Pages

July 10, 2015

MBIVU MBICHI URAIS NDANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI CCM KUJULIKANA LEO


Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo inakutana kuchuja majina ya makada wake 38 waliorejesha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho na majina 33 ni lazima yapigwe panga ili kupeleka majina matano kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupigiwa kura.
Kwa mujibu wa habari kutoka mitandao ya kijamii, kwenye vijiwe na mijadala sehemu mbalimbali, majina hayo matano yanaaminika kwamba yatatoka miongoni mwa watiania 10 ambao wametajwa zaidi katika mijadala hiyo.
Sababu kuu mbili ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye mijadala hiyo na hata na baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa Tanzania ni mbili. Mosi, uzoefu wao ndani ya ungozi wa serikali na pili, nafasi yao ndani ya chama, ama kama wajumbe wa NEC au Kamati Kuu.
Majina ambayo yanatazamiwa kwamba yanaweza kupenya Kamati Kuu ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro; Waziri Mkuu Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya; Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani; Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli;.
Kwa ujumla kundi la makada hao (hapo juu) kila mmoja ana nafasi ya kupenya kwenye mchujo wa Kamati Kuu, lakini pia anakabiliwa na changamoto kadhaa.
BILAL
Dk. Bilal ni Makamu wa Rais, katika hali ya kawaida ni vigumu msaidizi namba moja wa rais aliyeko madarakani kukosa nafasi ya kupenya ngazi hiyo hata kama ni kwa sababu tu za kiprotokali .
Mbali na wadhifa wake, Bilal anayetoka Zanzibar amepata kuwa Waziri Kiongozi na ana uzoefu wa kuendesha serikali, kwa maana hiyo anawakilisha kundi la upande mmoja wa Muungano na hivyo siyo rahisi jina lake kutokuzingatiwa. Hata hivyo, Bilal ana changamoto ya umri kwani kwa umri wa miaka 70 alio nao sasa inakuwa ni kazi kubwa kukimbizana na changamoto za sasa katika nafasi hiyo.
LOWASSA
Lowassa ni mbunge wa Monduli, lakini pia alipata kuwa Waziri Mkuu hadi alipojiuzulu Februari 2008 kutokana na kadhia ya Richmond juu ya mkataba wa kufua umeme. Hata hivyo, kadri muda ulivyosonga hadi sasa kadhia hiyo ilikuja kujidhihirisha kusukumwa zaidi na misuguano ya ndani ya CCM hasa juu ya chuki za nafasi ya uwaziri mkuu.
Kama walivyo watia nia wengi, ni mjumbe wa NEC, amekuwa waziri katika serikali ya Mzee Ali Hassan Mwinyi na ya Rais Benjamin Mkapa, anaijua serikali vizuri.
Lowassa amekuwa gumzo kubwa miongoni mwa watia nia wote kiasi cha kuandamwa hata na wapinzani wake ndani ya chama kwa kuwa tu kila wakati kura za maoni zimeonyesha kuwa ni chaguo la kwanza la wananchi katika kundi la wawania urais wote, ndani ya CCM na hata ndani ya upinzani.
Mwanasiasa huyo ambaye wengi waliamini kwamba kadhia ya Richmond ilikuwa imemmaliza, aliigeuza hali hiyo kiasi cha kuonekana kuwa mtu anayestahili kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mvuto wake kwa wananchi wengi, umefanya wapinzani wake wajipange kumwandamana kwa tuhuma mbalimbali, ambazo amezipuuza.
Wakati wa mchakato wa kutafuta wadhamini ndani ya CCM, Lowassa alionyesha kwa vitendo halisi jinsi anavyoungwa mkono na wanaCCM wenzake, kwani mikutano yake iligeuka kuwa ‘mafuriko’ kila mkoa alikokwenda. Alidhaminiwa na wanachama zaidi ya laki nane.
Lowassa anaungwa mkono na wananchi wengi kwa sababu ni miongoni mwa viongozi wa serikali wachache ambao wanatenda kwa vitendo halisi kuliko kupiga kelele kwenye majukwaa ya kisiasa. 
Anakumbukwa kwa ufuatiliaji wa karibu kwenye kila wizara aliyokuwa, anakumbukwa kwa kusaidia Tanzania kunufaika na maji ya ziwa Victoria na wakati akiwa Waziri Mkuu alianza kubadili mfumo wa utendaji serikalini kutoka ‘business as usual’ na kuibua ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi miongoni mwa watumishi wa umma.
