Bw. Mugusuhi Nyarusahe (39) aliyecharangwa kwa visu na wenzake.Stori:Gregory Nyankaira, Butiama/Risasi Mchanganyiko
MTU mmoja, Mugusuhi Nyarusahe (39) mkazi wa Kijiji cha Kinyambwiga wilayani Bunda, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara baada ya kucharangwa visu na wenzake tumboni, katika kile kilichodaiwa kuwa ni mzozo wa mgawo wa fedha zilizotokana na mauzo ya ng’ombe, tukio lililotokea wiki iliyopita. Nyarusahe ambaye ni maarufu kwa jina la Serikali, alipatwa na mkasa huo baada ya kuzuka ugomvi katika baa moja iitwayo Gateway Bar & Guest House iliyopo Kiabakari wilayani Butiama.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kundi la watu sita lilifika katika baa hiyo na kujitenga kando mishale ya saa 11 jioni na kuanza kuagiza vinywaji huku wakiwa na mazungumzo yao.
Ghafla, watu hao walianza kumwagiana pombe ovyo vichwani na kuzua taharuki kubwa kwa wateja wengine huku wakipasua chupa za bia na Mukebha Marwa alichomoa kisu kutoka ndani ya koti alilokua amevaa na kumchoma Mugusuhi na kusababisha utumbo kumwagika chini.
Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema watu hao walikuwa wakibishana juu ya mgawo wa fedha zilizotokana na mauzo ya ng’ombe wanaosadikika kuwa wa wizi.
Akizungumza akiwa hospitalini, Mugusuhi alisema ameanza kujitambua baada ya kuzirai tangu alipochomwa kisu na kwamba baada ya kukatwa utumbo mara tatu na kushonwa ameanza kupata nafuu “Mungu atanisaidia nitapona,” alisema.
Jeshi la polisi kupitia kwa msemaji wake Kamanda ASP Alex Kalangi limethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment