March 15, 2016

WATUMIA JINA LA MKUU WA WILAYA KUTAPELI MILIONI 10

Arusha.Watu wasiojulikana wameingilia mawasiliano ya simu za mkononi za Mkuu wa wilaya ya Arusha,Fadhili Nkurlu na kuwatumia ujumbe mfupi watu walio karibu nae kwa kuwaomba fedha kati ya Sh 1 milioni hadi 2 milioni .

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake,Nkurlu alisema watu hao walikata kwanza mawasiliano kwenye simu zake mbili na baadaye  kusajili upya laini zenye majina yake kuanzia saa 10 jioni hadi jana asubuhi na katika kipindi hicho kifupi walikua wameshajipatia kiasi cha Sh 10 milioni.

"Mwanzoni nilidhani kuna shida ya mawasiliano kwasababu hakuna simu iliyokua inatoka wala kuingia,ilipofika saa tatu usiku nilijaribu kutumia simu nyingine mbali na mitandao ya Voda na airtel ninazotumia mara kwa mara ikafanya kazi na kumtaarifu mke wangu aliyeniambia simu zangu zilikua hazipatikani na baadhi yao walinijulisha kuwa wametumiwa ujumbe mfupi wa kuomba msaada wa fedha ,"alisema Nkurlu

Alisema baada ya kukutwa na hali hiyo anaamini kuna mawasiliano kati ya wahalifu wa mitandao na baadhi ya wafanyakazi kwenye makampuni za simu wasio waaminifu wanaotoa taarifa za undani za watu ambao anawasiliana nao mara kwa mara na namna walivyoweza kusajili upya namba bila kitambulisho.

Aliwaasa wananchi kuwa makini kwa kutokutoa fedha kwa wanaowatumia ujumbe mfupi hadi wazungumze nao na kujiridhisha kama ni kweli waliowatumia ujumbe ni watu halisi na kuepuka utapeli ulioshamiri nchini kupitia njia ya mitandao.

"Nalaani kitendo hiki kwa nguvu zote kwasababu hakiwezi kufanikiwa bila ushirikiano na wafanyakazi wa makampuni ya simu,sasa najiuliza fedha zetu ziko salama kiasi gani kwenye mitandao ya simu au wale wanaotumia huduma za benki kwa kutumia simu,"alihoji

Aliitaka mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA)kufanya uchunguzi wa kina kwenye makampuni ya simu ili kujiridhisha kama wafanyakazi hawashirikiani na wahalifu wa mitandao na kuweka sheria kali ya namna ya kukabiliana nao.

Baadhi ya waliotumiwa ujumbe wa kutaka fedha ni Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro,Hashim Mgandilwa aliyeombwa Sh 2 milioni na Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Yotham Ndembeka aliyeombwa Sh 1 milioni.

Ndembeka alisema baada ya kupata ujumbe huo alimwambia hakua na kiasi hicho lakini wahalifu hao walitaka atume kiasi chochote kwani kingerudishwa jana asubuhi kutokana na dharula aliyokua nayo.

"Nilimwambia Mkuu wa wilaya ninaenda nyumbani kwake kumuona uso kwa uso lakini alikataa akidai yuko kwenye kikao cha dharula,kila nilipojaribu kumpigia hakua anapokea simu nikafahamu hakua mtu sahihi ninayemfahamu,"alisema

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha,Liberatus Sabas alisema hakua amepata taarifa rasmi ya tukio hilo ofisini kwake.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...