Pages

April 24, 2015

Rais Uhuru Kenyatta akatisha safari Marekani kutokana na Mapigano yanayoendelea nchini Yemen


RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya, amelazimika kukatisha safari yake ya kikazi kuelekea Los Angeles, Marekani, usiku wa kuamkia Aprili 24, 2015, baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kushindwa kutua nchini Yemen kutokana na usalama mdogo uliosababishwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo.
Msemaji wa Ikulu ya Nairobi, Manoah Esipisu, amesema kutokana na sababu hiyo, Rais Kenyatta alilazimika kukatisha safari yake hiyo usiku huo huo na kurejea nchini kwake kwa ndege hiyo hiyo kabla ya kutua salama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Ikulu ya Kenya, katika safari yake hiyo, Rais Kenyatta alikuwa akitumia ndege ya Jeshi la Wananchi la nchi yake, na alitakiwa kutua kwanza katika jiji la Sana’a nchini Yemen, kabla ya kuunganisha safari yake hiyo kwa kutumia ndege ya kawaida ya biashara hadi Los Angeles.
Katika safari hiyo ya kikazi, Rais Kenyatta alikuwa anakwenda Marekani kuhudhuria Mkutano wa Kiuchumi na Uwekezaji, na kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na waandaji wa mkutano huo, alitarajia kuhutubia mkutano huo Jumatano ya Aprili 29, 2015.
Taarifa hizi za Rais Kenyatta kunusulika katika ajali hiyo ya ndege katika safari yake hiyo na kuamua kukatisha safari na kurejea nchini mwake, zimeandikwa pia na Rais huyo kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Aidha, taarifa hizo pia zimeripotiwa kupitia katika mtandao wa kijamii maarufu nchini wa JamiiForums na mmoja wa wanachama wake aliyejitambulisha kwa jina la Beth.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...