Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma SACP Ferdinand Mtui
Askari nane wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kigona wakituhumiwa kwa
mauaji ya Erick Nilamewa (16) waliyemtuhumu kuwaibia simu moja aina ya
Techno na Sh. 6,000.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni Mtaa wa Mabatini Mwanga Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Wanajeshi
hao wakiwa nane, walionekana wakimpiga Nilamewa kwa mateke, fimbo na
kumchoma na pasi tumboni, kifuani na mgongoni, baada ya kumkamata
wakimtuhumu kwa wizi huo.
Mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni.
Aidha,
Ahamad Mussa, mkazi wa Mabatini eneo la Mwanga Manispaa ya
Kigoma/Ujiji, amelazwa wodi namba 7 katika hospitali ya Mkoa Maweni kwa
matibabu, kutokana na purukushani hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kigoma Ferdinard Mtui, alithibitisha kukamatwa kwa askari hao nane
wa JWTZ kwa tuhuma za mauaji ya kijana huyo na kumjeruhi Mussa (16).
Mtui
alisema “Ni kweli tunawashikilia wanajeshi nane na tunaendelea na
upelelezi, na baada ya uchunguzi tutawapeleka mahakamani ili sheria
iweze kuchukua mkondo wake.”
Akizungumza na Nipashe kutoka
kitandani alikolazwa, Mussa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza
katika Shule ya Sekondari Kitwe, alitumiwa ujumbe wa simu na wanajeshi
hao akiwa shuleni ambao walisema kwamba wanamhitaji.
“Baada ya
kutumiwa ujumbe huo mimi nilimbipu, akanipigia na kujitambulisha kuwa
yeye ni afande Aberi, akasema njoo mara moja nakuhitaji," alisema Mussa.
"Kwa sababu tunakaa mtaa mmoja, pia huwa naingiaga kwenye
makazi yao wanaponituma vitu mbalimbali kama sigara, sikuwa na wasiwasi
wowote kuhusu wito huo.”
Alisema alipofika alibisha hodi na
walimwitikia na kumwambia akae uani ndipo baada ya muda alitoka Aberi
akiwa amevaa kaptura ambaye alianza kuita wenzake ambao walianza
kumsulubu.
“Nilimsikia akiwaita wenzake wakina afande Mayowa,
Ally na wengine nimesahau majina yao lakini jumla walikuwa wanajeshi
nane ambao walikuwa wakinipiga.
"Waliniambia ninyooshe miguu
yangu juu ya ukuta na niliponyoosha walinipiga na ubao na fimbo ya
mianzi kichwani… damu zilianza kutoka.
"Wakachukua maji
wakasafisha, wakapiga tena kichwa nikaanguka chini kisha wakanipiga
mateke na kunichapa na nyaya za umeme huku wakiuliza ilipo simu na Sh
6,000 nilizoiba,” alisema Mussa.
Alisema wakati hali ikizidi
kuwa mbaya, "walichukua chupa ya pombe na kunimiminia" kabla ya
kujitokeza mwanamke mmoja wa nyumba ya jirani anayefahamika kwa jina la
mama Hoza ambaye aliwaambia wamwache "mtoto wa watu maana watamuua bure.
“Mimi sijaiba simu wala siku ya leo (jana) sijafika kambini hapo.
"Sijaiba
wao wakaendelea kunipiga na kunimwagia maji na kunigalagaza kwenye
mchanga wakati huo damu zinaendelea kuvuja kichwani, ndipo mimi
nikawambia naomba niende nyumbani nikamwambie mama yangu na tulienda na
mwanajeshi mmoja na tulipofika nyumbani tulimkuta mama yangu.
"Mwanajeshi
huyo akasimama nje mimi nikaingia ndani nikapita uani na kukimbia na
ndiyo ikawa pona yangu la sivyo na mimi ningefariki dunia.”
Alisema
baada ya yeye kukimbilia ndipo walipomkamata Erick mtaani na kumpeleka
kwenye makazi yao ambako walimpiga na kumtesa hadi walipoona hali yake
kuwa mbaya, walikwenda polisi kuchukua fomu namba 3 (PF3)kwa ajili ya
kumpeleka hospitali ya Maweni kwa matibabu, lakini alifariki dunia.
Mama
mzazi wa majeruhi huyo, Mwaisala Ahamad (36) alisema wanajeshi
walimuagiza mtoto mmoja kwenda nyumbani kwake kwamba wanamuitaji mtoto
wake na aliwaambia kuwa ameende shuleni.
“Waliniomba namba ya
simu ya mtoto wangu nikawapatia kwasabababu wanajeshi hawa walikuwa na
mazoea na mwanangu," alisema Mwaisala.
"Nilipowapa nilienda kwenye shughuli zangu kama kawaida sikuwa na wasiwasi wowote, hawa tunawajua.
"Wengine
wana nyota moja (luteni usu) na wengine mbili (luteni) na wengine tatu
(kepteni) na kutokana na vyeo walivyokuwa navyo sikutarajia mtoto wangu
yamkute yaliyomkuta.”
Aliongeza kuwa kama askari hao walihisi
kuwa mtoto wake ndiye aliyeiba simu yao walipaswa kumkamata na kumpeleka
kituo cha polisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Kigoma, Mshumbusi Edmond alithibitisha kumpokea marehemu Nilamewa
akiwa na majerahe kifuani, tumboni na mgongo lakini akafariki muda mfupi
baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
Mwili wake uko chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni, alisema.CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment