Dar es Salaam. Suala la Mjumbe wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Zakia Meghji kupiga kura upande wa Zanzibar wakati wa kupitisha Katiba Inayopendekezwa, limechukua sura mpya baada ya uliokuwa uongozi wa Bunge hilo kusema, “hakuna sehemu yoyote iliyobainisha kwamba alikuwa mjumbe kutoka Bara.”
Utata wa kura ya Meghji uliibuliwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba ambaye alisema mjumbe huyo alitakiwa kupiga kura upande wa Bara kutokana na Tangazo la Gazeti la Serikali namba 29 la Februari 7, mwaka huu lililomtambulisha Meghji kama mjumbe kutoka Tanzania Bara lakini katika upigaji kura alipiga upande wa Zanzibar.
Hatua ya mjumbe huyo kupiga kura upande huo wa muungano inachukuliwa na baadhi ya wanaopinga mchakato wa Katiba Mpya kama moja ya mbinu zilizotumiwa na uongozi wa Bunge Maalumu kulazimisha upatikanaji wa theluthi mbili ya kura kutoka visiwani ili kupitisha Katiba.
Hata hivyo, Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk Thomas Kashililah alisema jana kuwa: “Mnajichanganya tu, katika hilo tangazo la Serikali halikubainisha kwamba Meghji ni mjumbe wa Bara sisi tulichoangalia ni originality (asili) yake ni wapi hata kama anaishi Bara,” alisema Dk Kashililah na kuongeza: “Kama ndiyo hivyo, mbona Hamad Rashid anaishi Bara lakini asili yake ni Zanzibar? Mbona hilo hamuulizi? Hapo hakuna hoja kama wanatafuta kitu hicho hakipo.
“Katika Bunge hilo kulikuwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wajumbe 201 na wajumbe kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania... ieleweke kwamba mjumbe wa Baraza la Wawakilishi anaweza kuingia Bunge la Jamhuri lakini wa Jamhuri hawezi kuingia Baraza la Wawakilishi.”
Muda mrefu ambao Meghji amekaa Bara anaweza kufananishwa na ule ambao Mbunge wa Dole (CCM), Sylivester Maselle Mabumba ameishi Zanzibar lakini wakati akipiga kura kupitisha Katiba, asili ya Mabumba ambayo ni Bara haikuzingatiwa.
Taarifa katika tovuti ya Bunge zinaonyesha kuwa Mabumba alihitimu elimu yake ya msingi katika Shule ya Langoni, Dole – Zanzibar mwaka 1983 na mpaka sasa amekuwa akiishi Visiwani humo licha ya kwamba ni mzaliwa wa Kahama, Shinyanga.
Meghji alipopigiwa simu kuzungumzia suala hili, baada ya mwandishi kujitambulisha kwake alisema: “Unasema unaitwa nani, unasemaje”, kisha simu ikakatika na alipopigiwa tena alipokea lakini ilisikika sauti ikisema hasikii na alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakujibu.
Asili yake
Mjumbe huyo ni mmoja wa wabunge wa kuteuliwa na Rais katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na hakuna taarifa zozote zilizoambatana na uteuzi wake kuhusu ni upande upi wa muungano anakotoka. Taarifa rasmi zinaonyesha kuwa amekuwa akiishi mkoani Kilimanjaro ambako 1990 alikuwa mkuu wa mkoa huo, nafasi ambayo aliipata baada ya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi mwishoni mwa miaka ya 1980.
Meghji pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri akiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miaka tisa, Wizara ya Afya kwa miaka minne na Wizara ya Fedha kwa miaka miwili.
Wizara hizo mara kadhaa zimekuwa zikiongozwa na mawaziri kutoka pande zote mbili za muungano, lakini pia ni nadra kwa kiongozi kutoka Zanzibar kushika wadhifa wa mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya upande wa Bara.
Wasemacho wengine
Mratibu wa Mtandao wa Wanaopigania Haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa alisema kitendo kilichofanywa ni kuhalalisha uchakachuaji wa Katiba hiyo.
“Kama mtu ameteuliwa kutoka Bara hata kama ni Mzanzibari atatakiwa kupiga kura kama mtu wa Bara kwani kulikuwa na maana yake kuteuliwa upande mmoja.”
Mwanasheria Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema kuna vitu viwili vinatakiwa kutazamwa kwa makini; mosi ni uteuzi wake ulikuwa kutoka wapi na alipiga kura kama mjumbe wa wapi.
“Kama aliteuliwa kama mjumbe wa Tanzania Bara alitakiwa kupiga kura kama mjumbe wa Bara na kama aliteuliwa mjumbe wa Zanzibar angepiga kura kama Mzanzibari na si kuangalia asili yake na hili halina hata haja ya kuumiza kichwa kwani linaeleweka alipoteuliwa ndipo huko atapigia kura,” alisema Sungusia.MWANANCHI
No comments:
Post a Comment