WASIRA
Wasira ni miongoni mwa makada wa siku nyingi wa CCM, amehudumu kama waziri katika serikali za awamu tatu, ya Mwalimu Nyerere; ya Mzee Mwinyi na ya awamu ya nne, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe, akiwa amejizolea umaarufu ndani ya CCM na hata kwenye upinzani kwani mwaka 1995 alihamia NCCR-Mageuzi na kugombea ubunge jimbo la Bunda na kumshinda, Jaji Joseph Warioba. Hata hivyo, baadaye mahakama kuu ilitengua ubunge wake na kumtia hatiani kwa kuhusika na vitendo vya rushwa katika uchaguzi.
Ingawa kiutendaji Wasira anaonekana kama mmoja wa watu wanaojituma, kitendo chake cha kuhama CCM na kurejea tena kinaweza kuwa moja ya sababu za kutumika dhidi yake.
MEMBE
Amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje tangu mwaka 2007 alipoondoka Dk. Migiro kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN). Membe aliingia bungeni mara ya kwanza mwaka 2000 wakati wa utawala wa Mkapa, lakini ni chini ya Kikwete alipata nafasi ya kuwa Naibu Waziri, akianzia Mambo ya Ndani na baadaye Nishati na Madini kabla ya kuibukia Mambo ya Nje kama waziri kamili.
Ni mjumbe wa NEC kama walivyo makada wenzake. Kwa miaka mingi ya utumishi wake Membe ambaye pia ni ofisa wa usalama wa taifa, alifanya kazi nje ya nchi. 
Duru za kisiasa nchini zinasema kuwa ingawa hana mizizi mirefu ndani ya chama, kukaa kwake wizara ya Mambo ya Nje kwa muda huo kumempa uzoefu wa uendeshaji wa serikali. Hata hivyo kumekuwa na maoni kuwa Membe anabebwa na wakuu serikalini.
MIGIRO
Huyu ni mwanamke pekee anayepewa nafasi ya kufika mbali miongoni mwa watia nia wote kwa sababu ya nafasi yake, kwanza ndani ya nchi na nje alipokuwa UN. Anaelezwa kuwa na uzoefu wa ndani na wa kimataifa.
Katika kipindi hiki ambacho Rais Kikwete amekuwa anatoa fursa nyingi zaidi kwa wanawake katika vyombo vya maamuzi, Dk. Migiro anaweza kupenya kwenye kundi la tano bora hivyo kusaka kura za NEC kama anataka kufika kwenye tatu bora kwenye mkutano mkuu.
PINDA
Huyu ni waziri mkuu tanu Februari 2008 alipojiuzulu Lowassa. Pinda amekuwa mbunge tangu awamu ya pili ya Rais Mkapa na kuwa waziri wa Tamisemi. 
Muda wake mwingi wa utumishi alikuwa ndani ya Ikulu kama ofisa wa serikali. Ni mwanasiasa ambaye kimsingi hajawa na kishindo sana licha ya nafasi yake kubwa ya uwaziri mkuu.
Pinda amekuwa miongoni mwa mawaziri wakuu wapole ambao hawajaacha kishindo kama alivyokuwa Waziri Mkuu pekee wa Rais Mkapa, Sumaye ambaye alikaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10, lakini hakuacha kishindo chochote pia.
Hata hivyo, kwa sababu za itifaki kama ilivyokwa Dk. Bilal, itakuwa ni vigumu kumpiga panga jina lake katika ngazi ya Kamati Kuu, ingawa wote umri nao umesogea, Bilal miaka 70 na Pinda miaka 67.
MWANDOSYA
Mwandosya ni mwanasiasa aliyeweka rekodi mwaka 2005 kwa kuingia tatu bora katika kinyang’anyiro cha urais, akiachwa nyuma na Kikwete na Dk. Salim Ahmed Salim. 
Amekuwa moja ya nguzo ya siasa ya CCM kwa miaka mingi na ndiye alianzisha mkakati wa harambee ya kuchangia chama kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. 
Amehudumu katika awamu mbili kama waziri, awamu ya tatu na ya nne. Kwa kitambo alikuwa ndiye nguzo ya wanaCCM mkoani Mbeya, lakini kuibuka kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, kama mmoja wa watia nia, kumeibua maswali mengi kama Profesa Mwandosya bado anashikilia nafasi hiyo Mbeya na kanda yote ya nyanda za juu kusini. Hata hivyo, umri wa miaka 66 wa Mwandosya siyo haba katika dunia ya leo inayohitaji mchakamchaka.
SUMAYE
Sumaye aliweka rekodi ya waziri mkuu aliyekalia kiti hicho mfululizo kwa muda mrefu zaidi ya mawaziri wakuu tisa kuwahi kuteuliwa tangu uhuru.
Hakuna ubishi kwamba Sumaye ana uzoefu wa kuendesha serikali, amekuwa naibu waziri, waziri na waziri mkuu kwa miaka 10. Alishikilia ubunge wa jimbo la Hanang hadi alipoamua kustaafu mwaka 2005 baada ya kuliwakilisha kwa miaka 20.
Ingawa Sumaye hana kikwazo chochote cha kisiasa kupenya hatua ya Kamati Kuu, nguvu zake za kisiasa jimboni kwake zimepungua ndiyo maana mwaka 2012 alibwagwa katika nafasi ya UNEC na Mary Nagu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahisiano na Uratibu).
MAGUFULI
Dk. Magufuli amekuwa ni miongoni mwa mawaziri wachache wachapakazi tangu awamu ya Rais Mkapa na hata sasa. Amekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na kisha Waziri wa Ujenzi wakati wa Mkapa na chini ya Kikwete amekuwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo, kisha wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kila alikopelekwa amejitahidi kuchapa kazi.
Ni kati ya mawaziri wanaozijua wizara na majukumu yao sawasawa, ni mfuatiliaji. Kwa utendaji huo, Magufuli amejijengea sifa ya kuwajibika kama kiongozi.
Hata hivyo, kuna jambo kubwa ambalo limekuwa likiibuka kila wakati juu ya kuhusika kwake na uuzaji wa nyumba za serikali. Ingawa inadaiwa kuwa ulikuwa uamuzi wa baraza la mawaziri, bado wananchi wengi wamekuwa wakihoji uamuzi wa kuuza nyumba hizo. 
Mbali ya kuwa mbunge wa Chato tangu mwaka 1995, Magufuli hajawahi kugombea nafasi nyingine ya kuchaguliwa ndani ya CCM. Siyo mjumbe wa NEC na hakuna kumbukumbu zozote kwamba alipata kuomba nafasi hiyo. 
POLISI WAMWAGWA DODOMA
Wakati Kamati Kuu  ikikutana leo, kufyeka majina 33 ya wagombea na kubakisha watano bora, Jeshi la Polisi linadaiwa kumwaga askari 200 wa kikosi maalum katika mji wa Dodoma kulinda usalama.
Askari hao wanaodaiwa kutoka mikoa ya Manyara, Singida, Iringa na Morogoro ni wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao walianza kuingia mjini hapa jana mchana, ukiwa ni mkakati wa jeshi hilo kuongeza nguvu za kukabiliana na jambo lolote la vurugu au uhalifu wakati wa vikao vya CCM ya uteuzi wa mgombea urais.
Wakati vikosi hivyo vikielezwa kuingia katika mji wa Dodoma kwa ajili ya kuongeza ulinzi, NIPASHE ilishuhudia Kikosi Maalum cha Askari wa Farasi kikirandaranda katika viunga vya mji huo.
Ulinzi katika mji wa Dodoma umeimarika zaidi baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwasili makao makuu ya chama kuanza kibarua kigumu cha kuiongoza Kamati ya Usalama na Maadili kuchambua kwa makini ubora wa wanachama walioomba uongozi ama wanaoteuliwa katika ngazi mbalimbali za chama kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alipotafutwa na NIPASHE kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala la ulinzi kuimarishwa, hakuwa tayari kulizungumzia akisema  kuwa ni masuala yanayohusu mambo ya ndani ya Jeshi la Polisi.
Kesho Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) itayapigia kura majina matano yatakayotoka Kamati Kuu na kupatikana majina matatu ambayo yatapelekwa kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa chama hicho kwa ajili ya  kupigiwa kura ili apatikane mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM kugombea urais dhidi ya vyama vingine vya upinzani.
WAANDISHI WA HABARI WAPATA WAKATI MGUMU
Waandishi wa habari wanaoripoti habari  kuhusu mfululizo wa vikao vya mchakato wa uteuzi wa mgombea wa CCM jana walijikuta katika wakati mgumu walipotakiwa na maofisa wa usalama kuondoka katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM.
Maofisa hao waliwataka waandishi hao kuondoka eneo hilo na kuwaacha wapiga picha pekee kuendelea kuwapo eneo hilo kwa madai kwamba hapakuwapo na hotuba wala mkutano wa aina yeyote ambao ungehutubiwa  na Rais Kikwete wala viongozi wa CCM Taifa.
