Pages

February 20, 2016

Besigye akamatwa tena na polisi Uganda

Besigye
Image captionDkt Kizza Besigye
Wanajeshi wa Uganda wakishirikiana na maafisa wa polisi wamevamia na kuzingira afisi za chama cha upinzani za Forum for Democratic Change (FDC).
Kiongozi wa chama hicho, Dkt Kizza Besigye, ambaye amekuwa akiwania urais amekuwemo ndani ya afisi hizo na mwandishi wa BBC Patience Atuhaire anasema polisi wameondoka naye akiwa kwenye gari lao.
Kituo cha televisheni cha NBS kimeripoti kuwa Besigye na rais wa FDC Mugisha Muntu wamekamatwa katika makao makuu hayo eneo la Najjanankumbi, na wafuasi wa chama hicho wakatawanywa kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.
Mgombea mwingine wa urais Amama Mbabazi amepakia video kwenye Twitter inayoonesha maafisa wa usalama nje ya nyumba yake. Anasema polisi wameanza kuwakamata watu nje ya nyumba yake.
Viongozi wa chama cha FDC walikuwa wakijiandaa kuhutubia wanahabari kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika jana.
Maafisa wa usalama wanashika doria kwa wingi maeneo yanayozunguka makao makuu hayo ya chama cha FDC, mwandishi wa BBC Catherine Byaruhanga anasema.
Milio inasikika ingawa haijabainika iwapo ni ya risasi halisi, risasi za mipira au mabomu ya kutoa machozi.
Hii ni mara ya tatu kwa Dkt Besigye kukamatwa wiki hii. Alikamatwa jana jioni katika kitongoji cha Naguru, mjini Kampala katika nyumba ambayo upinzani ulidai wizi wa kura ulikuwa ukifanyika.
Jumatatu, alizuiliwa kwa muda wakati akifanya kampeni mjini Kampala. Polisi walisema alijaribu kupitia barabara isiyoruhusiwa.
Chanzo BBC Swahili

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...