Shirika
la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeahidi
kuendelea kuzisaidia redio jamii kwa lengo la kuhakikisha sauti za
wanyonge zinapazwa na kusikika ili kukuza demokrasia nchini.
Mwalikishi
wa shirika hilo ambaye pia ni mshauri na mkufunzi wa redio jamii Bi
Rose Haji Mwalimu aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Redio
Jamii cha Uvinza FM kilichozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni
Kanali Mstaafu Issa Machibya.
Bi
Haji alisema kwamba jitihada hizo ni kutokana na ukweli kwamba watu
wengi wanaishi vijijini ambako hawapati fursa ya kupata habari kwa
wepesi kwa ajili ya maendeleo yao kwa sababu wanaishi katika sehemu
ambazo hazifikiki kwa urahisi kutokana ya miundombinu duni ya
mawasiliano.
“Takwimu
zinaonyesha kwamba nchini Tanzania watu wenye uwezo wa kuangalia
telelvisheni ni asilimia 7 tu, kwa hiyo redio bado inachukua nafasi
kubwa zaidi ya upatikanaji wa taarifa kwa haraka, wepesi, urahisi na kwa
mapana zaidi,” alisema Bi. Rose Haji.
UNESCO
ni shirika la Umoja wa Mataifa ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitoa
msaada kwa redio jamii Tanzania katika kuzianzisha, kuzipatia vifaa na
kuzijengea uwezo kiufundi na mafunzo ili zijiendeshe zenyewe.
Redio
zilizoanzishwa na UNESCO ziko chini ya mtandao maalum ujulikanao kama
Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA).
Mkuu
wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akifanyiwa
mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji
wa kituo hicho, Kadisilaus Simon mara baada ya kuzindua rasmi redio
hiyo.
Mtandao
huo, hutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuharakisha maendeleo ya
wananchi na ushirikishwaji wa wananchi kupitia redio jamii hususan
matumizi ya Tehama, mchakato wa Rasimu ya Katiba, uchaguzi wa serikali
za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Takribani
Redio za Jamii zipatazo 30, ikiwemo ya Uvinza zinatekeleza mradi
maalum wa Uchaguzi unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
(UNDP) kwa kushirikiana na UNESCO, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bara na
Unguja (NEC na ZEC) na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini (RPP).
“Redio
zipatazo 30 zimeshapatiwa mafunzo yanayohusu maadili ya vyombo vya
habari, jinsia, na masuala ya jinsi ya kuandika habari za migogoro kwa
mtazamo chanya.
Viongozi
wa serikali za mitaa pia watashiriki katika mradi huu kuhakikisha
uhalali wa mradi huo, wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na makundi
maalum pia katika kuhakikisha mwendelezo wa utamaduni wa kuvumiliana,
kujadiliana bila kugombana ili kuwezesha uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa
amani na utulivu.
“Nina
uhakika kuwa ushirikiano huu utaendelea baada ya mafunzo haya na kwamba
redio jamii zitaleta mabadiliko makubwa kuhakikisha kuwa migogoro haina
nafasi katika jamii zetu. Vyombo vya habari vina wajibu wa kuhakikisha
kuwa vinaelimisha jamii juu ya athari za migogoro na kuhamasisha
utulivu, amani na uvumilivu katika jamii, ” alisema Bi. Rose Haji
Mwalimu.
Wakati
huo huo mwakilishi huyo wa UNESCO Bi Mwalimu ameuomba uongozi wa
halmashauri na wanajamii wa Uvinza kushirikiana na Redio Jamii Uvinza FM
katika mradi huu ambao utawanufaisha sana wanajamii wa Uvinza na
Kigoma kwa ujumla katika kuharakisha maendeleo.
Mtangazaji
wa kituo cha redio jamii Uvinza FM, Kadisilaus Simon akitekeleza
majukumu yake kwa furaha kabisa mara baada ya kupewa baraka na Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya.
“Redio
hii ni yenu sio ya Kalufya, yeye ameianzisha kwa ajili ya maendeleo ya
Uvinza, kitumieni, kitunzeni na mshiriki kikamilifu ili mpaze sauti zenu
kwa maendeleo yenu na kudumisha Amani, upendo na utulivu kuelekea
uchaguzi Mkuu mwaka 2015,” alisema Bi Mwalimu.
Nae
Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Bi. Hawa
Bayumi alisema kwamba Kampuni hiyo kwa kushirikiana na UNESCO bila
kujali biashara, imejikuta inalazimika kujihusisha na masuala ya
kijamii katika maendeleo kama shukrani za pekee kwa jamii kuruhusu
minara ya kampuni kujengwa sehemu zao.
“Ikiwa
ni njia ya kuishukuru jamii kwa kuiruhusu kampuni kujenga minara yake
sehemu zao za kuishi, njia pekee ni kutoa msaada kwa wanajamii hao
kuleta mabadiliko katika changamoto zilizopo ambazo ni umaskini,
unyanyasaji wa kijinsia, na imani potofu za kishirikina kwa kuboresha
miundombinu na mawasiliano”, alisema Bi. Bayumi.
Kwa
kupitia redio jamii Bi. Bayumi amesema changamoto hizo zitaisha kwa
kuhakikisha vipindi bora vinatayarishwa na kuhamasisha elimu kwa watoto,
afya masuala ambayo yanaipa kampuni ya Airtel alama kuwa ilichangia
maendeleo katika halmashauri ya Uvinza.
Kampuni
ya simu ya Airtel imeahidi kuendelea kushirikiana na asasi husika
hususan redio za kijamii kwa lengo la kukuza majadiliano ya kidemodrasia
nchini.
No comments:
Post a Comment