Hata hivyo, maafisa hao wa usalama walishindwa kutambua kazi ya uandishi wa habari siyo kuripoti tu hutoba za viongozi bali pia mambo mengine ambayo wananchi wana haki kuyafahamu.
“Mtoke hapa, hamtakiwi waandishi wa habari. Watu waliopewa ruhusa ya kubaki eneo hili kwa muda ni wapigapicha peke yao na hata wao tutawaondoa. Halafu kuanzia sasa mkae sehemu moja na mnapotaka kuzungumza na mtu aliye nje ya uzio mtumie lango kuu kutoka nje na siyo kuzungumza nao mkiwa ndani ya ukuta na wao wakiwa ng’ambo ya barabara,” alisema ofisa mmoja wa usalama.
 WATA
TAKUKURU: HAKUNA ALIYEKAMATWA
Wakati mijadala mbalimbali ikiwa imetawala katika mitandao ya kijamii tangu juzi kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilikuwa imewanasa baadhi ya wapambe wa mgombea wa kiti cha urais, Makongoro Nyerere, wakiwa wanagawana fedha hotelini ili kuwashawishi baadhi ya wajumbe wa Nec na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kumchagua, Takukuru imekanusha taarifa hiyo kuwa si ya kweli.
Ujumbe huo kuhusu tuhuma za kukamatwa na rushwa kwa baadhi ya wapambe wa mgombea huyo, zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe wa Nec na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu pia waliokutwa hotelini humo (jina linahifadhiwa) wakiwa ndani ya chumba namba mbili wakipokea rushwa ya kati ya Sh. 100,000 na 500,000.
Mkuu wa taasisi hiyo mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga, aliiambia NIPASHE kuwa: 
“Natumia nafasi hii kukanusha habari hizo zilizotolewa kwamba si za kweli. Taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na habari za kukamatwa kwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi  Julai 7, mwaka huu ni uzushi.”
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi iwapo madai hayo yana ukweli, Makongoro Nyerere alisema: “Walioeneza uzushi huo wamenidonoa tu, hawajanigusa kwa namna yoyote. Hujuma zinafanywa na watu ambao sifa yao imeshatiwa doa kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.”
“Watu sasa wamekwama, wanataka ionekane kila mtu ndani ya chama anahusika na rushwa, wakati kila mtu anafahamu kuwa wanaoendekeza vitendo vya rushwa ni watu wachache sana.”
KINGUNGE AMVAA NAPE
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge-Ngombale Mwiru, amesema kauli zilizotolewa juzi na msemaji wa CCM, Nape Nnauye ni za kibabe na zinalenga kuwanyima watu haki zao kikatiba na kikanuni.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Kingunge alisema maneno yaliyotolewa juu ya kuteua bila kujali shinikizo la watu au kikundi na kwa sababu ya muda hautoshi, hakuna mgombea atakayeruhusiwa kukata rufaa yana utata na yamevuruga hali ya hewa.
Alisema kama CCM haijali shinikizo la watu ambao ni wanachama, inajali nini kwa sababu shughuli ya siasa ni kwa ajili ya watu.
“Wanasema sisi warithi wa Nyerere, lakini wazingatie Mwalimu alisema nini juu ya chama. Mwalimu Nyerere alisema chama chetu katika kutafuta wagombea, naongezea hasa wa urais, chama kisikilize watu wanasema nini, ” alisema Kingunge.
Aidha, alisema kama ingekuwa wakati wa Mwalimu Nyerere mtu wa aina hiyo angefukuzwa na kuvuliwa uanachama wake.
Alieleza katika chama hakuna mtu zaidi kuliko wengine, hivyo wajitahidi kulinda na kuhakikisha umoja na nguvu unaendelea kuwepo.
“Baadhi yetu tunatumia nguvu kubwa sana kupambana na wanachama wenzetu ukilinganisha na nguvu ya kupambana na wapinzani wetu. Ni hatari sana. Sisi sote tujirekebishe tusipoteze nguvu zetu,” alisema Kingunge.
Alibainisha kuwa CCM haiwezi kusimama inapopambana yenyewe kwa yenyewe na kwamba inaweza kutokomea baharini.
Alisema wakiwapuuza watu wanasema nini wakaishia kujifungia kwenye kamati na kuona wanatosha watambue kuwa hawatashinda.
Akifafanua kuhusu madai ya msemaji wa CCM kuhusu muda wa ukataji wa rufaa kuwa hautoshi, Kingunge alisema kauli hiyo ni ya ajabu ukizingatia ratiba ya uchaguzi mkuu inajulikana siku zote wakati chama hakijazaliwa jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...